LATEST POSTS

Wednesday, February 12, 2014

Mama na mwanae wauawa kikatili - Shinyanga

MAUAJI ya kikatili dhidi ya wanawake wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga yamezidi kupamba moto kufuatia tukio la kuuawa mama na mwanaye walioshambuliwa kwa kukatwakatwa mapanga huko katika Kijiji cha Ngokolo Kata ya Bukomela usiku wa kuamkia juzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangala aliwataja wanawake waliouawa kuwa ni Mhulu Nh'ambo (50) na mwanaye Helena Charles (30), walioshambuliwa kwa kukatwakatwa mapanga na watu wasiojulikana mnamo saa moja usiku walipokuwa wakiandaa chakula cha usiku nyumbani kwao.
Kamanda Mangala alisema, siku hiyo ya tukio wakati mama huyo akiwa na mwanaye wakiandaa chakula cha usiku ghafla walivamiwa na kundi la watu wasiojulikana ambao waliwashambulia kwa kuwakatakata mapanga sehemu za kichwani na mgongoni hali iliyosababisha wapoteze maisha papo hapo kutokana na kuvuja damu nyingi.
Hata hivyo, alisema chanzo cha mauaji hayo mpaka sasa hakijafahamika na tayari polisi inamshikilia mtuhumiwa mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi na juhudi za kuwasaka watuhumiwa wengine zinaendelea ili waweze kukamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu shtaka la mauaji.
Kamanda Mangala ametoa wito kwa raia wema kutoa taarifa katika kituo chochote cha polisi ama ofisi za watendaji wa vijiji na kata pale watakapomuona mtu au watu wanaowatilia shaka ili waweze kukamatwa na kuchunguzwa iwapo walihusika na mauaji hayo.
Hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya alikiri kuwepo na wimbi kubwa la mauaji dhidi ya wanawake na kusema mauaji yanayofanyika hivi sasa ni tofauti na yale ya awali ambapo waliokuwa wakiuawa ni wanawake vikongwe wenye umri wa kuanzia miaka 60.
Alisema, hivi sasa takwimu zinaonesha wanawake wanaouawa ni pamoja na wale wenye umri wa kati ya miaka 50 hadi 20 ikiwemo wanaochinjwa na waume au wenzi wao wa kiume kutokana na kinachodaiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.
Mpesya aliyekuwa akihojiwa na mwandishi wa habari aliyekuwa akifanya utafiti wa vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo mauaji ya vikongwe katika wilaya hiyo ulioandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake nchini (TAMWA) alisema, takwimu zinaonesha hivi sasa ndani ya mwezi mmoja hutokea mauaji ya wanawake wasiopungua watatu.
Alisema, ugomvi wa kuwania mali ikiwemo mirathi na masuala ya kugombea ardhi ni moja ya chanzo cha mauaji hayo ambapo hata hivyo katika kipindi cha Novemba, mwaka jana wanawake watatu waliouawa kwa kuchinjwa akiwemo mwanafunzi wa kidato cha nne chanzo kilikuwa ni wivu wa kimapenzi.

0 comments: