LATEST POSTS

Wednesday, July 16, 2014

Gharama kubwa alikozikwa Ballali

  
Kaburi la aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Daudi Ballali lililopo katika makaburi ya Gate of Heaven nchini Marekani. Gharama ya kumzika mtu katika eneo hilo ni Sh7.9 milioni. Picha na Neville Meena  
Eneo alilozikwa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Daudi Ballali katika makaburi ya Gate of Heaven, Maryland nchini Marekani liliigharimu familia yake kiasi cha Dola 4,810 za Kimarekani (sawa na zaidi ya Sh8 milioni).
Ballali aliyefariki dunia Mei 16, 2008 nyumbani kwake Washington DC, alizikwa katika eneo namba 6, ploti ya 241, safu namba 17 katika makaburi hayo yaliyopo katika anwani ya 13801, Georgia Avenue Silva Spring, MD 20906.
Safu hiyo namba 17 aliyozikwa Ballali imepewa jina la Jesus in the Temple, ikimaanisha ‘Yesu Hekaluni’.
Gavana huyo wa zamani aliondoka nchini kwenda Marekani kikazi, akiacha mjadala mkubwa juu ya wizi wa fedha kutoka kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (Epa), huku jina lake likitajwa kuwa alihusika kuidhinisha fedha hizo kwa makampuni 22 kinyume cha taratibu.
Aliachishwa kazi baada ya ukaguzi wa kampuni ya Ernst and Young kubaini ufisadi mkubwa kwenye taasisi hiyo kuu ya fedha nchini. Muda mfupi baadaye Ballali alifariki, kifo ambacho kilizua mjadala kutokana na mazingira yake.
Kwa mujibu wa ramani, ambayo gazeti hili liliipata kutoka ofisi iliyopo kwenye makaburi hayo, aina ya kaburi la Balalli inaangukia katika eneo yalipo makaburi yenye mnara ambayo yanagharimu kiasi hicho cha fedha.
Pia aina hiyo ya eneo inaruhusu kuwapo kwa makaburi pacha iwapo mmiliki wa eneo husika atahitaji, lakini kwa gharama ambazo ni maradufu. Hata hivyo haikufahamika mara moja iwapo familia ya Ballali imechukua sehemu ya pili.
Idadi kubwa ya Wamarekani wanamiliki maeneo ambayo tayari wameyaandaa kwa ajili ya maziko baada ya kufariki dunia na maeneo hayo hulipiwa ada kila mwaka kwa gharama ambayo huzingatia matunzo na eneo yalipo makaburi hayo.
Mtanzania Safari Ohumai ambaye ni mkazi wa Greenbelt, nje kidogo ya Washington aliiambia Mwananchi nyumbani kwake kuwa: “Kufa hapa Marekani ni gharama kubwa. Lazima ulipie eneo ambalo umeliandaa kwa ajili ya maziko yako utakapofariki dunia”.
Taratibu za mazishi
Mazishi ya Ballali yalikuwa ya faragha kwani mwili wake haukuonyeshwa hadharani, hivyo Watanzania wengi wanaoishi katika miji ya Washington DC, Maryland na Virginia (DMV), hawakuweza kushiriki.
Familia ya Gavana iliyopo Marekani na Tanzania, kwa nyakati tofauti ilimwambia mwanandishi wa Mwananchi kwamba usiri wa taratibu za mazishi, ulikuwa ni utekelezaji wa matakwa ya Ballali ambaye kabla ya kifo chake aliagiza maiti yake isionyeshwe hadharani isipokuwa kwa ndugu wa karibu pekee.
Baadhi ya Watanzania ambao wameishi katika miji hiyo kwa miaka kati ya 15 na 20, walionekana ama kutomfahamu kabisa Ballali au kutofahamu alikokuwa akiishi, kifo na mazishi yake, tofauti na hapa nchini.
Ballali alifariki dunia akiwa nyumbani kwake Washington DC, Mei 16, 2008 baada ya kuugua kwa miezi kumi na baadaye kuzikwa Mei 23, tukio lililowahusisha ndugu wa karibu.
Usiri uliogubika kifo na mchakato wa mazishi yake ndiyo chachu ya kuwapo kwa hisia kwamba kiongozi huyo hakufa, bali alifichwa sehemu mojawapo ya Marekani kutokana na kile kinachodaiwa kwamba alikuwa na siri nyingi kuhusu kashfa ya fedha zilizochotwa kwenye Akaunti ya Epa.
Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika (Voa), Mwamoyo Hamza alisema: “Siyo rahisi kwa wana DMV wengi wa sasa kumfahamu Ballali, kwa sababu mbalimbali, lakini kubwa ni kwamba yeye alifika hapa (Marekani) siku nyingi sana.”
“Kwa mfano huu umoja wa sasa wa Watanzania wanaoishi DMV, Ballali hakuwa mwanachama, kwa hiyo naweza kusema alifahamika zaidi kwa wenzake wenye umri sawa na yeye waliokwenda Marekani miaka ya 60,” alisema Mwamoyo.
Kuhusu uamuzi huo, Mwamoyo alisema nchini Marekani msiba ni suala linalohusu familia zaidi na kwamba haikuwa ajabu kama familia ya Ballali iliamua kuomboleza kifamilia.
“Hapa ndiyo utamaduni wao, mazishi au masuala ya misiba huwa ni ya kifamilia kwa hiyo haikuwa ajabu kwa familia ya Ballali kufanya taratibu zao kwa jinsi walivyoona inafaa,” alisema Mwamoyo ambaye pia alibainisha kuwa Voa walifuatilia taarifa za kifo chake na walizitangaza katika taarifa zao.
Watanzania wengine
Mtanzania Harriet Shangarai anayeishi Maryland kwa zaidi ya miaka kumi sasa, alisema hamfahamu Ballali na wala hajawahi kusikia taarifa zake. “Huyo ndiyo nani? Mie simfahamu kwa kweli,”alisema Harriett alipozungumza na Mwananchi, eneo la Silver Spring.
Mtanzania mwigine, Abou Shatri, ambaye pia ni mkazi wa Maryland ambaye pamoja na kusihi nchini Marekani takriban miaka 20, hakuwahi kusikia taarifa zozote zinazomuhusu Ballali na wala hamfahamu.
“Ndugu yangu nisikudanganye, huyo mtu mimi simfahamu kabisa kwani huyo ndo nani?” alihoji Shatri na alipoelezwa kwamba alikuwa Gavana wa BoT ambaye pia aliishi Maryland na baadaye Washington, alisema hamfahamu kabisa.
Mbelwa Bandiwo, ambaye pia ni mkazi wa eneo la DMV, alisema anamfahamu Ballali lakini hakufuatilia msiba wake kwa sababu mazishi yalikuwa ni ya kifamilia.
“Hilo ni jambo la kawaida hapa Marekani. Mara nyingi mazishi ama shughuli za misiba huwa ni ya kifamilia zaidi na marafiki wa karibu. Kwa hiyo ndiyo maana Watanzania wengi wa maeneo haya watakwambia kwamba hawakushiriki kwenye huo msiba,” alisema Bandiwo.
“Lakini jambo jingine ni kwamba huu ni utamaduni tuliouzoea kwa hiyo ni jambo la kawaida kwamba katika familia nyingine hata makaburini huwa hawaendi kabisa kuzika, badala yake kazi hiyo hufanywa na kampuni zilizosajiliwa kwa ajili hiyo na baadaye labda Jumamosi au Jumapili ndipo familia huenda kuona mahali alipozikwa ndugu yao na kuweka maua”.

Itaendelea.....

Chanzo: Mwananchi

0 comments: