HALMASHAURI ya Wilaya mpya ya Kaliua mkoani Tabora,
imetoa onyo kali kwa watumishi wote wa halmashauri hiyo kutokuthubutu
kujihusisha na vitendo vya kifisadi katika fedha za miradi ya maendeleo.
Onyo hilo limetolewa juzi na Makamu Mwenyekiti wa
halmashauri hiyo, Mhe. Ibrahim Kifoka, alisema hayo
alipokuwa katika kikao cha waandishi wa habari muda mfupi baada ya madiwani wa
halmashauri hiyo kumaliza ziara ya siku moja jijini Mwanza.
Alisema siku zote vitendo vya kifisadi vimekuwa
vikirudisha nyuma maendeleo ya wananchi, hivyo uongozi wa halmashauri hiyo
utawachukulia hatua kali watumishi wote watakaobainika kujihusisha na hujuma
hizo.
Kifoka ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Silambo, alisema
jitihada zilizopo sasa ni kuhakikisha utekelezaji wa miradi na uwekezaji
unatekelezwa kwa mujibu wa taratibu na sheria za nchi.
Wa kwanza kulia ni Mheshimiwa Ibrahimu Kifoka (mwenye tisheti ya rangi nyekundu na nyeupe) akiwa katika picha ya pamoja na Mheshimiwa diwani wa Kata ya Sasu Mhe. Jafael Lufungija na mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Mhe. John Kadutu ( mwenye miwani.
“Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua inaamini kila
kiongozi lazima asimamie majukumu yake vizuri kwa ajili ya maendeleo ya
wananchi.
“Hatutakubali fedha za maendeleo zitumike vibaya,
tunataka zitumike vema kwa malengo yaliyokusudiwa,” alisema.
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Bw. Florence Mwale, ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili, alisema uongozi wa
halmashauri hiyo umejizatiti kukabiliana na changamoto za kimaendeleo baina ya
wananchi wake.
Alisema rasilimali na fursa za kimaendeleo zilizopo
wilayani humo lazima zitumike kwa vitendo kutatua adha mbalimbali
zinazowakabili wananchi.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment