LATEST POSTS

Thursday, August 6, 2015

Tuwakatae wanasiasa wenye roho ‘mtakavitu’

TANZANIA inaelekea pabaya na huenda ikawa mfano mbaya usiostahili kuigwa popote duniani katika suala la ushindani wa kisiasa. Maana halisi ya siasa imekosa utambuzi na badala yake imegeuzwa kuwa nyenzo ya chuki, fitina, uadui na kwa upande mwingine kitega uchumi (biashara) cha watu binafsi.
Maandalizi ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, yamedhihirisha wazi kuwa dhana ya demokrasia inaendelea kudhoofika badala ya kustawi katika vyama vya siasa nchini.
Wanasiasa waliojawa roho ‘mtakavitu’ wanapambana kwa ari ya kufa au kupona kupata uongozi ili kutumia nafasi hiyo kujineemesha na familia zao. Inashangaza kuona kuna wanasiasa nchini wanaoamini kimakosa kwamba bila kuwa rais, mbunge au diwani hakuna maisha tena Tanzania. Huo ni uroho wa madaraka.
Baadhi ya wanaowania uongozi wa kisiasa wamefikia hatua ya kushambuliana kwa matusi, ngumi na bakora hadharani wakati wa kujinadi kwa wapiga kura ndani ya vyama vya siasa. Wamesahau kwamba, siasa ni mchezo wa kushindana kwa sera na nguvu ya hoja.
Vitimbi vya kila aina vimeshika hatamu katika mchakato wa uchaguzi mkuu ujao tofauti na uliopita. Unafiki, chuki, fitina, rushwa, kashfa, kuchafuana na kudhalilishana vimetawala kampeni za uchaguzi ndani ya vyama.
Cha kushangaza ni kwamba, baadhi ya wanasiasa wameonyesha unafiki mkubwa kiasi cha kuongopa mchana kweupe kwa lengo la kupata umaarufu na kuwadhoofisha kisiasa wapinzani wao mbele ya jamii. Ni katika kipindi hiki cha hekaheka za uchaguzi si jambo la ajabu kusikia mwanasiasa anajitoa fahamu na kuita rangi nyeusi kuwa ni nyeupe na nyeupe kuwa nyeusi.
Ukweli usiopingika ni kwamba, wanasiasa wanaocheza rafu hizi dhamira yao si ya kutafuta uongozi wa kuwatumikia wananchi. Kinachowasukuma zaidi ni hisia za kupata uongozi kwa ajili ya kuutumia kwa maslahi yao binafsi na familia zao.
Ndiyo maana kwa mfano, wanasiasa wengi katika mikoa ya pembezoni wanapochaguliwa kuwa wabunge huhama majimbo yao na kwenda kuishi pamoja na familia zao Dar es Salaam na Dodoma. Kwa mawazo yao potofu wanaamini hadhi ya mbunge haistahili kuishi jimboni na kujichanganya na wananchi wa kawaida, hususan wasiojiweza kiuchumi.
Lakini jambo la kujivunia ni kwamba Watanzania wa leo wamefikia hatua ya kutodanganyika tena. Ni watu wanaojitambua na wenye ufahamu mzuri juu ya kiongozi bora na bora kiongozi. Kwa hiyo, kipindi hiki hawako tayari kufanya kosa la kukubali kushawishiwa na chochote ili kuchagua kiongozi kinyume cha matakwa yao.
Yeyote anayeamini kimakosa kwamba ili achaguliwe kuwa rais, mbunge au diwani lazima apambane na wapinzani wake wa kisiasa kwa kuwajengea chuki, uadui, kuwatusi, kuwazushia kashfa na hata kupigana nao, atarajie suluba kali ya kisiasa kupitia sanduku la kura katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
Watanzania wanapenda kuona nchi inayosifika kwa tunu ya amani duniani inakuwa na wanasiasa wanaotambua kwamba, siasa ni ushindani wa sera na nguvu ya hoja. Pia wanataka kuongozwa na wanasiasa waadilifu, waaminifu, wenye hekima na uwezo wa kuongoza wasaidizi wao kutafuta ufumbuzi thabiti wa matatizo yanayowanyima maendeleo ya kweli kuanzia ngazi ya familia.
Umakini wa wananchi, hususan wapiga kura katika uchaguzi wa viongozi wa kisiasa ni nyenzo muhimu itakayosaidia kuleta mabadiliko chanya ya kijamii na kiuchumi katika taifa letu. Hata hivyo, hilo haliwezi kufikiwa ikiwa tutaendelea kuwakumbatia ‘wanasiasa maslahi’ wanaotafuta uongozi kwa kutumia mbinu haramu ili baadaye waugeuze kuwa kitega uchumi chao. Tuamke.

Chanzo: Raia Tanzania 

Diamond na Zari wajaliwa mtoto wa kike. Diamond amemuanzishia mtoto wake ukurasa wa Instagram kwa jina Tiffah Dangote


Msanii wa Bongo mwenye umaarufu wa kimataifa, Diamond Platnumz, maarufu, Naseeb Abdul, amepata majukumu mapya baada ya kujaliwa mtoto.
Mkewe msanii huyo, Zarina Hassan, Zari the boss lady, alijifungua msichana mapema leo na kuipa furaha familia hiyo.
Baada ya kuokota tuzo tofauti kwenye mziki, Diamond hatimaye amepata tuzo kutoka kwa Mungu kwa kufanya juhudi nyingi za kutaka kuwa mzazi.
Diamond alipachika picha ya mtoto wake akibebwa na mamake, Sanura Kassim kwenye ukurasa wake wa Instagram na kupokea pongezi kutoka mashabiki.
Aidha, msanii huyo amemuanzishia mtoto wake ukurasa wa Instagram kwa jina Tiffah Dangote na kuvutia zaidi ya wafuasi elfu kumi na sita.
Diamond mwenye umri wa miaka 25, aliwashangaza wengi kwa kuanza kumfanyia bintiye ununuzi wa vifaa vya watoto kabla ya kuzaliwa.
Chanzo: BBC Swahili

Zari ajifungua mtoto wa kike " Princess Tiffa"

Zari
Staa wa Bongo Fleva ambaye jina lake limebeba uzito mkubwa Afrika, Diamond Platnumz anayo furaha kushare na sisi hii good news… Post yake Instagram inasomeka hivi >>> ‘My mom’s face it’s enough to Express how i feell… Welcome to the world @princess_tiffah Sura ya mama yangu inatosha kueleza ni kiasi gani najiskia ndani ya Moyo wangu… karibu kwenye ulimwengu@princess_tiffah‘ >>>> @

Chenge kuhojiwa na Baraza la Maadili leo

Mbunge wa Jimbo la Bariadi Magharibi, Andrew 
 Mbunge wa Jimbo la Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.

Mbunge wa Jimbo la Bariadi Magharibi, Andrew Chenge leo atapandishwa kizimbani kuhojiwa na Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kuhusika katika kashfa ya ‘kuchota’ fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.
Chenge ni mmoja wa viongozi waliopata mgawo wa fedha kutoka kwenye akaunti hiyo jambo ambalo ni ukiukaji wa sheria namba 13 ya maadili ya viongozi wa umma.
Watuhumiwa wengine ni aliyekuwa waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, mkurugenzi wa sheria, Wizara ya Ardhi, Rugonzibwa Mujunangoma na Mnikulu wa Ikulu, Shaaban Gurumo. Chenge alifungua kesi Mahakama Kuu akipinga kuhojiwa dhidi ya tuhuma za kukiuka maadili ya viongozi baada ya kupokea Sh1.6 bilioni kutoka kwa mkurugenzi wa VIP Engineering, James Rugemalira, fedha ambazo zinahusishwa na akaunti hiyo.
Katika vikao vilivyopita, Chenge alilitaka baraza kutojadili shauri lake kwa sababu kesi yake ya msingi kuhusu fedha za escrow ilikuwa imefunguliwa Mahakama Kuu.
Alisisitiza kuwa kuendelea kufanya hivyo ni kuingilia uhuru wa mahakama.
Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma lilisitisha kumhoji mtuhumiwa huyo ili kusubiri uamuzi wa Mahakama Kuu.
Hata hivyo, Mahakama Kuu ilitupilia mbali shauri lake la kuzuia kujadiliwa na kutoa nafasi kwa Baraza la Maadili kuendelea na kazi yake kuchunguza uvunjifu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Taarifa ya baraza iliyotolewa kabla ya kuanza kusikiliza mashauri hayo, ilibainisha kuwa vikao vyake vinafanyika baada ya Mahakama kutupilia mbali shauri la kikatiba lililofunguliwa kuzuia taasisi za Serikali pamoja na baraza hilo kuendelea kufanya uchunguzi wa aina yoyote unaohusiana na sakata la escrow.
Baadhi ya viongozi wa umma wanatuhumiwa kuhusika katika sakata hilo kwa sababu walipokea fedha katika akaunti zao kupitia Benki ya Mkombozi.
Kashfa ya escrow ilisababisha aliyekuwa waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na waziri wa Ardhi, Profesa Tibaijuka kuondolewa katika nyadhifa zao.

Lipumba njia panda CUF

Mwenyekiti wa chama  cha CUF , Profesa Ibrahim Mwenyekiti wa chama  cha CUF , Profesa Ibrahim Lipumba.

Sintofahamu imeendelea kukigubika Chama cha Wananchi (CUF), baada ya kauli ya mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba kuwaacha wafuasi wa chama hicho katika giza nene juu ya hatima yake kisiasa.
Hali hiyo ilitokea jana baada ya mkutano wa Profesa Lipumba aliouitisha na wanahabari kuahirishwa bila kuelezwa utafanyika lini badala yake akawaambia wafuasi wa chama hicho waliokusanyika makao makuu wa chama hicho, Buguruni kuwa “kila mwanachama ana wajibu wa kujenga chama bila kujali wadhifa wake.”
Makumi ya wafuasi hao walitaka kusikia Profesa Lipumba akieleza mustakabali wake baada ya kuripotiwa katika baadhi ya vyombo vya habari kuwa amejiuzulu.
Hata hivyo, wazee wa CUF waliwahi kufika katika ofisi ya mwenyekiti huyo na kumtaka awaeleze alichotaka kuzungumza na wanahabari kwanza, kitendo kilichosababisha kuchelewa kwa mkutano huo na kuvutia idadi kubwa ya wafuasi waliokuwa wakiimba... “Kimyakimya, nguvu ya Lipumba mnaijua.” Wimbo mwingine ulikuwa... “Si si si mnaona!! Nguvu ya Lipumba kuituliza hamuwezi.”
Baada ya kuahirishwa kwa mkutano huo na wafuasi kuendelea kuimba, Profesa Lipumba alitoka ofisini kwake saa 6.25 mchana na baada ya Msemaji wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Rajab Katimba kuwatuliza wafuasi hao, Profesa Lipumba alizungumza nao akiwataka waisome na kuielewa katiba ya CUF ambayo imewapa wajibu wa kukijenga chama chao.
Alisema mchakato wa kukijenga chama hautegemei wadhifa alionao kada husika, bali uanachama wake pekee unatosha kuleta maendeleo.
“Mwaka 1995 nilikuwa mwanachama wa kawaida nilipogombea urais kwa tiketi ya CUF na mwaka 1999 nilikuwa mwanachama wa kawaida nilipoongoza kampeni za Jimbo la Temeke na Ubungo ambapo tulishinda lakini wakatuibia kura,” alisema.
Huku akionekana mtulivu tofauti na nyakati nyingine anapozungumza na wafuasi wake, Profesa Lipumba alisema: “Chama ni taasisi na tukijenge kama taasisi, ni wajibu wa kila mwanachama bila kujali nafasi aliyonayo kukijenga,” alisema na kuhitimisha kwa salamu ya; “hakiii” na kujibiwa “kwa wote,” bila kuimalizia.
Baadhi ya wafuasi walionekana kutoridhishwa na kauli yake na kwamba ametumia mafumbo wakati walitaka kusikia habari ya kujiuzulu kwake... “Kiu yangu ilikuwa kumsikiliza baada ya kusikia fununu zilizoandikwa na gazeti jana (juzi) badala yake katuambia tujitahidi kuendeleza chama,” alisema Said Suleiman (58).
Hali ilivyokuwa
Mapema saa nne asubuhi, wafuasi hao walianza kuingia taratibu katika eneo la ofisi hizo na kujaa huku baadhi ya wazee wakiwa wameshaingia ofisini kwa Profesa Lipumba.
Saa 6.05 mchana, Naibu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya akiongozana na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, Abdul Kambaya waliingia ndani ya chumba cha mkutano huku wafuasi wakiwa wamejipanga mstari wakiimba nyimbo za kumsifu Profesa Lipumba na kusema mkutano umeahirishwa hadi utakapotangazwa tena baada ya wazee, wanachama na viongozi mbalimbali kuingia ofisini wakitaka kuelezwa fununu za kujiuzulu.
Kuhusu taarifa za Profesa Lipumba kujiuzulu, Kambaya alidai kwamba wanaosema hivyo wanapiga ramli na kwamba yanayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ni uzushi na hakuna matatizo yoyote baina ya CUF na Ukawa na kama yangekuwapo, juzi Katibu Mkuu wake ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad asingehudhuria Mkutano Mkuu wa Chadema.
Katika mkutano huo, Maalim Seif alisema hakukuwa na ukweli wowote juu ya kujiuzulu kwa Profesa Lipumba na wanaosema habari hizo wanataka kuwachafua na kuwavuruga Ukawa.
“Kiongozi yeyote anayetaka kujiuzulu lazima barua yake atume kwa katibu mkuu wa chama. Mimi sijapata barua yake na hadi jana saa nne usiku nilikuwa naye wala hakuonyesha dalili za kujiuzulu,” alisema.
Lakini wafuasi waliokuwa wamepiga kambi CUF jana waligawanyika kimawazo juu ya ukweli wa taarifa hizo.
“Hofu ya Profesa Lipumba kujiuzulu ipo, tena kubwa tu ndiyo maana tumekuja kusikiliza lakini kwa sababu amekaa na wazee hakuna kitakachoharibika. Ninaridhika CUF kuendelea kuwa ndani ya Ukawa ili upinzani tushike dola,” alisema Mohamed Njuma kutoka Vingunguti.
Ismail Hamis alisema inaonekana kuna mgogoro hivyo wanataka kujua kilichomkumba kiongozi wao.

Dk Slaa: Niko salama, nitazungumza muda ukifika

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa (wa 
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa (wa tatu kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Mbunge wa Moshi Mjini (Chadema), Philemon Ndesamburo (wa pili kulia) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Japhary Michael (kushoto) na viongozi wengine wa chama hicho walipomtembelea Slaa nyumani kwake Dar es Salaam jana.

Siku tatu baada ya Baraza Kuu la Chadema kuridhia kumpumzisha kwa muda Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa baada ya kutofautiana na Kamati Kuu kwa kumkaribisha waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kiongozi huyo amesema yupo salama na wakati mwafaka ukifika atazungumza ya moyoni.
Akizungumza kwa mara ya kwanza na gazeti hili tangu Chadema imkaribishe Lowassa na hatimaye kumpitisha kuwania urais kupitia muungano wa Ukawa, Dk Slaa alisema amekuwa akisikia mengi yakisemwa juu yake lakini yote yamekuwa yakimchekesha tu.
Hakuhudhuria vikao muhimu vya chama hicho na vile vya Ukawa, vikiwamo; wakati Lowassa akitambulishwa rasmi, akichukua fomu, kikao cha Baraza Kuu na juzi Mkutano Mkuu na hakuwa akipatikana kwa simu yake ya mkononi.
Wakati kimya kikitawala juu ya hatima yake, baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikiandika kuwa amejivua uanachama Chadema.
Lakini jana alisema: “Naangalia mambo mengi yanayoendelea kwenye mitandao halafu ninacheka tu, usifikiri sifuatilii, nafuatilia kinachoendelea na ninabaki nikicheka.”
Kuhusu hatima yake kisiasa na madai ya kujiuzulu uanachama ndani ya Chadema, alisema hawezi kuzungumza lolote kwa sasa na atafanya hivyo wakati mwafaka ukifika. “Usijali wakati wangu wa kuzungumza ukifika nitasema tu, sasa hivi nawaachia mzungumze, lakini nitazungumza,” alisema.
Kadhalika, alipoulizwa kuhusu taarifa zilizozagaa kuwa maisha yake yapo hatarini kwa kuwa anatishwa, Dk Slaa alisema hata hilo pia atalizungumzia wakati mwafaka ukifika.
“Ndiyo hayohayo ninayosema, wala msijali nitazungumza wakati ukifika,” alisema na kusisitiza: “Nipo salama.”
Dk Slaa alisema kwa sasa yupo mapumzikoni nje ya jiji la Dar es Salaam ingawa hakutaka kueleza ni eneo gani.
Juzi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alifafanua tofauti iliyojitokeza kati ya Kamati Kuu ya Chadema na Dk Slaa wakati wa mchakato wa kumpokea Lowassa.
Katika mkutano huo wa Baraza Kuu la Chadema, Mbowe alisema wamekubaliana katibu mkuu huyo apumzike kwa muda... “Nina hakika kwa tabia na hulka za Dk Slaa… kwa sababu anajua tunampenda na yeye anakipenda chama hiki, tunamwombea kwa Mungu ampe nguvu na ujasiri wa kuona kwamba kauli ya wengi ni kauli ya Mungu.”
Ndesamburo na siri nzito
Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo na makada wengine wa Chadema, jana walikwenda kuonana na Dk Slaa nyumbani kwake na kufanya naye kikao cha faragha.
Picha zilizomuonyesha Ndesamburo akiwa na Dk Slaa na makada wengine akiwamo Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Jaffar Michael, zilisambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii jana na kuibua mijadala.
Baadhi ya waliochangia mijadala hiyo walidokeza kuwa huenda Ndesamburo anayeheshimika ndani ya chama hicho alikwenda kujaribu kusawazisha hali ya mambo.
Mkuu wa Idara ya Habari wa Chadema, Tumaini Makene alikiri kuwa picha hizo ni halisi, baadhi zilipigwa juzi na nyingine jana mchana, lakini hakutaka kuingia undani wa mkutano wa wanasiasa hao.
Ndesamburo alithibitisha kukutana na Dk Slaa: “Ni kweli tulikwenda, kwani kuna tatizo gani? Si mzee mwenzangu? Halafu bado ni mwanachama wetu, hajatoka Chadema, hivyo tuna kila haki ya kwenda kumsalimia.”
Alipoulizwa kama alikwenda kumsihi Dk Slaa arejee kuendesha mapambano ya kuing’oa CCM, Ndesamburo alisisitiza kuwa walikwenda kumsalimia.
Michael alipoulizwa nia ya safari hiyo alijibu kwa kuuliza; “Dk Slaa ni katibu mkuu wetu kwani tunazuiwa kwenda kumsalimia?”
Dk Slaa aligombea urais mwaka 2010 na kushika nafasi ya pili baada ya Rais Jakaya Kikwete na ndiye aliyekuwa akitajwa kuwania tena nafasi hiyo kupitia Chadema na Ukawa kabla ya “kubadili gia angani” na kumteua Lowassa.

Prof. Lipumba ajiuzulu uenyekiti CUF

 

Profesa Ibrahim Lipumba 
Profesa Ibrahim Lipumba

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Prof. Ibrahim Lipumba leo ametangaza kujiuzulu uenyekiti ndani ya chama hicho.
Tamko hilo la Prof. Lipumba linahitimisha siku mbili za minong’ono na tetesi zilizogubika medani ya kisiasa nchini kuwa kiongozi huyo anaondoka katika chama hicho hali iliyolazimu wananchama, wapenzi na mashabiki wa kiongozi huyo kufurika makao makuu ya chama hicho Buguruni Dar es Salaam jana ili kujua hatma ya kiongozi wao huyo.
Akizungumzia sababu za kujiuzulu kwake, Profesa Lipumba amesema amekerwa na hatua ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao CUF ni chama shiriki kushindwa kusimamia makubaliano yaliyopelekea kuundwa kwa umoja huo.
Amesema Ukawa ulianzishwa kulinda maslahi ya wananchi yaliyoainishwa kwenye Katiba iliyowasilishwa kwenye Bunge Maalumu la Katiba, na kwamba nafsi yake inamsuta hivi sasa kuendelea na uongozi huku waliokuwa wanaipinga Rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba wakikaribishwa kuwania uongozi wa nchi kupitia umoja huo.
Prof. Lipumba amesema baada ya kujiuzulu atajikita kufanya shughuli za kitaaluma kwa kujihusisha zaidi na ushauri wa masuala ya uchumi na maendeleo.

Wednesday, August 5, 2015

Wasifu wa Edward Lowassa

Umoja usio rasmi wa vyama vinne vya upinzani nchini Tanzania unajulikana kwa jina la Katiba ya Wananchi (UKAWA), baada ya kusubiri kwa muda hatimaye umemtangaza Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kuwa mgombea wake wa urais.
Lowassa anagombea kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), huku vyama vingine vitatu vikimuunga mkono. Hii inatokana na sheria za Tanzania ambayo haitambui umoja wa vyama.
Kabla ya kujiengua chama Tawala chama cha Mapinduzi CCM, Edward Lowassa amekuwa mwanachama wa CCM kwa muda wa miaka 38, ambapo alijiunga na chama hicho mara tu baada ya kumaliza elimu yake ya chuo kikuu mwaka 1977.
Hatua ya mwanasiasa huyo mashuhuri nchini Tanzania kuamua kujiunga na chama cha upinzani Chadema, ikiwa imebaki miezi mitatu tu kuelekea uchaguzi mkuu, kumebadilisha kabisa upepo wa kisiasa nchini Tanzania, na hasa uchaguzi mkuu ujao.
 
Lowassa alikuwa Maziri Mkuu kati ya mwaka 2005 na 2008 kabla ya kujiuzuLu wadhifa huo kufuatia sakata la kashfa ya rushwa iliyohusisha kampuni ya kuzalisha umeme ya ki-Marekani Richmond Development Company LLC ya Houston Texas.
Hata hivyo wakati anatangaza kuhamia kwake Chadema, Lowassa alikanusha katu katu kuhusika kwa namna yoyote na kashfa hiyo na kudai kuwa yeye alifuata tu amri kutoka kwa ‘wakubwa’ walio juu yake.
“Kama kuna mtu yeyote mwenye ushahidi basi na aende mahakamani ama sivyo anyamaze” alisema Lowassa
“Kama kuna mtu yeyote mwenye ushahidi basi na aende mahakamani ama sivyo anyamaze” alisema Lowassa
Kuhama kwake kunamfanya Lowassa kuwa ndie kiongozi wa kwanza wa ngazi ya juu kabisa wa CCM kukihama chama hicho tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania mnamo mwaka 1992.
Mwanajeshi wa zamani na aliyewahi kupigana wa vita kati ya Uganda na Tanzania mwaka 1978/79, Lowassa aliiambia hadhara kwamba akiwa kama mtu mwenye uchungu na nchi yake isingekuwa rahisi kubaki ndani ya CCM huku akiona chama hicho kimepoteza mwelekeo na sifa ya kuongoza nchi.
Lowassa amekimbilia upinzani baada jina lake kukatwa wakati alipoomba kuwa mgombea urais kupitia chama tawala CCM katika uchaguzi mkuu ujao utakafanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Wakati mchakato wa CCM wa kumtafuta mgombea wao wa urais ulipoanza, Lowassa ndiye aliyekuwa kinara wa wagombea wote 42. Kila kona aliyozunguka, mikutano yake ya hadhara ilivutia maelfu ya watu waliomuunga mkono.
Wakati chama cha CCM kilimtaka kila mgombea apate sahihi za wadhamini 450 lakini Lowassa alipata sahihi za wadhamini zaidi ya 700,000.
Wasifu wa Edward Lowassa
Hata hivyo mchujo wa chama ulipofanyika jina lake lilikatwa mapema kabla hata ya kupelekwa kwenye vikao vya vya juu vya chama hicho. Ambapo baadae Waziri wa Ujenzi John Pombe Magufuli ndiye aliyeibuka kidedea na kuwa mgombea kupitia chama tawala CCM.
Lowassa ameushutumu mchakato CCM wa kutafuta mgombea urais akiuita kuwa ulijaa chuki na mizengwe dhidi yake, hali ambayo aliifananisha na ‘ubakaji wa demokrasia’
“Nitakuwa mnafki nikisema bado nina imani na CCM. CCM niliyoiona Dodoma si CCM niliyokulia”, alisema, na kuongeza “kama Watanzania hawapati maendeleo kupitia CCM basi wakayatafute nje ya CCM”
Wakati sakala la Richmond lilipoibuka miaka michache tu iliyopita, Chadema ilimfanya limsakama Lowassa kuwa ni mmoja wa mafisadi wakubwa nchini. Lakini wakati chama hicho kinamkaribisha kuwa mwanachama wao, kiligeuka na kusema hakuna mtu msafi nchini na kwamba hawawezi kuacha kumpokea mwanasiasa mwenye mtaji mkubwa wa wafuasi kama Lowassa.
Wakati akiwa Waziri Mkuu, Lowassa alisifika kama mchapakazi hodari na msimamiaji wa moja kwa moja wa shughuli za serikali. Bado anaendelea kufahamika kwa jina la utani la ‘mzee wa maamuzi magumu’.
Je unamfahamu Edward Lowassa ni nani katika siasa za Tanzania ?
Moja ya mafanikio makubwa ya uwaziri mkuu wake ni jitihada kubwa na mafanikio ya upatikanaji wa fedha za kujenga chuo kikuu cha Dodoma. Chuo hiki kikuu cha umma kilichopo katikati ya Tanzania kilianzishwa mwaka 2007.
Lowassa ni mashuhuri pia kwa kusimamia mpango wa serikali uliofanikiwa wa ujenzi wa shule za kata ambazo uliiletea Tanzania sifa kubwa kwa kutoa fursa ya watoto wengi kupata nafasi shuleni.
Mtoto wa Mzee Ngoyai Lowassa, ambaye aliwahi kuwa mtumishi wa serikali ya kikoloni, Lowassa ameanza harakati zake za kuwania urais tangu mwaka 1995 lakini inaarifiwa kwamba rais wa kwanza wa Tanzania Mwl Julius Nyerere alimkatalia kushika nafasi hiyo. Wafuasi wa Lowassa wamekuwa wakiyatupilia mbali madai hayo
Ulipofika uchaguzi wa mwaka 2005, Lowassa hakutaka kuwania urais, lakini badala yake alimnadi rafiki yake wa siku nyingi Rais wa sasa Jakaya Kikwete ambaye alipata ushindi wa kishindo wa zaidi ya asilimia 80.
SOURCE: BBC SWAHILI

MH370:Uchunguzi wa kina waanza Ufaransa

 

Watalamu kutoka Ufaransa, Malaysia na Australia wameanza kuchunguza mabaki ya bawa la ndege iliyopatikana juma lililopita likiwa limesombwa hadi ufukweni na maji ya bahari Hindi katika kisiwa cha Re-Union karibu na Madagascar.
Nia hasa ni kubaini iwapo mabawa hayo ni sehemu ya mabaki ya ile ndege ya Malaysia ya MH370, iliyotoweka.

Inaaminika kuwa mabaki hayo ni kipande cha bawa la ndege hiyo ya MH370
Mabaki hayo yamehifadhiwa katika kambi ya jeshi iliyoko katika mji wa Toulouse.

Wataalamu hao watachukua alama za rangi na alama nyingine yeyote ile itakayowasaidia katika utambuzi wa ndege hiyo.


Sehemu iliyoshikana na ndege pia inachunguzwa ili kujua ilimeguka kutoka wapi.

Ndege hiyo ya MH370, ilitoweka angani mwezi Machi mwaka jana ikiwa na abiria 239 na wahudumu wa ndege.

chanzo: BBC SWAHILI

Wanachama wavamia ofisi za CUF Dar

WANACHAMA wa Chama cha Wananchi (CUF) wamevamia makao makuu ya chama hicho leo asubuhi na kusababisha kikao cha mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba na wanahabari kuhairishwa.
Mkutano wa mwenyekiti huyo ulikuwa ufanyike leo saa nne asubuhi makao makuu ya Cuf yaliyopo Buguruni, Dar es Salaam lakini hadi saa tano, mwenyekiti alikuwa kwenye kikao cha ndani na “wazee wa chama” waliokuwa wanataka ufafanuzi kwa baadhi ya mambo.
“Wazee wanataka ufafanuzi kwa baadhi ya mambo ikiwa ni pamoja na taarifa zilizoenea kuwa amejiuzulu,” amesema Magdalene Sakaya, Naibu Katibu Mkuu Bara amewaamabia wanahabari.
Hata hivyo, wananchama waliokuwa nje wakati mwenyekiti Lipumba akiendelea na kikao cha ndani cha chama hicho walionyesha kushtushwa na taarifa zilizochapishwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii kuwa Profesa Lipumba ameachana na siasa za chama hicho.
Wasiwasi huo uliongezeka jana mara baada ya mtaalamu huyo wa uchumi kutoonekana wakati wa kumtangaza Edward Lowassa kuwania urais kupitia Chadema, moja ya chama kinachounda Ukawa huku Juma Duni Haji akipitishwa kama mgombea mwenza.

Thursday, July 30, 2015

Haya ni mabaki ya ndege ya Malaysia?


Mamlaka ya usafirishaji nchini Ufaransa imesema inachunguza mabaki ya ndege ya yanayodaiwa kupatikana ndani ya Bahari ya Hindi yanachunguzwa ili kubaini kama ni ya ndege ya Malaysia ya MH370 iliyopotea bila kuwa na taarifa zozote kwa muda mrefusasa.
Taarifa kutoka Marekani zinasema wachunguzihao ambao wameona picha za mabaki hayo wana uhakika mkubwa kwamba ni ya ndege hiyo ya Malaysia ambapo mabaki hayo ni sehemu ya bawa la ndege.
Hata hivyo, Wataalamu wa Ufaransa wanasema ni mapema mno kutoa uhakika kwamba mabaki hayo ni lazima yatakuwa ya ndege ya Malaysia aina ya Boeing 777 ambayo kupotea kwake kumeleta gumzo la kidunia.
Watu wapatao 239 waliokuwa wakisafiri na ndege hiyo walipoteza maisha.
Akizungumza mjini New York Marekani, Waziri wa Usafirishaji wa Malaysia Liow Tiong Lai amesema nchi yake imetuma wataalamu zaidi kuchunguza mabaki hayo.
"Tunahitaji kuthibitisha" amekaririwa akisema Waziri Lai,na kusisitiza kuwa kwa vyovyote vile, mabaki yaliyopatikana yanahitaji kuhakikishwa kabla ya kuthibitisha zaidi kama ndio hasa mabaki ya MH370.

Naibu Spika adaiwa kumpiga mgombea CCM

sdf
Dk. Joseph Chilongani aliyepigwa akiwa amezimia.
Job Ndugai
Job Ndugai.

Dodoma. Kampeni za wagombea ubunge wa Jimbo la Kongwa juzi zilikumbwa na tafrani baada ya Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai kudaiwa kumchapa fimbo na baadaye kumpiga ngumi mgombea mwenzake aliyeanguka na kuzirai.
Mgombea huyo, Dk Joseph Chilongani, ambaye hivi sasa amelazwa Hospitali ya Wilaya ya Kongwa, alipata kipigo hicho juzi saa 10.20 jioni wakati walipokuwa kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Ugogoni wilayani Kongwa.
Kwa kawaida, wagombea ubunge wa CCM hupelekwa pamoja na chama hicho kwenye mikutano ya kampeni ya kila kata ambako hujieleza kwa wanachama kabla ya siku ya kupigiwa kura.
Mpambe wa Dk Chilongani, Shaaban Chihimba alimwambia mwandishi wetu kuwa Ndugai alimshambulia mpinzani wake kutokana na kukasirika baada ya mgombea mwingine, Simon Katunga kujinadi kwa kuponda utendaji wa mbunge wa sasa wa Kongwa.
“Mgombea huyo alisema fedha zinazochangwa na wananchi kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika halmashauri yetu zimekuwa zikiliwa hivyo akichaguliwa atahakikisha fedha hizo zinatumika kwa mambo yaliyokusudiwa,” alidai Chihimba.
 Alisema kuwa kauli hiyo ilionekana kumkera  Ndugai, hali iliyomfanya kusimama na kutaka kwenda kumpiga mgombea huyo, lakini viongozi wa CCM walimzuia.
 “Akiwa anataka kuketi, alimuona Dk Chilongali akirekodi tukio hilo kwa kutumia simu ya mkononi, ndipo alipomwendea na kumpiga ngumi za usoni na fimbo kwenye tumbo hali iliyosababisha kuanguka chini na kuzirai,” alidai.
Video ambayo imesambaa kwenye mitandao ya kijamii, inamuonyesha Ndugai akiwa ameshikilia fimbo mkononi huku akisema “embu na wewe usinipige, unanipiga makamera ya nini?”
Chihimba alidai kuwa baada ya mgombea huyo kuanguka, mkutano huo ulivurugika na wagombea wengine wakishirikiana na baadhi ya wanachama walimchukua Dk Chilongani na kumpeleka kabla ya kupelekwa hospitali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema jana jioni kuwa Dk Chilongani alifika Kituo cha Polisi Kongwa na kutoa taarifa za kushambuliwa kichwani na tumboni kwa fimbo.
“Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kwa kuwahoji watu waliokuwapo na mara baada ya upelelezi kukamilika jalada litapelekwa kwa wakili wa Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa hatua stahiki za kisheria,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Ndugai alijibu kupitia ujumbe mfupi wa simu akisema: “Ni kweli kumetokea mtafaruku, lakini hakuna aliyepigwa ngumi. Na katika maisha yangu sijawahi kumpiga mtu ngumi.”
Mganga mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Dk Festo Mapunda alikiri kupokewa kwa mgombea huyo juzi jioni lakini alikataa kuzungumza zaidi.
Kaimu Katibu wa CCM Wilaya ya Kongwa, Peter Minja alikiri kutokea kwa tukio hilo lakini akasema si kwa ukubwa huo. “Leo asubuhi (jana), tutakuwa na kikao cha kulijadili na baadaye tutatoa taarifa... tunaendelea na kampeni,” alisema Minja.
Hata hivyo, Minja alikataa kuthibitisha iwapo ni kweli mgombea huyo alipigwa au kukanusha kwa madai kuwa hakuwepo eneo la tukio.
“Tulishamuita mgombea huyo na kumuonya kuhusu kujinadi kwa kukipaka matope chama na halmashauri kwa sababu Halmashauri ya Kongwa imepata cheti safi cha (Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali - CAG), lakini hakusikia aliendelea.
“Tumepata taarifa ya maneno, lakini tunasubiri ya maandishi, taarifa ya polisi na hospitali kwa kuwa utaratibu wa chama unasema kila mwenye malalamiko awasilishe katika vikao husika.”
Minja alisema alikwenda jana hospitalini kumuona mgonjwa huyo, lakini hakuweza kuzungumza naye.
Hata hivyo, alisema jana polisi waliwahoji baadhi ya viongozi, wanachama na wagombea kuhusu tukio hilo.
Alisema tukio hilo limesababisha mchakato wa kampeni za kura za maoni kusimama hadi leo.
“Tulikuwa tumebakiza kata mbili za Sejeli na Kongwa Mjini ambazo zimesalia kwa watia nia kupiga kampeni na hizi tutamalizia kesho,” alisema.

Wednesday, July 29, 2015

Mwigulu ahojiwa na Takukuru kwa rushwa



“Kuna baadhi walilalamika hadi kususia kampeni
“Kuna baadhi walilalamika hadi kususia kampeni lakini tumesuluhishwa na tunaendelea na kampeni,” Nchemba  

Singida/Tanga. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Singida, inamhoji Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba kwa tuhuma za kukiuka Sheria ya Gharama za Uchaguzi na Sheria ya Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Singida, Joshua Msuya alisema kwenye taarifa yake kwa umma na vyombo vya habari jana kuwa Mwigulu alianza kuhojiwa na Takukuru Wilaya ya Iramba kuanzia juzi na hadi jana alikuwa bado anaendelea kuhojiwa dhidi ya tuhuma zinazomkabili.
Hata hivyo, Mwigulu alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo alisema Takukuru ilikuwa imeandaa kikao cha usuluhishi miongoni mwa wagombea wa vyama vyote baada ya kuwapo kwa malalamiko kutoka miongoni mwao.
“Kuna baadhi walilalamika hadi kususia kampeni lakini tumesuluhishwa na tunaendelea na kampeni,” alisema.
Hivi karibuni wapinzani wa Mwigulu, David Jairo, Amon Gyuda na Juma Kilimba, walipeleka malalamiko Takukuru kuwa Mwigulu amekuwa akitoa ahadi za kuwapa wananchi wa jimbo lake pikipiki, baiskeli na kukarabati barabara kwa fedha zake katika kipindi cha kampeni, kitendo ambacho ni kinyume na sheria za uchaguzi.
Msuya aliwatahadharisha wagombea wa udiwani na ubunge mkoani hapa kutojihusisha na vitendo vya rushwa kwenye kampeni za kura za maoni na Uchaguzi mkuu.
Alisema watakaobainika kukiuka sheria hiyo kwa kutoa rushwa ya fedha taslimu, madawati, vifaa vya michezo au rushwa ya aina nyingine yoyote, watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Takukuru Tanga yaonya
Uongozi wa Takukuru Mkoa wa Tanga, umedhamiria kuwabana wagombea ubunge na udiwani kutokana na malalamiko kwamba baadhi wamekuwa wakitoa rushwa.
Tayari taasisi hiyo imeanza kuwahoji baadhi ya wagombea wanaotuhumiwa huku ikifuatilia kwa siri michakato ya uchaguzi katika vyama vyote vya siasa pamoja na kutoa elimu ya Sheria namba 6 ya Uchaguzi ya mwaka 2010.
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Tanga, Aidano Ndomba alisema jana kuwa wagombea watambue kwamba taasisi hiyo ipo kazini na itawabana wote watakaobainika kutoa au kupokea rushwa.
“Tumeanza kuchukua hatua ya kuwahoji na kukusanya ushahidi kwa baadhi ya wagombea ambao wamelalamikiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa,” alisema Ndomba na kusisitiza kuwa maofisa wa Takukuru wanafuatilia kwa siri michakato yote.

Tuesday, July 28, 2015

Mtuhumiwa kinara mauaji ya polisi

IMG_0240 
Kinara, Selemani Shabani Ulatule.


WAKATI jeshi la polisi nchini likiendelea kuwasaka watuhumiwa wa mauaji ya polisi na kupora silaha katika Kituo cha Stakishari, Ilala jijini Dar, Uwazi limefanikiwa kuipata picha ambayo inadaiwa ni ya mtuhumiwa kinara wa tukio hilo aliyetajwa kwa jina la Seleman Shaban Ulatule.
STAKI SHALI (1)
Ngome ya majambazi hao ilivyoteketezwa.

ENEO LA TUKIO
Mwishoni mwa wiki iliyopita, wanahabari wetu walifika katika Kijiji cha Mandikongo, Mkuranga,  Pwani na wakazi wa maeneo ya jirani wakiwa katika hofu baada ya watuhumiwa hao waliokuwa wakiishi jirani na kijiji hicho kutoweka.
 
STAKI SHALI (2) 

NGOME YAO YATEKETEZWA
Wanahabari wetu walioambatana na afisa mtendaji wa Kijiji cha Mandikongo, polisi na wanajeshi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), walishuhudia makazi ya watu hao yakiwa yameteketezwa kwa moto na wananchi wenye hasira kali.

WANANCHI WAZUNGUMZA
Wakizungumzia tukio hilo, wakazi wa kijiji hicho walisema majambazi hao waliokuwa wamejitenga na makazi ya wanakijiji, walitoweka na familia zao baada ya kupata taarifa kuwa kuna msako mkali unaofanywa na jeshi la polisi ambao ulifanikiwa kuwakamata baadhi ya watuhumiwa, bunduki 15 za kivita na fedha zaidi ya shilingi milioni 170.

STAKI SHALI (6)Shimo ambamo zilifichwa millioni 170.

WALIVYOFICHA FEDHA
Wakizidi kuelezea tukio hilo, wakazi hao waliwaonesha waandishi wetu shimo ambalo walilitumia kuhifadhia fedha hizo ambapo juu yake waliweka kinyesi cha binadamu kilichokadiriwa kuwa ni cha watu saba ikiwa ni alama yao ambayo pia itamfanya mtu akisogelea eneo hilo alipitie mbali kwa kuona kinyaa.
STAKI SHALI (7) 
“Tunaomba vyombo vya usalama kuhakikisha watuhumiwa wote wanapatikana na silaha nzito walizokimbia nazo maana wanaweza kuja kukivamia kijiji hiki na kufanya unyama wa kutisha pindi vikosi vya usalama vitakapoondoka hapa,” alisema mkazi mmoja wa kijiji hicho aliyeomba hifadhi ya jina lake gazetini.

MTENDAJI AZUNGUMZA
Afisa mtendaji wa kijiji hicho, Issa Said Mchalaganga aliwataja watuhumiwa ambao walikuwa wakiongozwa na kinara wao Seleman Shaban Ulatule ni pamoja na Said Mohamed Ulatule, Ally Mohamed Ulatule, Hamis Mohamed Ulatule, Haji Seleman Ulatule na Ally Said Ulatule.
“Hao wote walikimbia nyumba zao na baadaye kuharibiwa na wananchi kwa kuteketezwa kwa moto,” alisema Mchalaganga.

STAKI SHALI (3)…Iliyokuwa ngome yao.

WALIOKAMATWA
“Katika msako wa vyombo vya usalama walifanikiwa kumkamata Ramadhani Hamis Ulatule na mwenyekiti wa kijiji, Ramadhani Mohamed Ulatule kwa ajili ya mahojiano na kwa kweli tunampongeza Kamishna Suleiman Kova na vyombo vya usalama kwa kazi nzuri ya kubaini kikundi hiki na kufanikiwa kupata baadhi ya silaha,” alisema mtendaji huyo.

STAKI SHALI (4)Baadhi ya nguo zao walizoziacha kwenye ngome hiyo.

MAISHA YAO KIJIJINI HAPO
Wananchi wa kijiji hicho waliliambia Uwazi kuwa, watu hao ambao wanadaiwa kuwa majambazi kabla ya kubainika, walikuwa wakiishi maisha ya usiri na wakifanya mafunzo ya kijeshi porini.

WALIJITENGA NA SERIKALI
“Hawakupenda kushiriki na wanakijiji katika shughuli za maendeleo, upigaji kura, uhesabuji wa watu hata hospitali ya hapa walikuwa hawaji kupata huduma na haikujulikana walikokuwa wakipatia matibabu,” alisema mwanakijiji mmoja.

STAKI SHALI (5)Sehemu ya jiko.

YADAIWA KUNA ASKARI ALIYEKUWA AKIWATEMBELEA
Wananchi wa kijiji hicho walidai kuwa, kulikuwa na askari mmoja wa Gereza la Dondwe lililopo karibu na kijiji hicho ambaye alikuwa rafiki wa majambazi hao aliyekuwa akiwatembelea mara kwa mara katika makazi yao.
“Huyo askari tulikuwa tunamuona akienda huko porini mara kwa mara sasa tangu tukio litokee hajaonekana, tunaiomba serikali imfuatilie,” alisema mkazi mwingine wa kijiji hicho.

ushahidi makongoro 

WALIKATAA KUHESABIWA
Afisa mtendaji wa kijiji hicho aliwaeleza waandishi wetu kuwa walimtilia shaka kiongozi wa ukoo wa Ulatule, Seleman Shaban ambaye aliwahi kuandikiwa barua na mkuu wa Wilaya ya Mkuranga yenye kumbukumbu namba AB/226/290/1/40 ya Agosti 31, mwaka 2012 (nakala tunayo) ikimhoji kwa nini aliwakataza watu wa eneo lake kuhesabiwa kwenye sensa.
“Hapo ndipo tulipotilia shaka haswa baada ya tukio hili kutokea. Seleman alikuwa hataki kabisa kujihusisha na shughuli za serikali. Hata wakati wa zoezi la sensa aliwakataza watu wa eneo lake kuhesabiwa,” alisema mtendaji huyo.

WALIISHI NA RAIA WA KIGENI
Uchunguzi unaonesha kwamba watu hao hawakupenda wananchi kutembelea wala kukatisha katika makazi yao na kulikuwa na nyumba nyingine jirani ambazo zinadaiwa walikuwa wakiishi watu wasio Watanzania. 

SABABU YA KUVAMIA VITUO VYA POLISI NI NINI?
Inadaiwa kuwa kuna majambazi wana mpango wa kuanzisha kikosi kikubwa kama jeshi la kupambana na dola ambayo imewashikilia wafuasi wao katika magereza mbalimbali nchini.
Imeelezwa kwamba, utaratibu huo ulikwepo tangu zamani na walikuwa wakipata silaha za kivita kutoka kwa wakimbizi wa nchi jirani lakini hali hiyo ikadhibitiwa na serikali kukawa hakuna silaha inayoingia nchini kinyume na taratibu.

WABADILI MBINU
Inasemekana kwamba baada ya kuwa na uhaba wa silaha wakawa wanawavamia polisi katika vituo, mabenki na popote pale wanapofanyia doria wakiwa na silaha kisha kuwapora.
Uchunguzi mwingine unaonesha kwamba walioua katika Kituo cha Polisi Stakishari ni baadhi ya kikosi chao na baada ya kufanya mauaji walipitia Barabara ya Nyerere na kuingia Banana kuelekea Kitunda, Msongola, Mbande kisha kuingia katika pori la Kijiji cha Mandikongo.

KAMISHNA KOVA ANENA
Kamishna Kova alipoulizwa kuhusu mzee Ulatule na sakata zima la kambi hiyo ya watu hao waliotoroka alisema, suala hilo atalizungumzia Ijumaa kwa sababu ndiyo siku aliyopanga kuzungumza na waandishi wa habari.
“Siku hiyo ndiyo niliyopanga kuzungumza na waandishi wa habari hivyo uje na swali hilo nitalijibu,” alisema.

TUJIKUMBUSHE
Julai 12, mwaka huu watu wanaokadiriwa 16 walifanya uvamizi katika Kituo cha Polisi Stakishari na kuua polisi wanne na raia watatu kisha kupora silaha zaidi ya 24 ambapo Kamanda wa Kanda Maalum ya Kipolisi Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, SACP Lucas Mkondya waliapa kuwakamata watuhumiwa hao na silaha walizoiba.
Msako wa polisi katika ngome hiyo iliyokuwa jirani na Kijiji cha Mandikongo, polisi walifanikiwa kupata bunduki 15 ambazo baadhi ni zile zilizoporwa katika Kituo cha Stakishari.

Chanzo: Global Publishers

Hotuba ya Lowassa kujiunga Chadema

Ndugu waandishi wa habari na ndugu Watanzania wenzangu.
Yamepita majuma mawili tangu mchakato wa kuchagua mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) ukamilike. Nimetumia muda huu kutafakari kwa kina yaliyotokea Dodoma na hatima yangu katika siasa nchini. Ninajua marafiki wengi na wananchi wenzangu wanaoniunga mkono wamekuwa wakisubiri kwa hamu nitoe kauli.
Nilipokuwa natangaza nia ya kugombea urais kule Arusha, nilieleza nia yangu ya kuanza mchakamchaka wa maendeleo ya nchi yetu na kuondokana na umaskini. Pamoja na yaliyotokea Dodoma, azma hii bado iko palepale.
Lakini nianze kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetupa sisi pumzi ya kuendelea kuwa wazima wa afya njema hadi hivi sasa. Nawashukuru pia mke wangu Regina, wanangu, wanafamilia na marafiki wote kwa mapenzi, msaada na uvumilivu wao wakati wa kipindi hiki kigumu tunachopitia. Nawashukuru sana pia maelfu ya wanachama wa CCM walionidhamini na mamilioni zaidi walioniunga mkono.
Katika safari zangu za mikoani wakati wa kuomba udhamini, nilitiwa hamasa na umati mkubwa wa watu waliojitokeza kuniunga mkono.Aidha, ninawashukuru sana wana kamati wangu, makundi mbalimbali na mamilioni ya vijana wakiwamo; “For You Movement”, “Friends of Lowassa” “Team Lowassa”, Umoja wa Bodaboda na wengine wengi ambao walijitolea kwa hali na mali katika Safari yetu ya Matumaini.
Nitakuwa sijahitimisha orodha ya shukrani iwapo nitaacha kuwashukuru viongozi wa dini zote nchini ambao waliungana na waumini wao wengi katika maombi na kwa kuniunga mkono. Najua sote tumevunjika moyo kwa yaliyotokea Dodoma na mazingira yaliyopelekea matokeo yale.
Kama ilivyokwishaelezwa, mchakato wa kuteua wagombea uligubikwa na mizengwe, ukiukwaji wa maadili, uvunjaji wa Katiba na taratibu za uchaguzi za CCM.
Zaidi ya hayo uchaguzi ulisimamiwa kwa upendeleo dhahiri na chuki iliyokithiri dhidi yangu. Kikatiba, Kamati ya Maadili si chombo rasmi na haina madaraka ya kuchuja na kupendekeza majina miongoni mwa wale wanaoomba kugombea Urais kupitia CCM.
Kilichotokea Dodoma ni kupora madaraka ya Kamati Kuu na kukiuka katiba ya CCM. Aidha, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu viliitishwa na kuburuzwa ili vitekeleze azma ya watu binafsi pasipo kujali demokrasia, katiba, kanuni na taratibu za uchaguzi ndani ya CCM. Niliwekewa mizengwe na kuzushiwa majungu na uongo mwingi, kuhakikisha kuwa jina langu halifikishwi mbele ya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu kujadiliwa licha ya ukweli usiopingika kuwa nilikuwa mgombea anayeungwa mkono na wananchi na wanachama wengi wa CCM kuliko wenzangu wote. Kibaya zaidi ni kile kitendo cha kuwanyima wagombea wote 38 haki ya kujieleza mbele ya Kamati Kuu.
Ni dhahiri kwamba njama dhidi yangu ndani ya CCM si jambo jipya.Kumekuwa na mkakati wa siku nyingi wa kulichafua jina langu kwa uzushi na uongo usio na kifani. Aidha, mmeshuhudia jinsi vijana kadhaa walivyotumika kunikashifu na kunitukana na bila aibu na uongozi wa CCM na Serikali kuwazawadia madaraka makubwa.
Kwa namna ya kipekee napenda kuwapongeza na kuwashukuru wazee wetu akiwamo Mzee Kingunge Ngombale Mwiru na baadhi ya  wajumbe wa Kamati Kuu ikiwa ni pamoja na waheshimiwa Emmanuel Nchimbi, Sophia Simba na Alhaj Adam Kimbisa kwa uadilifu na ushujaa wao mkubwa wa kuisimamia katiba ya CCM na misingi ya haki na kukataa maamuzi batili ya Kamati ya Maadili na Kamati Kuu kuhusu uteuzi wa wagombea.
Cha msingi kuzingatia ni kuwa ili kuhitimisha njama za kunipora mimi na wagombea wengine haki zetu za msingi za kusikilizwa, viongozi wachache walikuwa tayari kupanda mbegu ya chuki na mfarakano ambao ni mfano mbaya kwa CCM na hata Taifa letu. Watanzania walitarajia chama kinachoongoza nchi kiwe ni mfano wa utawala wa sheria na kinara katika kutetea misingi ya haki na demokrasia na siyo kuihujumu. Yaliyotokea Dodoma yameitia dosari nchi yetu.
Kwa kifupi, ninaamini sikutendewa haki katika mchakato mzima wa kupendekeza majina na kuteua mgombea wa urais kupitia CCM. Nilinyimwa haki yangu ya msingi ya kusikilizwa na kuchaguliwa.
Kwa mantiki hii nitakuwa mnafiki kama nitaendelea kujidanganya mimi mwenyewe na umma wa Watanzania kwa kusema kuwa bado nina imani na CCM au kuwa CCM ni chama kitakachowaletea ukombozi wa kweli wa kiuchumi, kisiasa na kijamii. CCM niliyoiona Dodoma siyo tena kile chama nilichokulia na kilichonipa malezi na maadili ya siasa yaliyojengwa kwenye misingi ya haki, usawa na uadilifu.
Ni dhahiri kwamba CCM imepotoka na kupoteza mwelekeo na sifa ya kuendelea kuiongoza Tanzania yetu. Mimi kama Mtanzania aliye na uchungu na nchi yake nasema imetosha na SASA BASI!
Kama Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alivyosema, CCM siyo baba yangu wala mama yangu na kwamba kama Watanzania hawapati mabadiliko ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM. Sasa tuyatafute mabadiliko nje ya CCM.
Hivyo basi, baada ya kutafakari kwa kina nimeamua kuwa kuanzia leo ninaondoka CCM na kuitikia wito wa Ukawa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuungana nao katika kuleta mabadiliko ya kweli ya nchi yetu. Navishukuru vyama vyote vya siasa chini ya Ukawa, yaani Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD kwa mwaliko wao na imani yao na kuthamini mchango ninaoweza kutoa kufanikisha azma ya kuleta mabadiliko na maendeleo ya kweli ya Taifa letu. Waheshimiwa Freeman Mbowe, Profesa Ibrahim Lipumba, Mheshimiwa James Mbatia na Emmanuel Makaidi asanteni sana.
Ndugu zangu, sikuufanya uamuzi huu kwa pupa, lakini unafika wakati wa kuchukua maamuzi hata kama ni magumu  kwa kuamini fika kuwa ni kwa masilahi ya Taifa letu.
Nimejiridhisha kuwa ndani ya Ukawa Taifa letu linayo fursa ya pekee na ya kihistoria kushinda Uchaguzi Mkuu ujao na ya kuleta mabadiliko ya msingi katika nchi yetu. Kwa uamuzi na ushiriki wangu huu, ninaamini kwa dhati kuwa tutaondoa uhodhi wa madaraka wa chama kimoja na kujenga demokrasia yenye ushindani wa kweli kisiasa.
Namalizia kwa kutoa wito kwa Watanzania wenye nia njema na nchi yetu na wanaotaka kujenga demokrasia na kuleta mageuzi na maendeleo ya kweli, kujiunga nasi katika safari hii mpya ya kuinusuru nchi yetu.
Safari ya Matumaini inaendelea kupitia Ukawa lakini haitafanikiwa iwapo sote hatutajiandisha kupiga kura. Natoa wito kwa wakazi wa Dar es salaam, kutumia fursa iliyopo kujiandikisha kwa wingi.
Aidha, nawakumbusha Watanzania kote nchini waliojiandikisha kutunza shahada zao na kukumbushana kupiga kura ili ifikapo Oktoba mwaka huu tupate ushindi wa kishindo.
Ndugu zangu Watanzania, tuungane pamoja kuuondoa umaskini na kuleta mabadiliko ya kweli.
NARUDIA CCM SIYO MAMA YANGU