Askari wa Kikosi cha FFU, Mohamed Mjombo (Namba E 5607) ameuawa
kwa kupigwa risasi, huku mwingine akijeruhiwa baada ya majambazi kuvamia
hoteli ya kitalii ya Pongwe Bay iliyo Pongwe mkoani Kusini Unguja.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kamishna wa
Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame alisema tukio hilo lilitokea juzi
saa 3:00 usiku wakati wageni wakiwa wamepumzika na askari hao wa FFU
kutoka Kituo cha Polisi Machui wakiwa katika lindo kwenye hoteli hiyo.
Kamishna Hamdan alisema muda huo lilifika gari
moja na baada ya kuegeshwa watu watatu waliteremka na kumvamia askari
mwenye Namba F 6198, Ibrahim Juma Mohamed na kujaribu kumnyang’anya
silaha aina ya SMG na katika purukushani hiyo walimpiga risasi ya
begani.
Alisema askari huyo anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Mnazi Mmoja.
“Majambazi walifanikiwa kumpora bunduki aina ya
SMG na kisha kumpiga risasi na kumjeruhi begani. Tuko katika msako
mkubwa hivi sasa,” alisema Kamishna huyo wa Polisi Zanzibar.
Hata hivyo, alisema wakati Mjombo akisonga mbele
kujaribu kumsaidia mwenzake, alifyatua risasi lakini ikakwama katika
chemba na majambazi hao kufanikiwa kumpiga risasi sehemu ya ubavu na
kutoroka.
Alisema askari huyo wa FFU alifariki majira ya saa
7:00 usiku katika Hospitali ya Mnazi Mmoja na kuzikwa jana huko Bambi
Mkoa wa Kaskaszini Unguja. Watu wawili wanashikiliwa na polisi kuhusiana
na tukio hilo na wengine wanaendelea kusakwa.
“Tayari tumepeleka kikosi cha askari maalumu
kutoka Mkoa wa Mjini Magharibi na Mkoa wa Kusini Unguja, ili kuhakikisha
usalama unaimarishwa katika maeneo ya ukanda wa utalii,” alieleza
Kamishna Hamdan.
Daktari bingwa wa Hospitali ya Mnazi Mmoja,
Msafiri Marijani ambaye ndiye aliyemfanyia uchunguzi Mjombo, alisema
askari huyo alipoteza damu nyingi baada ya kupigwa risasi ubavu wa
kushoto na kutokea paja la kulia na ndio maana alipoteza maisha.
“Uti wa mgongo pia ulivunjika,” alisema Dk.
Marijani. “Amepoteza damu nyingi iliyokuwa ikivuja ndani ya tumbo na
nje. Risasi bado haijapatikana mahali ilipo mwilini.”
Akizungumzia tukio hilo, mwenyekiti wa Jumuiya ya
Uwekezaji Katika Sekta ya Utalii Zanzibar (ZAT), Abdulswamad Said
alisema wakati umefika kwa SMZ kuimarisha ulinzi katika Ukanda wa Utalii
kwa vikosi vya SMZ na Polisi kufanya kazi pamoja ili kulinda
wawekezaji, watalii na wananchi.
Abdulswamad alisema uongozi wa ZAT uliwahi
kukutana na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na kuomba vikosi vya
SMZ viongezewe nguvu za ulinzi ili kukabiliana na matukio ya uhalifu na
kusema jambo la kushangaza pamoja na Rais kutoa agizo hilo, hakujawa na
utekelezaji wa wazi.
“Matukio ya watu kumwagiwa tindikali, milipuko ya mabomu na
uhalifu wa kutumia silaha hayatoi sura nzuri kwa maendeleo ya utalii
Zanzibar. Juhudi zaidi zinahitajika kukabiliana na vitendo hivyo
hatari,” alisema mwenyekiti huyo wa ZAT.
Taarifa kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa
majambazi hao walikuwa wamebeba silaha za kivita na kuaminika huenda
walikuwa na silaha aina ya AK 47, lakini hawakufanikiwa kupora mali
hotelini hapo.
0 comments:
Post a Comment