LATEST POSTS

Monday, March 3, 2014

Majambazi waua wenzao

WATU wawili wanaosadikiwa kuwa majambazi, wamefariki dunia wakiwa njiani kupelekwa Hospitali ya Wilaya ya Tarime, mkoani Mara ili kupatiwa matibabu baada ya kujeruhiwa na risasi walizopigwa na wenzao.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya, Justus Kamugisha, alisema tukio hilo limetokea juzi saa 2:40 asubuhi, katika Kitongoji cha Kokemange, Kijiji cha Nyamwaga, wilayani Tarime.
Alisema watu hao walipigwa risasi na majambazi wenzao wakiwa njiani kuwapeleka polisi eneo wenzao walijificha na silaha walizokuwa wakizitumia kufanya uhalifu.
Aliwataja waliokufa kuwa ni Wambura Sagare Orondo (26), mkazi wa Kitongoji cha Nyaichirichiri, Kijiji cha Kitawasi ambaye alijeruhiwa vibaya tumboni na Shabani Nyang'era 45, mkazi wa Kijiji cha Borenga, Wilaya ya Serengeti, aliyejeruhiwa kifuani.
"Katika tukio hili, polisi walijibu shambulio la risasi hivyo majambazi waliojificha walifanikiwa kutoroka na kutelekeza bunduki moja aina ya G3 ambayo namba zake zimefutwa na imekatwa kitako pamoja na risasi tano katika magazini.
"Hawa majambazi waliofariki, walikuwa wakitafutwa muda mrefu kwa tuhuma za unyang'anyi wa kutumia silaha, mauaji na wizi wa mifugo," alisema Kamanda Kamugisha.
Aliongeza kuwa, chanzo cha tukio hilo ni baada ya majambazi kutoka nchi jirani ya Kenya, kubaini wanafuatiliwa na kuamua kujihami kwa kufyatua risasi.
Aliwaomba wananchi waendelee kutoa taarifa kwa jeshi hilo ili watuhumiwa wa unyang'anyi na mauaji waweze kukamatwana kufikishwa katika vyombo vya sheria.

0 comments: