LATEST POSTS

Tuesday, July 21, 2015

UKWELI MAUAJI POLISI STAKISHARI

TAKRIBANI siku 9 tangu kutokea kwa uporaji wa silaha na mauaji ya askari wanne na raia watatu katika Kituo cha Polisi Stakishari jijini Dar es Salaam, moshi mweupe wa ukweli umenza kufuka.

Gaston polisi aliyenusurika.

Uchunguzi na vyanzo mbalimbali vya habari wakiwemo polisi ambao hawakutaka kutajwa majina yao, umesaidia timu ya waandishi wetu kubaini jinsi tukio hilo la kinyama lilivyofanyika.
“Wavamizi inaonesha walipanga zoezi hilo mapema, walijua wapi ghala la silaha lipo, walisoma pia mazingira ya ulinzi yalivyo pale kituoni nyakati za usiku,” polisi mmoja wa Stakishari aliyeomba hifadhi ya jina lake alisema.

UVAMIZI ULIVYOKUWA
Imeleezwa na mashuhuda wa tukio hilo kwamba majira ya saa 5 usiku, Julai 12, mwaka huu, watu zaidi ya 16 wakiwa na bunduki huku wakiwa wamevalia makoti meusi, walifika kituoni hapo kwa staili ya kutaka huduma lakini ghafla walifanya shambulizi la kushtukiza.
“Niliona pikipiki kama saba zinaingia eneo la kituo, nikadhani ni bodaboda wana shida kituoni, ghafla nikaanza kusikia milio ya risasi.“Nikakimbia kuelekea nyumbani kujifungia, baada ya hali kutulia nikarudi kituoni nikakuta askari na raia wameuawa,” alisema shuhuda wa tukio hilo ambaye hakupenda kutajwa jina lake.

POLISI, RAIA WALIVYOUAWA
Habari zinadai kuwa baada ya wahalifu hao kufika kituoni hapo, watatu kati yao walitengeneza mzozo wa kuigiza ili kuwahadaa askari waliokuwepo kituoni kuwa kufika kwao kulikuwa ni kupata huduma na siyo vinginevyo.
Inaelezwa kwamba wakati wahalifu hao wakizozana kuelekea mapokezi ya polisi, wenzao walitawanyika kuzunguka eneo lote la kituo kwa lengo la kudhibiti usalama.
“Askari mwenye silaha alikuwa mmoja pale kituoni, alipowaona wale watu watatu aliwauliza shida yao, kabla hajawajibu wakamfyatulia risasi zilizomjeruhi begani na kifuani.“Alipodondoka chini waliingia mapokezi, wakakuta polisi wawili na raia watatu, wakawaua wote kwa risasi.
“Askari wengine wawili waliwafuata vyumbani walikokuwa wamekimbilia kujificha, wakawaua, baadaye wakavunja ghala la silaha na kuiba,” chanzo chetu kilisema.


RAIA WALIFUATA NINI KITUONI?
Uchunguzi unaonesha kuwa raia watatu waliouawa katika tukio hilo, walikwenda kituoni hapo usiku kwa ajili ya kupata msaada wa polisi kufuatia tuhuma za kuibiwa kwa shilingi laki nne kwenye eneo walilokuwa wamekaa.
Inaelezwa kwamba, Jackline Mdume (marehemu) mkazi wa Manzese, Dar aliitwa na rafiki yake aliyetajwa kwa jina la utani la Mchakarikaji mwenyeji wa Tabata Kisukulu ili wakabadilishane mawazo ya kimaisha.
Akiwa na rafiki yake kwa mazungumzo, muuzaji wa vinywaji baridi aliyekuwa akiwahudumia, alilalamika kuibiwa kiasi cha shilingi laki nne ambapo mtuhumiwa wake mkuu alikuwa ni Jack.“Baada ya mzozo wa muda mrefu wakakubaliana waende polisi, Erick Swai (marehemu) alijitolea gari la kuwapelekea kituoni.
“Baadaye Swai akamuomba kijana mwingine (jina halikupatikana) amsindikize, wakamchukua na Jack. Mlalamikaji na mwenyeji wa Jack wakasema wataenda kwa usafiri wao, wakiwa kituoni ndiyo yakatokea hayo mauaji,” alieleza mtoa habari wetu.

 
ASKARI MAJERUHI AONGEA
Akiongea  na gazeti hili katika Hospitali ya Taifa  Muhimbili wiki iliyopita, askari aliyejeruhiwa katika tukio hilo la kikatili, PC  Gaston Shadrack alisema  kupona kwake ni  mipango ya Mungu.Akiongea  kwa masikitiko huku Mkuu wa Kituo (OCS) wa Stakishari akiangua kilio baada ya kumuona  askari wake aliyenusurika, Gaston alisimulia kuwa walitangulia watu wanne wakiwa  wamevaa makoti huku wakilumbana kama  watu waliodhulumiana.
Majeruhi huyo alipojaribu kuwahoji, ghafla  walichomoa silaha na kuanza mashambulizi makali.
“Mimi baada ya kupigwa risasi niliangukia tumbo hivyo walidhani nimekufa, hawakuhangaika na mimi tena, waliingia kituoni, wakaua askari wenzangu  pamoja na raia.
“Mmoja kati ya watu wale alikuja nilipokuwa nimeanguka, akanipiga teke, akawaambia wenzake ‘amekufa’, niliendelea kujilegeza huku nikiilalia bunduki yangu wasiione.
“Sikuwa na nguvu za kuinuka, walipomaliza uhalifu wao walitoka kwa tahadhari kubwa, niliendelea kutulia pale chini.
“Wakati wanaondoka pikipiki moja iligoma kuwaka, nikafyatua risasi mbili zilizompiga mmoja wao, akadondoka,” alisema PC Gaston.

 
WAHALIFU WALIONDOKAJE?
Habari kutoka eneo la tukio zinadai kuwa baada ya kufanya mauaji na kukusanya silaha, wahalifu hao walitoweka kupitia njia tofautitofauti.
Aidha, inadaiwa kuwa rundo la bunduki walizopora waliziingiza kwenye gari aina ya Toyota Noah la rangi nyeusi ambalo lilikuja na kuegesha karibu na kituo hicho.Inaelezwa kuwa mbali na bunduki, wahalifu hao walifanikiwa kuiba pia radio ya mawasiliano ya kipolisi (radio call) ambayo waliitumia kujua namna walivyokuwa wakifuatiliwa na vyombo vya usalama.

SILAHA ZINAZOIBWA ZINAPELEKWA WAPI?
Kitendawili cha wapi silaha zinazoibwa zinapelekwa na kwa kazi gani, bado hakijateguliwa ingawa yamekuwepo madai kuwa kuna kundi la watu ambalo linakusanya silaha hizo kwa lengo la kufanyia uhalifu mkubwa.

 
Baadhi ya wananchi ambao hawakupenda kutajwa majina yao, waliviomba vyombo ya usalama kuyachunguza mapori ya Kisarawe na Mkuranga, Mkoa wa Pwani na mkoani Morogoro kwa madai kuwa misitu hiyo inatumiwa na wahalifu kupata mafunzo na kuhifadhi silaha.
“Mambo mengine tunaogopa kuyazungumza waziwazi lakini serikali ikiamua kufanya uchunguzi kwenye misitu mikubwa pamoja na kufuatilia nyendo za baadhi ya mashirika ya dini, watabaini mambo mazito sana,” alisema mwananchi mmoja mkazi wa Kisarawe alipozungumza na gazeti hili.

FAMILIA ZA ASKARI WALIOUAWA ZANENA
Mke wa marehemu CPL Peter Sabuni mwenye namba E 1279, Mary Sabuni alishangazwa na mauaji ya mumewe huku akijiuliza kama ataweza kuwatunza watoto akiwa peke yake.“Nipo kwenye wakati mgumu, mtu niliyekuwa namtegemea ameuawa kinyama, sijui nitawalea vipi wanangu,” alisema Mary huku akiangua kilio.
Naye ndugu wa CPL Gaudiani Cyprian ambaye alijitambulisha kwa jina moja la David, alisema wamepata msiba mzito na ambao hauelezeki.“Nafikiri unajua kuwa baada ya msiba wa ndugu yangu kutokea, mama yetu alipopata taarifa alidondoka na kufariki dunia, hivi ninavyokwambia tuna misiba miwili mizito.”
Aidha mke wa SGT Adam Nyamuhanga mwenye namba D 69652, Jesca Adam alisema haamini kilichotokea, anaona kama ni ndoto ya mchana.“Mume wangu aliniaga anakwenda kazini atarudi kesho, mpaka usiku saa tatu siku ya tukio niliwasiliana naye, leo naambiwa ameuawa! Siamini,” alisema.
Naye mdogo wa marehemu H 1030, PC Antony Komu aliyejitambulisha kwa jina la ‘Komu Mdogo’ alisema amepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha kaka yake.“Kaka yangu alikuwa ndiyo kila kitu kwangu, ndiye alikuwa akinisomesha, sasa sijui nitasomaje, naona giza kwenye maisha yangu,” alisema.

KAMISHINA KOVA HUYU HAPA
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Kipolisi Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova wakati anawaaga wapiganaji hao, alisema: “Nakemea na kulaani kitendo hiki cha kinyama na tutahakikisha waliohusika wanakamatwa wote kwa muda mfupi. Pia tutahakikisha serikali inalipa mafao kwa kila askari  aliyepoteza maisha.”
 
OMBI KUTOKA KWA POLISI
Baadhi ya maofisa wa polisi wameiomba serikali kuangalia namna ya kuwasaidia watoto wa marehemu ili kuwawezesha kupata haki zao za msingi likiwemo suala la elimu.
“Tumesikia Kamishna Kova amesema atasimamia mafao ya marehemu, hilo ni sawa lakini waangalie jinsi ya kuwasaidia watoto hasa wale wadogo ambao wazazi wao wamepoteza maisha wakilitumikia taifa,” alisema polisi mmoja kwa sharti la kutotajwa jina lake.

Source: Global publishers

MAGUFULI AZOA WANACHAMA WAPYA MJI MDOGO WA MUGANZA WILAYANI CHATO, GEITA



   Mgombea Urais kwa chama cha Mapinduzi CCM, Dkt. John Pombe Magufuli akipokea kadi za Wanachama wa vyama mbalimbali vya upinzani na kujiunga na CCM, jana jioni katika viwanja vya Mji mdogo wa Muganza, wilayni Chato Mkoani Geita, Mh. Magufuli amezoa wanachama wapya waliorudisha kadi zao wapatao zaidi ya 150.
  Dkt. Magufuli akipokea kadi za Wanachama wa vyama mbalimbali vya upinzani na kujiunga na CCM. Mh. Magufuli yuko jimboni kwake Wilayani Chato kuwaaga na kuwashukuru Wananchi wake kwa kumpa ridhaa ya kuwaongoza kwa miaka 20 akiwa Mbunge.
   MKe wa Magufuli, Mama Janeth Magufuli akiwasalimia na kuwashukuru Wananchi wa mji huo kwa mapokezi mazuri na makubwa waliyoyapata wilayani humo.
  Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Ndugu Rajab Luhwavi akiwasalimia wanachama wa CCM pamoja na Wananchi waliofika kumlaki Dkt. Magufuli jana jioni.
   Mgombea Urais kwa chama cha Mapinduzi CCM,Dkt John Pombe Magufuli akiwapungia mkono pia na kuwashukuru Wananchi wake kwa kumpa ridhaa ya kuwaongoza kwa miaka 20 akiwa Mbunge wao. 
  Baadhi ya Wananchi wa Muganza wakishangilia kwa  furaha kubwa mara baada ya Dkt. Magufuli kujitambulisha kwao na pia kuwashukuru kwa kumpa ridhaa ya kuwaongoza kwa miaka 20 ya Ubunge ndani ya jimbo hilo.
Wananchi wa Muganza wakimsikiliza Dkt. Magufuli. 
  Baadhi ya Wananchi wa Muganza wakishangilia kwa  furaha kubwa mara baada ya ,Dkt. Magufuli kujitambulisha kwao na pia kuwashukuru kwa kumpa ridhaa ya kuwaongoza kwa miaka 20 ya Ubunge ndani ya jimbo hilo.
    ..Furaha ikitawala.
  Dkt. Magufuli akiwaaga na kuwashukuru Wananchi wake kwa kumpa ridhaa ya kuwaongoza kwa miaka 20 akiwa Mbunge wao.
  Mmoja wa Wafuasi wa chama cha Chadema Jumanne Majani akionekana kuwa na furaha ya kupitiliza mara baada kumuona Dkt. Magufuli, katika kijiji cha Kibehe alipokuwa akielekea Mji Mdogo wa Muganza kuwasalimia na kuwashukuru wananchi wa Mji huo.
  Mmoja wa Wafuasi wa chama cha Chadema Jumanne Majani akionekana kuwa na furaha ya kupitiliza mara baada kupewa ruhusa ya kusalimiana na Dkt. Magufuli, katika kijiji cha Kibehe.
Jumanne Majani alipopewa fursa ya kuzungumza chochote.
 Baadhi ya Wananchi wakiwa wameziba barabara wakitaka kumuona na kumsalimia Dkt. Magufuli ikiwemo pia kumpongeza kwa kuteuliwa kuipeperusha bendera ya CCM katika kuwania Uraisi kupitia chama hicho
  Wafuasi wa CCM wakishangilia mara baada ya kumuona Dkt Magufuli alipokuwa akipita kuwasalimia wananchi.
 Mmoja wa Wafuasi wa CCM akishangilia mara baada ya kumuona Dkt Magufuli.
 
Chanzo: Global publishers

Tuesday, July 14, 2015

MHE. MAGUFULI APOKELEWA KWA KISHINDO DAR, AHUTUBIA NYOMI MBAGALA

Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli na mgombea mwenza Mhe. Samia Suluhu Hassan wakiteremka kwenye ndege.
 
…Magufuli akisalimiana na wanachama wa CCM.
Ndege iliyombeba Mhe. Magufuli na Mhe. Samia kutoka Dodoma wakati ikiwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Makada na wanachama wa CCM wakijiandaa kuwapokea viongozi hao.
Magufuli akizungumza na wanachama pamoja na wananchi (hawapo pichani) waliojitokeza kumlaki uwanjani hapo.
Wanachama wa chama hicho waliojitokeza kumsikiliza kwenye Uwanja wa Zakheem, Mbagala jijini Dar.
Waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda hawakuwa nyuma katika shamrashamra hizo.

MGOMBEA wa nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Dk. John Pombe Joseph Magufuli, leo ametambulishwa rasmi kwa wakazi wa Jiji la Dar, ambapo amepokelewa kwa kishindo na makada wa chama hicho katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na kuelekea Mbagala - Zakheem ambako alizungumza na wakazi wa jiji la Dar. 

NABII AWALAZIMISHA WAFUASI WAKE KULA NYOKA AKIDAI CHOCOLATE


KATIKA hali ya kushangaza, nabii mmoja nchini Afrika Kusini ajulikanaye kwa jina la Penuel Mnguni, kutoka End Time Disciples Ministries, wikiendi iliyopita aliamua kuwalazimisha waumini wake kuna nyoka akidai kuwa amembadili nyoka huyo kuwa chocolate.

Nabii huyo alidai kuwa nyoka hawezi kumdhuru mtu yeyote anayemla na hiyo ni ishara kula tayari amebarikiwa. Tuna mamlaka ya kubadilisha kitu chochote na kitakubali maana tuna mamlaka tuliyopewa na bwana alieleza nabii huyo.

Sunday, July 12, 2015

Mgombea urais mteule John Magufuli amteua Samiah Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza

Mgombea urais mteule kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli amteua Samiah Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza  kwenye Uchaguzi  Mkuu 2015.
 Mhe. Samiah Suluhu Hassan


MAGUFULI NDIYE MGOMBEA URAIS WA CCM 2015






BUNGE wa Biharamulo Mashariki (CCM) na Waziri wa Ujenzi, Mhe. John Pombe Magufuli ameshinda katika uchaguzi wa kumpata mgombea urais wa CCM kwa mwaka 2015. Magufuli ameshinda baada ya kupata jumla ya kura 2104 sawa na 87.1%, Balozi Amina Salum Ali amepata kura 253 sawa na 10.5% na Dk. Asha-Rose Migiro 59 sawa na 2.4%.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Anne Makinda ndiye aliyepewa jukumu la kutangaza mshindi aliyepatikana kwa kura za Kikao cha Mkutano Mkuu wa CCM kilichofanyika kuanzia jana na kuendelea leo asubuhi mkoani Dodoma.
KURA ZILIZOPIGWA: 2422
KURA ZILIZOHARIBIKA: 6
KURA HALALI: 2416

Thursday, July 9, 2015

Kingunge amtolea uvivu Nape Nnauye

Mwanasiasa mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale-Mwiru 

 Mwanasiasa mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale-Mwiru amemshukia Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye kwa kauli zake alizodai zinaminya demokrasia na kwamba CCM haiwezi kusimama wanapopambana wenyewe kwa wenyewe.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Kingunge (pichani), ambaye hivi karibuni aliweka bayana kumuunga mkono Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa katika harakati zake za kuwania urais, alisema hakubaliani na kauli ya Nape kuwa wagombea wasioridhika na uamuzi wa Kamati Kuu (CC), hawawezi kukata rufaa kwa sababu ya muda kuwa mfupi.
Alisema CCM imeweka utaratibu wa wanachama kudai haki zao ndani ya chama, pindi wasiporidhishwa na uamuzi wa vikao vya chini.
Alisema mwaka 2005, mgombea wa nafasi ya urais, John Malecela alikata rufaa katika Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) baada ya jina lake kutopelekwa.
“Aliyekuwa mwenyekiti wa chama wakati ule Mkapa (Benjamin), alikubali baada ya kushauriana na wenzake kwa sababu haikuwa zawadi, bali ni haki yake,” alisema.
Hata hivyo, alisema baada ya kujielezea mbele ya NEC na wajumbe kuulizwa, walikubali kuwa majina matano yaliyoletwa na CC yanatosha.
“Kufikiria kwamba mtu akose haki kwa sababu ya kukosa muda huko ni kuwakosesha watu haki,” alisema.
Kingunge alisema amani na utulivu ni mambo yanayojengwa kwa haki na lazima imani ijengwe na viongozi.
Alisema lugha za kibabe ambazo zimekuwa zikitolewa na baadhi ya viongozi huku chama kikaa kimya ndizo zinazowatia watu shaka.
“Sasa hivi kumekuwa na nguvu kubwa ya kupambana ndani ya chama kuliko wapinzani… nyumba ikigawanyika haiwezi kusimama na CCM haiwezi kusimama inapopambana yenyewe kwa yenyewe,” alisema.
Alisema kukiwa kuna jitihada za kunyima haki watu, kunaweza kusababisha machafuko.
“Asitokee mtu akadhani kuwa nchi ni yake pekee yake, sitaki kusema kwa sababu matokeo yake mnayajua. CCM ni yetu sote hata sisi tuliokuwapo tangu zamani,” alisema. “Ukisema wagombea hawataweza kukata rufaa unapotosha misingi, kwa nini unataka kuminya haki hiyo sasa? Ingekuwa wakati wetu na Mwalimu (Julius Nyerere), mtu wa namna hiyo tungemvua uongozi.”
Hata hivyo, Nape alipoulizwa alisema hawezi kujibu tuhuma hizo kwa kuwa hajamsikia na anayetakiwa kuzijibu ni aliyempa kazi.
“Siwezi kujibu kwa sababu sijamsikia, sijui kasema wapi, amesema nini na kama amesema mimi siwezi kujibu mwenye wajibu huo ni aliyenipa kazi,” alisema Nape.

Dewji aaga Singida, aliza wapiga kura

Mbunge wa jimbo la Singida mjini akiwaaga maelfu ya wapiga kura wake wakati wa mkutano wa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya mwaka 2005/2010 na 2010/2015 ambapo pia alitangaza rasmi kutogombea tena jimbo la Singida mjini
 
Singida. Mbunge wa Singida Mjini (CCM) na mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji amewaliza baadhi ya wapigakura wake wakati akitangaza kutogombea tena nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu ujao kwa ya madai ya kubanwa na majukumu ya kifamilia na biashara.
Dewji ambaye amekuwa mwakilishi wa jimbo hilo kwa awamu tatu mfululizo, alitangaza uamuzi wake huo kwenye mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi.
Alisema kuwa aliomba ridhaa ya kuwatumikia wananchi wa Singida Mjini mwaka 2000, hakuwa na familia na pia biashara zake hazikuwa kubwa kama ilivyo sasa.
Alisema katika kipindi chote cha uwakilishi wake, wakazi wa Singida Mjini wamempa heshima kubwa, ukarimu wa hali ya juu, wema uliotukuka na uvumilivu usio na kifani na kwa hali hiyo, hatawasahau kamwe na ataendelea kuwatumikia kupitia mfuko maalumu aliouanzisha.
Aliwataka wakazi hao kuendeleza moto wa maendeleo waliouwasha miaka 10 iliyopita kwa miaka mingine kama hiyo ijayo ili jimbo hilo lipige hatua zaidi.
“Kwa kutambua heshima mliyonipa na imani kubwa mliyonionyesha kwa vipindi vyote vya uongozi wangu, ingawa nina huzuni lakini sina budi niwaombe kuwa mwaka huu wa uchaguzi sigombei tena na ninatoa fursa kwa kada mwingine wa CCM anipokee kijiti hiki kuliongoza jimbo letu,” alisema kwa huzuni. Baada ya kutamka maneno hayo, wananchi wengi katika walipiga kelele kwa nguvu wakionyesha kutokubaliana na uamuzi wake. Huku moja ya sauti ikisikika... “Hatutaki mbunge mwingine ni wewe tu hadi tukuchoke.”
Awali, Dewji alitaja baadhi ya maendeleo yaliyofanyika katika vipindi vyake, kuwa ni pamoja na kujenga shule 15 za sekondari kutoka mbili zilizokuwapo.
Alisema kwa kutumia fedha zake alijenga na kuchimba visima 45 vya majisafi na salama.

Wednesday, July 8, 2015

Mwisho wa vichwa 33 leo

 

Dodoma. Kisu kikali cha Kamati Kuu ya CCM (CC) leo kitaondoka na vichwa 33 kati ya 38 vya walioomba kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho kumrithi Rais Jakaya Kikwete anayemaliza ngwe yake.
Kikao hicho ni hatua ya pili baada ya kukamilika kwa kikao cha Kamati ya Maadili kilichokutana jana usiku chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete huku kikitawaliwa na usiri mkubwa, kuhama ukumbi na kila dalili za kubadili ratiba iliyopangwa awali ili kuvuruga mipango ya kambi za wagombea.
Habari zilizolifikia gazeti hili zilisema kulikuwa na uwezekano wa kubadili ratiba ili vikao vya Kamati ya Maadili na CC ama vifuatane au vifanyike usiku ili kuyanyima makundi nafasi ya kujipanga.
Alipoulizwa jana kuhusu vikao hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alidai kuwa hata yeye hakuwa na uhakika wa lini na muda gani hasa kikao cha Kamati ya Maadili kingefanyika.
Awali, vifaa vya ukaguzi wa wajumbe vilikuwa vimewekwa katika Makao Makuu ya CCM, White House lakini baadaye jioni viliondolewa na hapakuwa na taarifa zozote zilizotolewa.
Habari zilizopatikana baadaye zilidai kuwa kikao hicho cha Maadili kilitarajiwa kufanyika Ikulu ya Dodoma kuanzia saa nne usiku wa jana.
Haya yanajitokeza wakati macho na masikio ya Watanzania yakiwa hapa Dodoma kusikiliza namna kazi ya kuchuja wagombea itakavyofanyika na kujua ni watu gani 33 watakaoanza kulambwa na kisu cha CC, hasa kwa majina makubwa yanayotazamwa na wengi, mara tu baada ya kujadiliwa na Kamati ya Maadili.
Kazi za Kamati Kuu leo
Kikao cha CC kina majukumu matatu leo ambayo ni kufikiria na kutoa mapendekezo kwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), majina yasiyozidi matatu ya walioona kuwania urais wa Zanzibar ambayo imeombwa na Rais wa sasa, Dk Ali Mohamed Shein pekee, kufikiria na kutoa mapendekezo kwa NEC majina yasiyozidi matano ya walioomba kuwania urais wa Muungano na kuandaa mkutano wa NEC.
Vigezo vya maadili
Kulingana na kanuni za Uongozi na Maadili, toleo la 2012 kifungu cha 4(ii), kuhusu taratibu za kuomba uongozi, wanachama wanaogombea uongozi ambao uteuzi wao hufanywa na vikao vya kitaifa, watachunguzwa kwanza uadilifu wao na chombo cha maadili cha CCM kwa ushirikiano na vyanzo vingine.
Kanuni hizo zinasema mwanachama wa CCM anapoomba uongozi katika ngazi yoyote, itikadi na mwenendo wake vitachunguzwa kwanza na Kamati ya Usalama na Maadili inayohusika, ndipo maombi hayo yaliyoambatanishwa na mapendekezo ya kamati hiyo yatakapofikishwa mbele ya kikao chenye madaraka ya kutoa uamuzi.

Ikiwa mwanachama hakupendekezwa kwa sababu ya kukiuka Katiba ya CCM, Kanuni za CCM na sheria ya nchi, hatakuwa na haki ya kukata rufaa kwa mtu yeyote au kikao chochote. Lakini ikiwa mwanachama atakataliwa kugombea kwa sababu ya madhambi yake katika chama, basi ni wajibu wa Kamati ya Usalama na Maadili kumjulisha makosa yaliyomnyima haki ya kugombea, naye anaweza kukata rufaa kwa mujibu wa haki zake kikatiba.
Mtu yeyote anayetuhumiwa mbele ya Kamati ya Usalama na Maadili ya ngazi yoyote, kwa kosa lolote linalohusiana na maadili au nidhamu ya chama atasomewa na kutakiwa kuzijibu tuhuma hizo mbele ya wajumbe wa kamati hiyo ama kwa kauli yake mwenyewe au kwa maandishi, lakini hataambiwa nani aliyezileta tuhuma hizo, isipokuwa kama imekwishajulikana mapema kutokana na mijadala ya vikao, vyombo vya sheria au vyombo vya habari.
Kanuni ya maadili inaendelea kusema kuwa uchambuzi wa tuhuma hizo utafanywa kwa kutumia njia mbalimbali pamoja na mashahidi watakaopatikana.
Uchunguzi utakapokamilika na endapo itadhihirika kwamba tuhuma zina uzito, mtuhumiwa ataitwa mbele ya kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili ya ngazi inayohusika, kama ni lazima, ili apate kuhojiwa ana kwa ana.
Pia, kanuni inasema Kamati ya Usalama na Maadili ya ngazi inayohusika itatoa mapendekezo yake kuhusu suala hilo kwenye kikao cha uamuzi kinachohusika. Mtuhumiwa atapewa nakala ya uamuzi kwa maandishi.
Wagombea wanne kukosa CC
Katika kikao cha CC kinachofanyika leo, wajumbe wanne ambao ni miongoni mwa majina 38 yatakayojadiliwa katika mchujo huo watalazimika kukaa kando ili kukwepa mgongano wa masilahi.
Wajumbe hao ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Asha-Rose Migiro, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Ghalib Bilal na Waziri wa Kilimo na Chakula, Stephen Wasira.
Kwa mujibu wa Kanuni za Uteuzi wa Wagombea wa CCM katika Vyombo vya Dola, Toleo la Pili – Februari, 2005, ukurasa wa 25, kifungu cha 21 (3); wajumbe wa vikao vya uchujaji na uteuzi wa wagombea kwa ngazi inayohusika hawaruhusiwi kuendelea na kazi ya uchujaji na uteuzi iwapo wao ni wagombea katika ngazi hiyo.
Kanuni hiyo pia imetoa miiko ya shughuli za uchujaji na uteuzi wa wagombea na wajumbe wote wanatakiwa na kanuni kuzingatia maadili na nidhamu ya chama katika kusimamia na kutekeleza shughuli za uteuzi.
Kanuni hizo zinasema ni mwiko kwa kiongozi yeyote kwa maneno au vitendo kumpendelea au kumsaidia kupata kura nyingi mwombaji mmoja dhidi ya mwingine, kutumia au kuhusisha ukabila, dini, rushwa, rangi, hila na eneo analoishi au anakotoka katika shughuli yoyote ya uchaguzi.
Pia, ni mwiko kwa kiongozi yeyote au mwombaji yeyote wa nafasi ya uongozi au mwanachama yeyote aliyekabidhiwa dhamana ya usimamizi au uangalizi au uratibu wa kura za maoni, uchujaji na uteuzi, kufanya vitendo
Kuhusu misaada, kifungu cha tano (a) kinasema ni marufuku kwa mgombea yeyote mtarajiwa au wakala wake, kufanya vitendo vyovyote vinavyoonekana dhahiri kuwa ni sehemu ya kampeni za kuwania nafasi anayoitafuta kabla ya muda rasmi wa uongozi unaohusika haujamalizika.
Kanuni imetoa adhabu kwa watakaovunja miiko hiyo na kwa kiongozi atakayethibitika kuivunja atavuliwa uongozi na kwa mwanachama anayeomba kugombea nafasi yoyote atakayethibitika kuivunja hiyo hatateuliwa kugombea nafasi anayowania.

Chanzo: Mwananchi
vya ukiukwaji wa kanuni.

Wiki ngumu kwa CCM Dodoma

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakitafanya maamuzi yake kwa presha ya watangaza nia ya kutaka kuteuliwa kuwa wagombea wa CCM ili kupeperusha bendera ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu kwani mfumo wake wa kumpata mgombea uko wazi na ni wa miaka yote.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema kumekuwa na taarifa nyingi za mtaani juu ya kumpata mgombea Urais wa chama hicho lakini wao kama chama hawafanyi kazi kwa shinikizo kwani kanuni zake ziko wazi za kuanza na wagombea watano baadaye watatu na mwisho mmoja.

Alisema kwa sasa hakuna mgombea wa kuondoka katika chama hicho baada ya jina lake kutoonekana katika wagombea watano baadaye watatu hadi mwisho kupata jina moja kwani wagombea wote 38 walichukua fomu waliapa kutohama ikiwa majina yao hayataonekana kwenye kinyang'anyiro hicho.

"Hatufanyi kazi kwa presha za nje bali tutafuata taratibu zote zinazotakiwa na kwa sasa hivi hata ikiwa mtu jina lake halitaonekana basi muda wa kukata rufaa hakuna, lakini sio kwamba tunawakataza wasikate rufaa lakini wanakata rufaa kwa nani, wakati wote ni wana-CCM na mimi simuoni mtu wa kuondoka CCM kwani hata huko nyuma hata mawaziri walikatwa lakini wote walikuwa pamoja na ninaamini hata mchakato huu kila mtu atatendewa haki na tutabaki wamoja," alisema Nnauye.

Alisema kila mgombea anajua wazi kuwa kuna kushinda na kushindwa na kuna kuteuliwa na kutokuteuliwa na asiyekubali kushindwa si mshindani.

Alisema jana ndio mchakato rasmi wa kumpata mgombea urais wa CCM umeanza ambapo Kikao cha kwanza kitakuwa ni Sekretarieti ya Maadili ya Chama hicho ambacho kitaongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana huku ajenda kuu ikiwa ni maandalizi ya Mkutano Mkuu wa chama hicho pamoja na mambo mengine ya ratiba, malazi ya wajumbe.

"Julai 8, 2015 kutakuwa na Kikao cha Usalama na Maadili ambacho kitaongozwa na Rais Jakaya Kikwete ambapo Julai 9, 2015 kutakuwa na uzinduzi wa ukumbi mpya wa CCM ulioko nje kidogo ya mji wa Dodoma kabla ya Rais Kikwete kwenda kuvunja Bunge na baadaye kitafanyika kikao cha Kamati Kuu ya CCM, "alisema Nnauye.

Nape alisema Julai 10,  Halmashauri Kuu ya Chama hicho itakutana kwa mambo makuu matatu ambayo ni kupitisha jina la mgombea urais Zanzibar lakini pia itapitia ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020 ambayo iliandaliwa na Kamati iliyoongozwa na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira na ambayo itapelekwa kwenye Mkutano Mkuu.

Alisema Halmashauri Kuu itapokea majina matano ya wagombea na kisha kupigiwa kura ili kupata majina matatu. Aliongeza kuwa Julai 11, 2015 Mkutano Mkuu wa CCM utafanyika ili kupitisha ilani ya CCM  lakini pia kupiga kura ili kupata jina moja kutoka majina matatu  ambapo ndio litakuwa jina la mgombea Urais kupitia CCM.

Akizungumzia maandalizi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM ambao wanakadiriwa kufikia zaidi ya wajumbe 3,000, alisema wamejipanga vizuri na wajumbe wote wasiwe na wasiwasi ya maandalizi yakiwemo malazi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa alisema Mkoa huo kwa sasa unatarajiwa kuwa na wageni zaidi ya 3,000 ambao watakuwepo kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano Mkuu wa CCM hivyo kwa sasa wao kama Mkoa wamejipanga vizuri kuhakikisha wageni wote wanafika na kuondoka salama.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Gallawa alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa imejipanga vizuri kuhakikisha ulinzi na usalama utakuwepo wa kutosha hasa katika kipindi hiki ambacho kuna ongezeko la wageni.

"Nawatahadharisha wale wote wanaojipanga kwa namna moja ama nyingine kushiriki vitendo vya uvunjifu wa amani  tutawashughulikia kwa mujibu wa sheria za nchi na yule ambaye asiyekuwa mjumbe wa mikutano na wala sio mwalikwa ni bora asiende kabisa Dodoma, "alisema Gallawa.

Chanzo: Mwananchi

Monday, July 6, 2015

DIAMOND AFANYIWA KUFURU NIGERIA


 
Pasua anga! Staa grade one kwenye Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ amefanyiwa kufuru ya bonge la pati na msanii mwenzake kutoka nchini Nigeria, Kingsley Chinweike Okonkwo ‘KCEE’ Ijumaa Wikienda lina ubuyu kamili.
Staa grade one kwenye Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

Kwa mujibu wa chanzo cha karibu kilichosafiri na staa huyo ambaye yupo nchini humo kwa ziara yake inayofahamika kama ‘Nana Tour’, tangu Diamond alipofika siku ya kwanza akiwa na mameneja wake, Salam, Babu Tale, DJ wake aitwaye Romy Jones na wengine, mastaa kibao wakubwa walikuwa wakihitaji kuwa wenyeji wake.
“Jamaa ana uhusiano mzuri sana na mastaa wa Nigeria. Kuna ambao ameshafanya nao kazi kama Yemi Alade, Tiwa Savage, Bracket, Iyanya, KCEE na P Square (bado haijatoka). “Pia wapo wengine kibao wanaotaka kufanya naye kazi hivyo wanamuwinda.
Waliposikia anakuja kufanya ziara ya wimbo wake mpya kila mmoja alitaka kuwa mwenyeji wake.
“Simu zilikuwa nyingi lakini mwisho wa siku KCEE alikuwa ameshafika uwanja wa ndege kutupokea na hiyo ilikuwa rahisi kwake kwa kuwa naye hivi karibuni alimshirikisha katika wimbo wake wa Love Boat,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo kinaendelea kumwaga ubuyu kuwa baada ya kufika nyumbani kwa KCEE, staa huyo mwenye mikoko na majumba ya kutosha nchini humo kupitia muziki, aliwafanyia bonge la ‘sapraiz’ kwa kufungua makabati yake ya rangi ya dhahabu na kuwaonesha tuzo kibao alizozipata kisha wakajimwaga sebuleni ambapo waliandaliwa pati ya madikodiko ya Kinigeria.

Wakipata msosi.

“KCEE ni kati ya wasanii wenye mafanikio na mali kibao. Jumba tu aliokaribishwa ndani yake lilijengwa kwa kuchanganya nakshinakshi za dhahabu.”
Ijumaa Wikienda lilimtafuta Diamond kupitia Mtandao wa WhatsApp kuhusiana na mapokezi yake ambapo alifunguka:
“Nashukuru kwa Nigeria kunipokea vizuri najihisi kama niko nyumbani, nasema asante sana kwa watu hawa kwani wameonesha sapoti ya nguvu hata katika kunipigia kura katika Tuzo za MTV MAMA,” alisema Diamond na kuongeza.
“Kwa sasa akili yangu yote nimeielekeza kimataifa zaidi baada ya kufanya kolabo za kutosha Afrika.”
Hivi karibuni Meneja wa Diamond, Babu Tale alikaririwa akisema kuwa mashabiki wategemee kolabo ya kimataifa na msanii mkubwa na kudokeza kuwa msanii huyo anaweza kuwa Usher Rymond, Chris Brown, Ne-YO au yeyote mkubwa kutoka Marekani.

Chanzo: Global Publishers

BANZA TUMWACHIE MUNGU!

Ugua pole! Hali ya mwanamuziki wa Dansi Bongo, Ramadhan Masanja ‘Banza Stone’ ni ya kumwachia Mungu kwani bado ni tete na watu wamekuwa wakimiminika kwa ajili ya kumuona katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar alikolazwa.
Mwanamuziki wa Dansi Bongo, Ramadhan Masanja ‘Banza Stone’ akiwa katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar alikolazwa.

Ijumaa Wikienda lilitia maguu kwenye hospitali hiyo na kufanikiwa kumuona Banza ambaye kwa wakati huo alikuwa amezungukwa na watu mbalimbali, wakiwemo wanamuziki wenzake wa dansi wengi wakiwa ni wale wa Bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’.
Kila aliyekuwa akimuona mwanamuziki huyo aliyekuwa akibamba vilivyo kila alipopanda jukwaani, alikuwa akihuzunika huku wasanii wenzake wakiangua vilio kutokana na kutoamini alivyo Banza kwa sasa.
Akipewa kikombe cha uji.

“Yaani inahuzunisha kwani huyu siyo yule Banza tuliyemzoea, hali yake hii ni ya kumwachia Mungu tu kwani ndiye anayejua kila tatizo linalomtokea binadamu litaondokaje, kikubwa ni kuendelea kumuombea tu maana hatua aliyopo siyo nzuri, ni Mungu tu aweke mkono wake,” alisema mmoja wa wanamuziki ambaye hakutaka jina liandikwe gazetini.
Naye kaka wa Banza, Hamis Masanja alisema waliamua kumpeleka hospitali kutokana na hali yake kuwa mbaya ambapo Mkurugenzi wa Twanga Pepeta, Asha Baraka akiwa na viongozi wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) walifika nyumbani kwa ajili ya kumjulia hali ndipo wakaafikiana kumpeleka hospitali.
Kwa muda mrefu Banza amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa fangasi za kichwani hali iliyomsababishia matatizo ya kutosikia na kutoona vizuri huku akishindwa kabisa kunyanyuka kitandani.
Banza akiwa na afya yake jukwaani.

KUTOKA KWA MHARIRI
Ijumaa Wikienda linaungana na Watanzania kumuombea Banza Mungu amponye kwa neno lake kutoka kwenye Kitabu cha Yeremia 30:17 linalosema: “Kwa maana nitakurudishia afya nami nitakuponya jeraha zako, asema Bwana kwa sababu wamekuita mwenye kutupwa wakisema ni Sayuni, ambao hapana mtu autakaye.”

Chanzo: Global publishers

Mkojo wa paka sasa wageuka ‘dili

 
 
Paka ni mnyama rafiki anayependwa na binadamu. Ni mnyama pekee  anayeweza kuishi na binadamu ndani ya nyumba moja tofauti na wanyama wengine.
Katika maisha ya kawaida ya mwanadamu hasa jamii Afrika, paka hutumika pia kama mlinzi kuzuia au kudhibiti panya ndani ya nyumba kwa kuwakamata na kuwa mlo wake.
Lakini Waswahili husema; “tembea uone mambo.”
Usemi huo umetimia kwangu baada ya kufika mkoani Morogoro, hivi karibuni na kutembelea Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
Katika chuo hicho, wasomi wazalendo ambao ni watafiti wa masuala ya kilimo na ekolojia ya panya, wamebaini kwamba mkojo wa paka unaweza kutumika kama njia ya  kufukuza panya kwenye mashamba na makazi ya watu.
Tofauti na wengi walivyozoea kwamba paka hutumika  kufukuza panya nyumbani, lakini sasa kwa ugunduzi wa wataalamu hao  mkojo wa mnyama huyo rafiki wa binadamu
pia unaweza kufanya kazi hiyo. Mkuu wa mradi huo katika Kitengo cha Kudhibiti Viumbe Waharibifu Shambani kutoka SUA, Profesa Loth Mulungu anasema kwamba walianza mradi huo mwaka 2012, lengo likiwa kudhibiti panya.
“Tulitafiti ili kuwezesha mkojo wa paka kutumika kama kiuatilifu cha kufukuza panya nyumbani na kwenye mashamba,” anasema Profesa Malungu.
Anasema kuwa mradi huo unadhaminiwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), na ulianzishwa kama moja ya njia mbadala za kukabiliana na panya waharibifu.
“Panya ni kiumbe mharibifu shambani, hata nyumbani. Ili kumwangamiza, zimekuwapo njia mbalimbali za kuwadhibiti ikiwamo utumiaji wa sumu ambayo si rafiki wa mazingira pamoja na afya za binadamu.
Pia inatokea, nao panya wakigundua mwezao mmoja amekufa kwa kula chakula chenye sumu, wanaobaki hawali tena chakula hicho,”anasema na kuongeza:
“Lakini kwa huu mkojo wa paka, wakinusa harufu watakimbia wakidhani paka yupo kwenye eneo husika.”
Mkojo unavyodhibiti panya
Akizungumzia mkojo huo unavyodhibiti panya, Profesa Mulungu anasema utafiti umeonyesha kuwa mkojo wa paka jike una harufu kali ikilinganishwa na ile ya paka dume na ndiyo panya akiinusa anakimbia na harudi eneo husika.
Profesa Mulungu anaeleza kuwa: “Utafiti bado unaendelea ili kupata viini vilivyoko kwenye mkojo huo kabla ya kutengenezwa kwenye maabara. Utafiti wetu umebaini kuwa mkojo huo unafanya kazi kwa asilimia 100.”
Anabainisha kuwa ingawa kazi ya utafiti huo haijakamilika, umefanikisha kubaini aina mbili za viini kwenye mkojo wa paka, ambavyo humfanya panya agundue kuwa harufu husika ni ya paka.
“Utafiti ukikamilika na kiwatilifu kikatengenezwa, tutakuwa na jibu zuri zaidi na kufanikisha tafiti yetu. Kiwatilifu hi
Licha ya mradi huo, SUA pia inafanya mradi mwingine wa utafiti wa panya kwa kutumia njia za ekolojia, ambapo makamu mkuu wa chuo kikuu hicho Profesa Gerald Monela anasema:
“SUA inaahidi kutumia uwezo, ubunifu na utalaamu wa watafiti wake katika kusaidia kudhibiti tatizo la panya waharibifu wa mazao ambao wamekuwa wakisababisha hasara kubwa kwa wakulima nchini kila mwaka.”
Anasisitiza: “ Tanzania pekee hupoteza zaidi ya tani 400,000 za mahindi kila mwaka kutokana na uharibifu unasababishwa na panya.”
Anabainisha kuwa chakula hicho kinachopotea kingeweza kutosha kulisha zaidi ya Watanzania milioni mbili kwa mwaka mzima, hivyo ni kiasi kikubwa cha upotevu.
Anaongeza kuwa mbali tatizo la upotevu wa chakula, pia panya husababisha magonjwa mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa tauni.
Profesa Monela anasema kuwa SUA ina wataalamu wenye weledi wa kudhibiti tatizo hilo na tayari mafanikio makubwa yameonekana nchi nzima kutokana na usaidizi wa chuo kikuu hicho.
Mradi huo unazijumuisha taasisi mbalimbali za hapa nchini kama zikiwamo Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Chuo Kikuu cha Da es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Chang’ombe (DUCE), Chuo Kikuu cha Muhimbili(MUCHS katika taasisi ya tiba asilia na Chuo Kikuu cha Dodoma.
Mwaka 2012 katika maonyesho ya Taasisi za Elimu ya Juu yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, mtafiti wa kituo cha utunzaji wadudu kilichoko chini ya SUA, Profesa Christophar Sabuni alisema kuwa kituo hicho kinafanya utafiti utakaosaidia wananchi kupata njia mbadala na salama kwa binadamu ya kufukuza panya sehemu mbalimbali, badala ya kutumia sumu kama inavyofanyika sasa.
“…Hasa tukilenga kwenye mazao na makazi ya watu, utafiti huu unalenga kumsaidia mwananchi kufukuza panya na kuondoa uharibifu. Wanaopata adha kubwa ya wanyama hawa ni wananchi, hivyo utafiti huu utawasaidia sana,” alisema Profesa Sabuni.
Alifafanua kwamba mchakato wa utafiti huo ulianza kwa kuangalia ni haja ndogo ya paka wa jinsia ipi unaoweza kupata dawa ya kufukuza panya na kugundua kuwa paka wa jike ni bora zaidi.
“Unapofanya utafiti, huna budi kuangalia njia itakayosaidia kutimiza lengo haraka, tukaamua kuangalia jinsia dume na jike na kugundua kuwa harufu ya mkojo wa paka jike itatufaa zaidi,” alisema.
Alisema kupitia utafiti wao, wanalenga kuichakata haja ndogo hiyo kutoka kimiminika hadi kuwa katika hali ya ungaunga ili kurahisisha utumiaji wake kama dawa.

Alibainisha kuwa utafiti unatarajiwa kuchukua wastani wa miaka mitano ikiwa ni mwendelezo wa tafiti mbalimbali zilizowahi kufanywa na kituo hicho.
Profesa Sabuni alieleza kwamba, awali utafiti huo ulihusisha utafiti wa mafunzo ya panya kwa ajili ya kugundua mabomu yaliyotegwa ardhini na kugundua vimelea vya kifua kikuu katika makohozi.
Naibu makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa Yunika Ngaga alikaririwa hivi karibuni akieleza kuwa SUA kwa sasa kinaendelea kufanya zaidi ya tafiti 200 za kilimo ili kukiwesha kilimo kuwa endelevu nchini.
Profesa Yunika alikuwa akizungumza wakati wa warsha kwa waandishi wa habari juu ya kilimo na lishe iliyofadhiliwa na Innovative Agriculture Research iAGRI SUA.
Alisema kwamba SUA ina nafasi kubwa ya kufanya mikakati inayopangwa na Serikali ukiwamo kuwezesha mpango wa Kilimo Kwanza kutekelezeka akieleza kwamba kuwapo kwa mpango wa kilimo endelevu kwa kutumia tafiti kutaleta manufaa kwa wakulima na taifa.
Alisema kuwa bado kuna upungufu unayotokana na kilimo kutokuwa katika mpangilio endelevu kufuatia tafiti hizo kutotumika.
Utafiti mwingine wa SUA
Mwaka 2012 kitengo cha Apopo katika chuo kikuu hicho kilibaini kuwa panya ni wanyama wenye uwezo mkubwa wa kunusa na kufanya kazi adimu kama za kutegua mabomu yaliyotegwa ardhini kwa umbali wa mrefu wa kipimo cha mita.
Utafiti huo ulianza kufanywa na raia wa Ubelgiji, Bart Weetgen, mwaka 1998 katika chuo Kikuu cha Antwerp nchini Ubelgiji.
Kwa mujibu wa kituo cha Apopo, Weetgen alianza kwa kuuchambua upekee wa panya, kabla ya kuanza kuwatumia kunusa mabomu.
“Weetgen aliona kuwa, panya wa porini aina ya rodent wanaopatikana zaidi Tanzania, wanaweza kubaini kirahisi mabomu yaliyofukiwa ardhini,”alieleza Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Apopo, Majenda Mhutila.
Kiongozi Mkuu wa Mafunzo kwa panya, SUA, Abdullah Mchomvu alieleza kuwa panya walionekana kufaa zaidi kufanya kazi hiyo kwa sababu ya maumbile yao.
cho kitatumika na watu katika kudhibiti panya,” alisisitiza .

Alisema kuwa umbile la panya pamoja na uzito wake humfanya asiweze kulipua mabomu ardhini mara anapoyabaini.
Lakini, pia panya walionekana kuwa na tabia ya kipekee ya kuhifadhi na kufukua.
“Kwa uasilia panya hukusanya mazao wakati wa mavuno, kisha kuyaficha katika mashimo shambani. Baadaye hutumia njia ya kunusa kuyapata mazao waliyoyaficha nyakati za ukame. Kwa maana hiyo, tulitumia sifa yake hiyo na kumtumia kubaini kwa kutumia harufu,” alisema Mchomvu.
Aliongeza kuwa panya walibainika kuwa na uwezo mkubwa wa kutumia pua zao kuliko kuona, kwani macho yao hayana nguvu nyakati za mchana.
“Ni nafuu zaidi kumtunza panya kuliko mbwa. Kwa mfano panya 200 huweza kukaa katika jengo moja. Panya wana uwezo wa kufuata zaidi vitendo, kuliko kutazama kinachofanywa na mwongozaji,”alisema akiongeza:
“Sifa hizi, ndizo zilizotumiwa na watafiti kumhakiki panya kuwa mteguaji bingwa wa mabomu kuliko binadamu au vifaa vya kiteknolojia.”
Wanavyoweza kutegua mabomu
Mchomvu aliweka wazi kuwa, ili panya aweze kuifanya kazi ya kutegua mabomu ni lazima apate mafunzo, ambayo humpitisha katika hatua tisa muhimu.
Aliitaja hatua ya kwanza kuwa ni kumfanya awe rafiki au kumjengea tabia za kumzoea mwanadamu.
Alibainisha kuwa mkufunzi wake hutakiwa kumfanya panya amzoee, kwa sauti na kwa harufu ili asimdhuru.

Chanzo: Mwananchi