Namshukuru
Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha
kumaliza mwezi Septemba salama na kuwasiliana kwa kutumia utaratibu wetu
huu mzuri. Naomba radhi kuzungumza nanyi siku ya leo kwa sababu
nilikuwa safari na nilirejea jioni ya tarehe 30 Septemba, 2013. Awali
nilifikiria nisiseme, nisubiri mwisho wa mwezi wa Oktoba. Lakini, baada
ya kupata taarifa ya yaliyojiri, nimeshauriwa na nimekubali angalau
niyasemee baadhi ya mambo huenda itasaidia. Niwieni radhi nisipoyasemea
baadhi ya mambo siyo kwa kuyapuuza, bali kwa kuepuka hotuba kuwa ndefu
mno. Nitayatafutia mahali pengine pa kuyasemea.
Uhusiano na Rwanda
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi wa Julai, nilizungumzia hali
ya uhusiano wetu na Rwanda kutokuwa mzuri na tatizo la ujambazi na
wahamiaji haramu katika Mikoa ya Kigoma, Geita na Kagera. Nafurahi
kusema kuwa kwa yote mawili kuna maendeleo ya kutia moyo.
Tarehe 5 Septemba, 2013, nilikutana na kuzungumza na Mheshimiwa Rais
Paul Kagame wa Rwanda mjini Kampala. Tuliitumia fursa ya ushiriki wetu
katika Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu kuzungumzia uhusiano baina yetu
na nchi zetu. Mazungumzo yalikuwa mazuri na sote tulikubaliana kuwa
yaliyopita si ndwele tugange yajayo. Kwa sababu hiyo tulielewana kuwa
tutengeneze mazingira yatakayosaidia kutuliza hali na kurudisha nchi
zetu katika uhusiano mwema kama ilivyokuwa siku zote. Nawaomba ndugu
zangu hususan wanasiasa, watumishi wa umma, wanahabari na wenye mitandao
ya kijamii na blog na wananchi kwa ujumla tusaidie kuimarisha uhusiano
mwema baina ya Rwanda na Tanzania na watu wake.
Majambazi na Wahamiaji Haramu
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba hiyo pia nilisema kuwa tutachukua hatua thabiti dhidi
ya majambazi na wageni wanaoishi nchini bila ya kuzingatia taratibu
zinazohusika. Niliwataka majambazi wajisalimishe wao na silaha zao kwa
hiari. Wale wanaoishi nchini bila ya kuwa na kibali halali wahalalishe
ukaazi wao au warejee makwao. Nilitoa siku 14 kuanzia tarehe 29 Agosti,
2013 wafanye hivyo kwani baada ya hapo tungeanzisha operesheni maalum
ya kushughulika na watu wa makundi yote mawili.
Ndugu Wananchi;
Kumekuwepo na mafanikio ya kutia moyo. Kwa upande wa wahamiaji
wanaoishi nchini kinyume cha sheria watu wapatao 21,254 waliondoka kwa
hiari. Hali kadhalika zaidi ya ng’ombe 8,000 waliondolewa na silaha 102
zilisalimishwa. Baada ya operesheni kuanza tarehe 6 Septemba, 2013 na
kumalizika tarehe 20 Septemba, 2013, wahamiaji haramu 12,828
walirejeshwa makwao na watuhumiwa 279 wa unyang’anyi wa kutumia silaha
walikamatwa. Aidha, mabomu 10 ya kutupa kwa mkono (offensive hand
grenades), silaha 80, risasi 780 na mitambo 2 ya kutengeneza magobole
vilikamatwa. Pia, ng’ombe 8,226 walikamatwa wakichungwa katika mapori
ya hifadhi. Kwa upande wa mazao ya misitu, mbao 2,105 zilikamatwa
pamoja na nyara mbalimbali za Serikali.
Ndugu Wananchi;
Agizo la kuwataka watu wanaoishi nchini isivyo halali wahalalishe
ukaazi wao au waondoke kwa hiari au wataondolewa lilipotoshwa hasa na
vyombo vya habari vya nje ya Tanzania. Walikuwa wanadai eti Tanzania
ilikuwa inafukuza wakimbizi. Madai hayo si ya kweli hata kidogo. Hadi
kufikia tarehe 30 Septemba, 2013 wakimbizi 68,711 walikuwepo kwenye
Kambi ya Nyarugusu, Mkoani Kigoma. Hakuna mkimbizi ye yote aliyetakiwa
kuondoka. Ukweli ni kwamba hakuna mtu ye yote kati ya wale watu
walioondoka kwa hiari au kusaidiwa kuondoka wakati wa operesheni ambaye
ni mkimbizi. Kama ingekuwa hivyo, wa kwanza kulalamika wangekuwa
wenzetu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa. Bahati nzuri jambo
hilo halikutokea.
Ndugu Wananchi;
Yalikuwepo pia madai kwamba tunawaonea na kuwatesa watu walioishi
nchini miaka mingi. Ati iweje sasa ndiyo waambiwe kuwa siyo raia. Siku
zote Serikali ilikuwa wapi? Uraia haupatikani kwa kuishi nchi ya kigeni
kwa miaka mingi. Unapatikana kwa kutimiza masharti ya kuomba na kupewa
uraia. Kama mtu hakufanya hivyo anabaki kuwa raia wa nchi aliyotoka au
walikotoka wazazi wake. Ipo mifano ya watu mashuhuri ambao
walilazimika kuachia nyadhifa zao baada ya kugundulika kuwa siyo raia.
Hawakuwa wanaonewa, ndiyo matakwa ya Katiba na Sheria za nchi yetu.
Ndugu Wananchi;
Katika kutekeleza operesheni hii niliagiza kuwa wale watu ambao
wameishi hapa nchini miaka mingi ambao wana nyumba, mashamba au mali
mbalimbali au wameoa au kuolewa na wana watoto au hata wajukuu
waelekezwe kuhalalisha ukaazi wao. Iwapo watakataa kufanya hivyo basi
wasaidiwe kurejea kwao. Pia niliagiza watu wasiporwe mali zao wala
kudhulumiwa. Sijapata taarifa ya kufanyika kinyume na maelekezo yangu.
Lakini kama wapo watu waliotendewa tofauti, taarifa itolewe kwa Wakuu
wa Wilaya na Mikoa au hata Ofisi ya Rais ili hatua zipasazo
zichukuliwe. Hatutaki watu wadhulumiwe au kuonewa.
Napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Waziri wa Ulinzi na JKT,
Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa
Emmanuel Nchimbi kwa uongozi wao mzuri katika zoezi hili. Pia,
nawapongeza Makamanda na askari wa JWTZ na Polisi pamoja na maafisa wa
Idara ya Uhamiaji, Idara ya Mifugo, Idara ya Wanyamapori, Idara ya
Misitu na Idara nyinginezo za Serikali kwa kazi kubwa na nzuri
waliyofanya. Najua awamu ya kwanza imeisha tarehe 20 Septemba, 2013 na
kama nilivyosema kuwa safari hii operesheni itakuwa endelevu, muda si
mrefu awamu ya pili itafuata. Nawaomba waendelee kuchapa kazi kwa
bidii, maarifa na nidhamu ya hali ya juu.
Ziara ya Canada na Marekani
Ndugu Wananchi;
Kati ya tarehe 17 na 28 Septemba, 2013 nilifanya ziara ya kikazi
katika nchi za Canada na Marekani. Nchini Canada nilitembelea Chuo
Kikuu cha Guelph ambapo nilitunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu kwa
kutambua jitihada zetu tuzifanyazo kujiletea maendeleo na mafanikio ya
kutia moyo tunayoendelea kupata licha ya changamoto zinazotukabili.
Katika mazungumzo yangu na uongozi wa chuo hicho wamekubali kuwa na
ushirikiano wa karibu na Wizara zinazohusika na Elimu, Kilimo na Mifugo
pamoja na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Morogoro na Chuo Kikuu cha
Dodoma. Nimewataka Mawaziri wa Wizara hizo na viongozi wa vyuo hivyo
kuchangamkia fursa hiyo bila kuchelewa.
Ndugu Wananchi;
Nchini Marekani nilikutana na kuzungumza na maafisa na viongozi
mbalimbali wa Serikali ya nchi hiyo wakiwemo Rais Barack Obama na baadhi
ya Wabunge wa Bunge la Marekani. Mazungumzo yetu yalilenga kuimarisha
ushirikiano baina ya nchi zetu na mambo yalienda vizuri. Wote
walituhakikishia kuwa mambo tuliyoyazungumza na kukubaliana na Rais
Barack Obama wakati wa ziara yake nchini yanaendelea kufanyiwa kazi.
Miongoni mwa hayo maombi yetu ya kupatiwa vitabu milioni 2.4 vya sayansi
na hisabati yamekubaliwa na utekelezaji umeanza. Upatikanaji wa vitabu
hivyo utamwezesha kila mwanafunzi wa sekondari kuwa na kitabu chake.
Ndugu Wananchi;
Jambo lingine kubwa na la faraja kwetu ni kuwa mapendekezo yetu ya
miradi ya umeme na barabara za vijijini za kugharamiwa na Serikali ya
Marekani kupitia Shirika lao la Changamoto za Milenia yamepokelewa
vizuri. Kinachosubiriwa ni miradi ipi itakubaliwa na Bodi ya MCC na
kiasi gani cha fedha kitatengwa na Bunge la Marekani kwa ajili hiyo.
Tuzo ya Uhifadhi
Jambo lingine muhimu katika safari yangu ya Marekani ni kutunukiwa
tuzo na “International Congressional Conservation Foundation” kwa
kutambua juhudi zetu katika kuhifadhi wanyama pori na mafanikio
tuliyoyapata. Licha ya changamoto mbalimbali tunazokabiliana nazo, tuzo
hii imetupa moyo wa kuongeza nguvu katika jitihada tunazozifanya sasa
kupambana na ujangili na matatizo mengine ya uhifadhi wa wanyama na
misitu.
Ndugu Wananchi;
Kilichotupa moyo zaidi ni kauli za utayari wa kutusaidia katika
mapambano hayo zilizotolewa wakati wa kupewa tuzo na katika mkutano wa
mfuko wa Maendeleo wa Clinton na katika mkutano maalum wa kupambana na
ujangili na biashara ya meno ya tembo duniani.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Ndugu Wananchi;
Shabaha kuu ya safari yangu ya Marekani ilikuwa kuhudhuria Mkutano wa
68 wa Umoja wa Mataifa unaoendelea jijini New York mpaka Desemba,
2013. Mada kuu ya mkutano wa mwaka huu ni kuandaa agenda ya maendeleo
baada ya mwaka 2015 yaani: Post 2015 Development Agenda: Setting the
Stage. Kama mtakavyokumbuka Malengo ya Milenia yaliyoamuliwa na Baraza
Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2000, yanafikia ukomo wa utekelezaji wake
mwaka 2015.
Katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka huu mjadala umehusu nini
kifanyike baada ya mwaka 2015. Hata hivyo, mjadala huo unaanza kwa
kufanya tathmini ya utekelezaji wa yale Malengo Manane ya Milenia ya
mwaka 2000 umefikia wapi mpaka sasa na utafikia wapi mwaka 2015 kwa kila
nchi na kwa dunia kwa ujumla. Tathmini ya jumla inaonesha kuwa
kumekuwepo na jitihada kubwa ya kutekeleza malengo haya katika kila
nchi. Yapo malengo ambayo utekelezaji wake umefikia shabaha hivi sasa
na yapo ambayo upo uwezekano wa shabaha kufikiwa ifikapo mwaka 2015.
Vile vile yapo ambayo shabaha haitafikiwa.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wetu, Tanzania, tumefikia shabaha katika mambo yafuatayo:
- Lengo la Milenia namba 2 kuhusu uandikishaji wa watoto wenye umri wa kwenda shule ya msingi;
- Lengo la Milenia namba 3 hasa kuhusu usawa wa kijinsia katika Shule
za Msingi na Sekondari. Ukweli ni kwamba, wasichana wanaanza kuwa wengi
kuliko wavulana. Hatujafikia shabaha kwa upande wa usawa wa kijinsia
katika elimu ya juu na ni vigumu kulifikia ifikapo 2015. Pia
hatujafikia lengo kwa upande wa usawa wa Wabunge wanawake na wanaume.
Hata hivyo, kwa kutumia mchakato wa Katiba unaoendelea sasa tunaweza
kufikia lengo katika uchaguzi wa 2015 iwapo tutaamua iwe hivyo;
- Lengo la Milenia namba 4 kuhusu kupunguza idadi ya vifo vya watoto wachanga na wale wenye umri chini ya miaka mitano;
- Tumefikia shabaha kwa Lengo la Milenia Namba 6 kuhusu kupunguza maambukizi ya UKIMWI; na
- Kwa upande wa lengo namba 7 kuhusu mazingira, tumefikia shabaha kwa
upande wa upatikanaji wa maji mijini. Bado tuko nyuma kwa maji vijijini
ingawaje tunaweza kufikia lengo ifikapo mwaka 2015 kama tutaendeleza
uwekezaji tulioamua kufanya katika bajeti ya mwaka huu. Lakini,
hatutaweza kufikia shabaha kwa upande wa usafi wa mazingira mijini na
vijijini ifikapo mwaka 2015. Safari bado ndefu sana.
Ndugu Wananchi;
Malengo ya Milenia namba 1 na namba 5 ambayo bado tuko nyuma sana ya
shabaha hatutafikia lengo ifikapo 2015. Tumeendelea kutekeleza lengo la
Milenia namba 1 kuhusu kupunguza umaskini na njaa kwa zaidi ya nusu
kutoka kiwango cha mwaka 2000. Hatua tunazochukua kuleta mageuzi katika
kilimo zina lengo la kuhakikisha usalama wa chakula na kuongeza mapato
ya wakulima. Mafanikio yanaanza kuonekana lakini si ya kiwango cha
kutufikisha kwenye lengo ifikapo mwaka 2015. Tunao, pia, mpango wa
kupanua programu ya TASAF ya Conditional Cash Transfer ili tuwafikie
watu wengi maskini. Hata kama tutafanikiwa kuutekeleza mapema mpango
huu utatusogeza sana mbele lakini bado tutakuwa chini ya lengo kwa
upande wa kupunguza umaskini ifikapo 2015.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa Lengo la Milenia namba 5, kuhusu afya ya kina mama
wajawazito bado tuko nyuma katika kupunguza vifo vya kina mama
wajawazito na kuongeza idadi ya wajawazito wanaojifungua chini ya
uangalizi wa wataalamu wa afya. Hatutaweza kufikia shabaha ifikapo
mwaka 2015. Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (2007 – 2017) una nia
ya kukabiliana na matatizo haya. Tumeongeza ujenzi wa zahanati, vituo
vya afya na hospitali, tumeboresha upatikanaji wa dawa na tumepanua sana
mafunzo ya madaktari, wauguzi na wakunga mambo ambayo yamesaidia
kutufikisha hatua tuliyopiga mpaka sasa. Naamini juhudi zetu
tukiziendeleza zitatusogeza mbele zaidi ingawaje bado tutakuwa chini ya
lengo. Miaka michache ijayo, tatizo hili nalo litakuwa historia.
Ndugu Wananchi;
Lengo la Milenia namba 8 linazihusu nchi tajiri kuongeza michango yao
kusaidia nchi zinazoendelea kutekeleza Malengo ya Milenia. Bahati
mbaya sana mataifa tajiri hayajafikia viwango wanavyotarajiwa kutoa na
hata vile wanavyoahidi wenyewe kutoa katika majukwaa mbalimbali. Kama
wangetimiza ahadi zao, sura ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia
ingekuwa tofauti kabisa.
Ndugu Wananchi;
Hiyo ndiyo hali ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia hapa nchini.
Hakuna nchi ye yote duniani iliyofanikiwa kutekeleza shabaha za malengo
yote kwa ukamilifu. Ushauri wa viongozi wote waliozungumza ulitaka
mataifa yaliyoendelea yatimize ahadi zao za kuchangia utekelezaji wa
Malengo ya Milenia. Ilionekana suala la upatikanaji wa fedha halina
budi kuangaliwa kwa makini sasa na baada ya mwaka 2015. Bila ya hivyo
ufanisi utakuwa mdogo katika kuongeza kasi ya utekelezaji kwa pale
paliposalia kufikia malengo ya 2015 na hata kwa Malengo ya baada ya
mwaka 2015.
Mashambulizi ya Kigaidi ya Westgate, Nairobi
Ndugu Wananchi;
Wakati nikiwa safarini, tarehe 21 Septemba, 2013 kulitokea
shambulilizi la kigaidi katika Jengo la Biashara la Westgate, huko
Nairobi, Kenya. Watu 67 walipoteza maisha na zaidi ya 200
walijeruhiwa. Nilituma salamu za pole na rambirambi kwa Mheshimiwa Rais
Uhuru Kenyatta na wananchi wa Kenya na kuwahakikishia kuwa tupo pamoja
nao katika wakati huu wa majonzi.
Nafahamu kuwa baada ya tukio hilo watu wengi hapa nchini wameingiwa
na hofu kuhusu usalama wetu. Ni hofu ya msingi kwani tarehe 8 Agosti,
1998 Ubalozi wa Marekani hapa nchini ulishambuliwa na magaidi na ndugu
zetu 11 wasio na hatia walipoteza maisha.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwafahamisha kuwa tangu shambulio la mwaka 1998, Serikali
imekuwa inajenga uwezo wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kupambana
na ugaidi katika nyanja mbalimbali. Tunaendelea kujiimarisha bila
kusita siku hadi siku. JWTZ, Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa
wamekuwa na ushirikiano wa karibu kwa ajili hiyo. Juhudi zetu hizo
ndizo zinazotufanya tuwe salama hadi sasa.
Baada ya tukio la Kenya, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama
vimeimarisha mikakati yao maradufu. Pamoja na kujizatiti kwetu huko
hatuwezi kusema kuwa tukio la kigaidi halitaweza kutokea nchini.
Uhakika huo hatuna kwani hata mataifa makubwa na tajiri
yameshambuliwa. Kilicho muhimu ni kuendelea kuchukua tahadhari na
wananchi kusaidia ili vyombo vyetu vifanikiwe zaidi.
Hali kadhalika, tumewataka watu wote wenye shughuli zinazokusanya
watu wengi kama vile maduka, maofisi, mahoteli, migahawa n.k. waweke
kamera za ulinzi nje na ndani ya maeneo yao. Pia waangalie uwezekano wa
kuweka vifaa vya upekuzi (metal detectors and x-rays). Najua watu
wanaweza kulalamikia usumbufu au gharama, lakini gharama na hasara ya
kushambuliwa ni kubwa zaidi kuliko ya usumbufu huo.
Ndugu Wananchi;
Nawaomba muendelee kufanya shughuli zenu bila ya hofu ingawaje
msiache kuwa makini na kuchukua tahadhari. Watu watoe taarifa kwa
vyombo vya usalama wanapoona mtu au watu au kitu cha kutilia shaka. Ni
muhimu kwa usalama wake, wa kila mtu, jamii na taifa. Maafisa husika wa
vyombo vya ulinzi na usalama wataendelea kuelimisha umma kuhusu hatua
mbalimbali za tahadhari za kuchukua. Sisi Serikalini tumejipanga
kuchukua hatua zaidi kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi yetu na watu
wake.
Mchakato wa Katiba Mpya
Ndugu Wananchi;
Kama mtakavyokumbuka, Bunge lilitunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
Novemba, 2011. Sheria hii imeweka mchakato mzima wa kupata Katiba hiyo
na kuunda taasisi zake. Mwezi Mei, 2012, Tume ya Mabadiliko ya Katiba
iliundwa na imekamilisha hatua tatu muhimu katika mchakato huo. Hatua
hizo ni kupokea maoni ya wananchi, kutayarisha rasimu ya kwanza ya
Katiba Mpya na kupokea maoni ya Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na ya
taasisi. Hivi sasa Tume inaandaa mapendekezo ya Rasimu ya Pili ya
Katiba itakayopelekwa kwenye Bunge Maalum. Baada ya tafakuri zake,
Bunge Maalum litatoa rasimu ya mwisho ya Katiba ambayo itapelekwa kwa
wananchi kwa ajili ya uamuzi wa mwisho kupitia kura ya maoni. Baada ya
hatua hiyo, ndipo tutakapokuwa tumepata Katiba Mpya.
Ndugu Wananchi;
Baada ya Bunge la Novemba, 2011 kupitisha Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba, kulikuwepo na madai ya kutaka sheria hiyo iboreshwe kutoka vyama
vyote vya siasa vikiwemo vyama vya upinzani na Chama tawala.
Majadiliano yalifanyika baina ya Serikali na vyama hivyo pamoja na
shirikisho la asasi za kiraia. Makubaliano yalifikiwa kuwa marekebisho
yafanyike kwa awamu. Awamu ya kwanza ihusishe Tume ya Mabadiliko ya
Katiba kisha hapo yafanyike marekebisho yanayohusu Bunge Maalum na
mwisho Kura ya Maoni.
Kama ilivyokuwa kwa mabadiliko yaliyohusu Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, safari hii nayo vyama vya siasa vilitoa mapendekezo yao.
Yalifanyika mazungumzo kati yao na Serikali na maelewano kufikiwa kuhusu
maeneo ya kufanyiwa marekebisho. Serikali ilitayarisha rasimu ya
Muswada na kuuwasilisha kwa wenzetu wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar.
Ndugu Wananchi;
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilitoa mapendekezo yake na ushauri
kwenye maeneo mawili. Kwanza kwamba uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum
ufanywe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na
kuafikiana na Rais wa Zanzibar. Pili walishauri kwamba kama Bunge
Maalum litashindwa kufikia maamuzi ndani ya siku 70 zilizopendekezwa,
liweze kuongezwa muda hadi kufikia siku 90. Maeneo mengine ya Muswada
waliafikiana nayo.
Ndugu Wananchi;
Kwa kuzingatia utaratibu wa kutunga Sheria, Serikali ilifikisha
Muswada kwa Spika wa Bunge ambaye nae aliuwasilisha kwenye Kamati ya
Kudumu ya Katiba, Sheria na Utawala. Kama ilivyo ada, Kamati hiyo
ilifanya vikao na wadau na kupokea maoni yao kuhusu Muswada. Nimeambiwa
kulikuwa na mjadala wa kina na mapendekezo mazuri yalitolewa na wadau.
Kisha hapo Wajumbe wa Kamati walikaa wenyewe kujadili Muswada
walikuwepo pia Wabunge ambao si Wajumbe wa Kamati walioshiriki kwa vile
Kanuni zinaruhusu. Nimeambiwa pia kwamba mjadala ulikuwa mpana na wa
kina zaidi. Mapendekezo kadhaa yalitolewa na Wajumbe kuhusu vifungu
mbalimbali vya Muswada.
Ndugu Wananchi;
Nimefahamishwa kuwa Wabunge wa vyama vyote walichangia na kwamba
baadhi ya nyakati mambo yalipokuwa ugumu mawazo mazuri ya baadhi ya
Wabunge wa upinzani yalisaidia kupata ufumbuzi. Nimeambiwa pia kwamba
Wajumbe wa Kamati na upande wa Serikali walikubaliana kwa maeneo mengi
isipokuwa machache ambayo walikubaliana kwa pamoja wayapeleke Bungeni
ili Wabunge nao wayajadili na kuyapatia ufumbuzi.
Ndugu Wananchi;
Baada ya Kamati kumaliza kazi yake, Waziri wa Katiba na Sheria,
Mheshimiwa Mathias Chikawe aliwasilisha Muswada Bungeni. Akafuatiwa na
Mheshimiwa Gosbert Blandes kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, kutoa maoni ya Kamati. Baadaye
Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Mheshimiwa Tundu Lissu alitoa maoni
yake.
Ndugu Zangu;
Baada ya watu hao watatu kutoa maoni yao ilitarajiwa kuwa Wabunge
wangeanza kujadili Muswada. Naambiwa mambo hayakuwa hivyo. Badala yake
kukazuka malumbano baina ya Spika na baadhi ya Wabunge wa Upinzani
wakitaka Muswada usijadiliwe. Ilifikia wakati hoja hiyo ikabidi
iamuliwe kwa kura ambapo ilishindwa. Katika hali isiyotarajiwa, Wabunge
wote wa upinzani wakatoka nje ya Bunge isipokuwa wawili. Kitendo hicho
kimewanyima Wabunge wengi wa upinzani fursa ya kutetea hoja zao
walizozitoa kupitia hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani. Pia
wamejinyima nafasi ya kusema mambo mengine wakati wa mjadala na Kamati
ya Bunge zima.
Wabunge waliokuwepo waliendelea kuujadili Muswada na kutoa hoja na
mapendekezo ya kuuboresha. Walifanya hivyo wakati wa mjadala na wakati
wa kupitia kifungu kwa kifungu. Baadhi ya hoja na mapendekezo
yalikubaliwa na mengine yalikataliwa. Miongoni mwa yaliyokubaliwa na
Wabunge, kwa mfano, ni kuhusu elimu ya mtu atakayekuwa Mwenyekiti wa
Bunge Maalum na lile la ukomo wa uhai wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Ndugu Wananchi;
Kwa maoni yangu madai ya Kambi ya Upinzani yanazungumzika na hata
baadhi yangeweza kukubalika kama Wabunge wake wangekuwepo Bungeni na
kushiriki mchakato wote wa kujadili na kupitisha Miswada Bungeni.
Bahati mbaya hawakuwepo, hivyo hapakuwepo na mtu wa kusema mawazo yao.
Baada ya kupoteza fursa yao halali, kutaka kupata ufumbuzi nje ya Bunge
ni jambo lisilowezekana. Haya ni masuala yanayohusu Bunge ambayo
hujadiliwa na kuamuliwa Bungeni na si vinginevyo. Kuandamana nchi nzima
au kuchukua hatua za kutotii sheria kama Mwenyekiti wa CHADEMA,
Mheshimiwa Freeman Mbowe anavyotaka, hakutaleta mabadiliko wanayoyataka
katika sheria hii. Naamini na wao wanautambua ukweli huo.
Ndugu Wananchi;
Kuna msemo wa wahenga kuwa “historia hujirudia”. Naomba hekima
ziwaongoze viongozi wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi na zituongoze sote
kutumia utaratibu tulioutumia mwaka 2012. Kulipotokea mazingira kama
haya pande zote zilikaa pamoja na kuzungumzia hoja moja baada ya
nyingine na kukubaliana nini kifanyike na kifanyike vipi. Baada ya
kuridhiana hatua zipasazo za kisheria na kanuni zilichukuliwa na
kumaliza mzozo.
Ndugu Wananchi;
Kufanya kinyume cha hayo hakutaleta ufumbuzi wa mzozo huu.
Tutaliingiza taifa kwenye matatizo yasiyokuwa ya lazima. Tukikataa
kufanya hayo Watanzania wanayo kila sababu ya kuhoji dhamira zetu na
kutilia shaka nia zetu. Watakuwa na haki ya kuuliza nia ni hii yetu
sote ya kupata Katiba Mpya kwa kutumia njia za kikatiba na kisheria au
tuna dhamira nyingine iliyojifisha?
Kama dhamira yetu ni kutaka kupata Katiba mpya kwa mujibu wa Katiba
na Sheria, ushauri wangu na rai kwa ndugu zetu wa CHADEMA, CUF na
NCCR-Maguezi ni kuwa waachane na mipango ya maandamano na kufanya
ghasia. Badala yake watumie njia halali zinazotambulika kikatiba na
kisheria kujenga hoja za kufanya marekebisho wanayoyaona wao yanafaa
kuboresha Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Tukifanya hivyo tutakuwa tunajenga badala ya kubomoa. Tutaliponya
taifa. Sisi katika Serikali tuko tayari.
Ndugu Wananchi;
Napenda pia kuzisemea baadhi ya hoja zilizotolewa na Kambi ya
Upinzani. Kwanza kabisa nasema kuwa nimesikitishwa sana na madai na
tuhuma za uongo eti katika uteuzi wa Tume ya Katiba sikuheshimu
mapendekezo ya TEC, CCT na walemavu.
Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
Siyo tu kauli hiyo ya Mheshimiwa Tundu Lissu ni uzushi na uongo mtupu
bali pia ni ya unafiki, fitina na uzandiki wa hali ya juu. Nasema
hivyo kwa sababu, sipendi kuamini kuwa Mheshimiwa Mbunge amesema yale
kwa kutokufahamu ukweli au kwa bahati mbaya. Amesema yale kwa makusudi
mazima ya kupotosha ukweli ili pengine isaidie kujenga hoja yake ya
kutaka Rais asiteue wale Wajumbe 166 wa Bunge Maalum.
Napenda ieleweke kuwa siishabikii kazi hiyo, lakini kwa kutimiza
wajibu na maslahi ya taifa nikiagizwa na Sheria za nchi nitafanya.
Nasema hivyo kwa sababu nafahamu ni kazi ngumu. Kama kazi ya uteuzi wa
Wajumbe 30 wa Tume haikuwa rahisi hata kidogo, hii ya uteuzi wa watu 166
itakuwa ngumu zaidi. Ile ya Tume ilikuwa ngumu kwa namna mbili.
Kwanza, kwamba taasisi zilizoomba na waombaji walikuwa wengi mno kuliko
nafasi za kujaza yaani 15 Zanzibar na 15 Bara. Zanzibar ziliomba
taasisi zaidi ya 60 na waombaji walikuwa zaidi ya 200 wakati Bara
kulikuwa na taasisi zaidi ya 170 zikiwa na waombaji zaidi ya 500.
Kupata watu 30 kutoka orodha kubwa kiasi hicho si mtihani mdogo. Pili
kwamba tulitakiwa kuunda Tume inayoasili sura ya taifa, yaani watu wa
nchi yetu kwa maeneo, vyama vya siasa, dini, wanawake, vijana, walemavu,
wafanyakazi, wasomi, Wabunge, Wawakilishi, wanasheria, wafanyabiashara,
wakulima, asasi za kiraia n.k.
Ndugu Wananchi;
Pamoja na changamoto hizo, lakini tulifanikiwa kuunda Tume
iliyopokelewa vizuri na jamii na kufanya watu wengi hata wale ambao
hawakuteuliwa wahisi kuwakilishwa. Tulifanyaje? Kwanza kabisa
tulihakikisha kuwa tunapata wawakilishi wa vyama vya siasa vyenye
wawakilishi Bungeni na kwenye Baraza la Wawakilishi na tunapata
wawakilishi wa mashirika ya dini zetu kubwa yaani, TEC, CCT na
BAKWATA. Ndiyo maana nikasema kuwa kwa Mheshimiwa Tundu Lisu kudai
kuwa mapendekezo ya TEC na CCT hayakuheshimiwa ni uongo wa mchana
usiokuwa na kichwa wala miguu.
Baada ya hapo ndipo tukaangalia waombaji wa makundi na taasisi
nyingine. Tulijitahidi sana kupata watu ambao wanawakilisha kundi
zaidi ya moja. Tulifikiria hivyo kwa sababu ni ukweli ulio wazi kuwa si
kila taasisi iliyoomba itapata mwakilishi kwani hata tungependa iwe
hivyo nafasi hazikuwepo. Kwa kutumia utaratibu huu makundi mengi
yamepata uwakilishi kutokana na watu waliopendekezwa na makundi mengi.
Tumefanya kazi kubwa sana ya kuwianisha mambo na makundi ya maslahi
mbalimbali nchini.
Ndiyo maana naiona mantiki ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
akishirikiana na Rais wa Zanzibar wa kuwateua Wajumbe wa Bunge Maalum.
Dhana kuwa kila kikundi kiteue chenyewe watu ingefaa sana kama
kungekuwepo na nafasi za kutosha kila kundi nchini. Hilo haliwezekani,
labda tuwe na Bunge Maalum lisilokuwa na ukomo wa wajumbe.
Ndugu Wananchi;
Mimi na Rais wa Zanzibar tumekuwa tunajiuliza baada ya kazi ngumu na
nzuri tuliyoifanya na iliyopongezwa na wengi ya kuteua Tume ya
Mabadiliko ya Katiba nini kilichoharibika sasa hata tuonekane
hatuaminiki kuteua hawa 166? Kama ni kwa sababu za Mheshimiwa Tundu
Lissu, nimeshasema hazina ukweli wowote. Ninapojiuliza kwa nini aseme
uongo nashindwa kupata jibu linaloingia akilini. Wakati mwingine
nafikiria kuwa ni hiana. Lakini nadhani ni hila za kisiasa zenye nia ya
kutaka kupata watu wa kutetea maslahi ya chama chake. Kama hiyo ndiyo
shabaha basi amekosea sana.
Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
Hatutengenezi Katiba ya Chama fulani bali Katiba ya nchi, Katiba ya
watu wa vyama vyote na wasiokuwa na vyama ambao ndiyo wengi kuliko
wote. Lazima tuongozwe na ukweli huo na tuwe na msimamo huo wakati
wote. Lazima tukumbuke kuwa si watu wote wanaostahili au kuwa na sifa
ambao wataomba na kupata nafasi ya kuwa Wajumbe, hivyo wale wachache
watakao bahatika lazima wawasemee wote. Wanatakiwa kusikiliza na
kuwakilisha mawazo ya wote hata wale wasiokuwa wa Chama chao au kundi
lao.
Ndugu Wananchi;
Bahati nzuri hii ndiyo sifa kubwa iliyooneshwa na Wajumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba. Wamewasimamia na kuwasemea watu wote bila ya
kubagua. Natambua kuwepo kwa baadhi ya watu ambao hawafurahii msimamo
huo na matokeo ya kazi yao. Watu hao kuwalaumu Wajumbe wa Tume kwa
ajili hiyo ni kuwaonea na kutowatendea haki. Tunataka watakaokuwa
Wajumbe wa Bunge Maalum nao waige mfano huu mzuri. Wajali maslahi
mapana ya taifa letu na watu wake badala ya kujali yale ya taasisi zao
au makundi yao.
Zanzibar Kutokushirikishwa
Ndugu Wanachi;
Nimeambiwa pia kuliwepo madai ya Zanzibar kutokushirikishwa
ipasavyo. Nimeeleza kwa kiasi gani Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
imeshirikishwa na kutoa maoni yake yaliyojumuishwa katika Muswada.
Hivyo basi napata tabu kuyaelewa madai kwamba Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar haikushirikishwa msingi wake nini! Labda kuna kitu
sikuambiwa!
Nimeulizia kuhusu hoja ya Kamati kutokufanya vikao Zanzibar
kusikiliza maoni ya wadau wa Zanzibar. Nimeambiwa kuwa Kanuni za Bunge
hazina sharti hilo hivyo Kamati haistahili kulaumiwa. Kama hivyo,
nashauri kuwa suala hili lirudishwe Bungeni ili Wabunge walizungumze na
kulifanyia uamuzi muafaka. Vinginevyo watu wataendelea kulauminiana
isivyostahili. Hivyo basi, kuligeuza jambo hili kuwa ni suala la
kukataa Muswada au kususia vikao vya Bunge au kufanya maandamano sidhani
kama ni sawa.
Ndugu Wananchi;
Nimeambiwa pia kuwa kulikuwa na hoja ya kutaka idadi ya Wajumbe wa
kutoka Tanzania Bara na Zanzibar iwe sawa kama ilivyo kwenye Tume ya
Mabadiliko ya Katiba. Sababu ya idadi ya Wajumbe wa Tume kuwa sawa
inatokana na utaratibu wao wa kufikia uamuzi. Ni kwa maelewano ya wote
(consensus) na siyo kwa kupiga kura. Ndiyo maana idadi imewekwa sawa
ili sauti za pande zote zisikike sawia. Bunge Maalum lina sharti la
kufanya uamuzi kwa theluthi mbili ya kura za kila upande kukubali. Bila
ya hivyo hakuna uamuzi.
Hivyo basi, katika Bunge Maalum nguvu si uwingi wa kura ambazo upande
fulani unaweza kupata bali ni ulinganifu sawa wa kura za kila upande
peke yake. Huu ndiyo msingi unaotumika katika Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania hivi sasa kwa lengo la kulinda maslahi ya
Zanzibar. Zanzibar ina Majimbo 50 ya uchaguzi na Tanzania Bara ina
Majimbo 189, hivyo ukiamua kwa wingi kila wakati Wazanzibari
watashindwa. Lakini, hapajakuwepo madai ya Zanzibar nao kutaka kuwa na
idadi sawa ya majimbo kama Bara au kupunguza majimbo ya Bara yawe sawa
na ya Zanzibar kwa sababu wingi si hoja. Msingi unaotumika ni kutoa
nguvu sawa za uamuzi kwa kila upande wa Muungano wakati wa kuamua
masuala ya Katiba. Hakuna mdogo wala mkubwa, wote wako sawa. Hakuna
mdogo kumezwa na mkubwa. Ndiyo msingi unaopendekezwa kutumika kwenye
Bunge Maalum hivyo hakuna kitakachoharibika kwa idadi ya Wajumbe
kutokukulingana. Nadhani inafaa ibaki ilivyo. Lakini kama Wabunge
wataamua waongeze idadi itakuwa kwa sababu nyingine siyo hii ya mfano wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Ndugu Wananchi;
Katika orodha ya madai ya ndugu zetu wa upinzani lipo suala la uhai
wa Tume ya Katiba. Wanataka usiishe wanapokabidhi rasimu ya pili kwa
Bunge Maalum bali waendelee kuwepo mpaka mwisho wa mchakato. Nimeulizia
ilikuwaje? Nimeelezwa kuwa jambo hili halitokani na mapendekezo ya
Serikali wala ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala.
Limetokana na pendekezo la Mbunge katika Bunge wakati wa kupitia vifungu
na kuungwa mkono na Wabunge wengi. Kwa hiyo kuilaumu Serikali si
haki. Serikali inaweza kuwa mshirika katika hoja hii.
Nami naiona hoja ya Wajumbe wa Tume kuwa na wajibu wakati wa Bunge
Maalum hasa wa kusaidia kufafanua mapendekezo ya Tume. Je ushiriki huo
uwe vipi? Je ni Wajumbe wote au baadhi yao ni jambo linaloweza
kujadiliwa.
Ndugu Wananchi;
Naomba nimalizie kwa kuwasihi viongozi wa CHADEMA, CUF na
NCCR-Mageuzi kuongozwa na hekima iliyotumika wakati tulipokuwa na tatizo
linalofana na hili kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Mimi naamini
kama iliwezekana kufanikisha mambo wakati ule inaweza kufanya hivyo hata
safari hii. Itatufikisha pale tunapopataka salama salimini bila
maandamano, kushupaliana au uvunjifu wa amani. Kupanga ni kuchagua,
naomba sote, mmoja mmoja na kwa umoja wetu tuchague njia ya mazungumzo
na maelewano kwani itaihakikishia nchi yetu amani, usalama na utulivu.
Tukifanya hivyo historia itatuhukumu kwa wema.
Mungu Ibariki Tanzania.
Nawashukuru sana kwa kunisikiliza.