LATEST POSTS

Monday, December 2, 2013

HAKIMU WA WILAYA ALIYESIMAMISHWA AKUTWA NA MAJALADA THELATHINI NYUMBANI KWAKE

ALIYEKUWA Hakimu Mkazi  wa Mahakama ya wilaya ya Urambo Mkoani Tabora Oscar Bulugu,  anayekabiliwa na tuhuma tatu za kuomba na kupokea Rushwa amejikuta matatani baada ya kukutwa akiwa na majalada ya Kesi zaidi ya Thelathini nyumbani kwake.
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoani Tabora, Fidelis Kalungura, imeeleza kuwa Hakimu huyo alipekuliwa na Maafisa wa TAKUKURU na kukutwa na majalada yapatayo Thelathini na Moja ya kesi mbali mbali.
Kalungura aliongeza kuwa  TAKUKURU ilichukua jukumu la kufanya upekuzi nyumbani kwa Hakimu Bulugu baada ya wananchi kupeleka malalamiko ya mara kwa mara wakidai kutotendewa haki na Mahakama ya Wilaya ya Urambo.
Katika malalamiko yao wananchi wamekuwa wakidai kuwa wanapofika Mahakama ya Wilaya ya Urambo wanakosa huduma kwa  kuwa majalada ya kesi zao hayaonekani kwa makarani kwa vile  yapo kwa  Hakimu aliyesimamishwa.
Kufuatia malalamiko hayo  TAKUKURU iliamua kufanya uchunguzi  wa kina na baada ya kujiridhisha walienda kupekua nyumbani kwa Hakimu huyo na kukuta akiwa na majalada hayo
Mwezi Aprili mwaka huu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa,(TAKUKURU),Mkoani hapa ilimkamata na  kumfikisha Mahakamani Hakimu mkazi mfawidhi huyo,Oscar Bulugu kwa tuhuma tatu za kuomba na kupokea rushwa ya shilingi milioni tano.
Hakimu  Bulugu Katika kesi yake inayomkabili  anatuhumiwa kuwa alitenda makosa hayo kati ya Mwezi Machi 15 mwaka huu  hadi Machi 22 huko wilaya ya Urambo akiwa ni Hakimu Mkazi Mfawidhi.
Katika kesi hiyo upande wa mashitaka ulidai kuwa Machi 15 mwaka huu mtuhumia akiwa ni Hakimu wa  wilaya ya Urambo alimshawishi Lucas Raymond Changala ampe fedha hizo ili kumpa dhamana ndugu yake aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya wizi wa fedha za benki ya NMB.

Mwanasheria wa TAKUKURU katika shauri hilo,  Simon Mashindia,  alidai katika shtaka la pili kuwa tarehe 18 Machi Mwaka huu hakimu huyo ambaye ni mtuhumiwa alipokea shilingi milioni moja toka kwa Changala kama malipo ya awali ili aweze kumpa dhamana Phillipo Raymond aliyekuwa mtumishi wa benki ya NMB tawi la Urambo anayetuhumiwa kuiba zaidi ya shilingi milioni mia moja.

Mwanasheria huyo wa TAKUKURU alidai katika shitaka la tatu kuwa tarehe 21/03/2013  mtuhumiwa huyo alipokea tena shilingi milioni moja ikiwa ni endelezo la malipo aliyoomba aweze kumpa dhamana mtumishi huyo wa NMB tawi la Urambo.
CHANZO: TABORA YETU

0 comments: