Mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha ITV, Ufoo Saro amejeruhiwa
vibaya baada ya kupigwa risasi mbili jana alfajiri huko Kibamba, Dar es Salaam.
Katika
tukio hilo linalodaiwa kufanywa na mzazi mwenzake, Anthery Mushi ambaye alijiua
baadaye, pia anadaiwa kumuua mama yake Ufoo, Anastazia Saro.
Ufoo
alipigwa risasi moja tumboni na kutokea kwenye mbavu na nyingine ilipita
kifuani hadi kwenye ziwa lake la kulia na kutokea kwenye mkono wa kulia.
Baada
ya tukio hilo, Ufoo alipelekwa katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha kabla ya
kuhamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako alifanyiwa upasuaji.
Kamanda
wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo lililosababisha vifo hivyo na kumjeruhi mwandishi huyo.
Kova
alimtaja Mushi, ambaye alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Saro akidai kuhusika
na tukio hilo.
“Mushi alimpiga risasi za kifuani mama yake
Ufoo, ambaye alifariki palepale. Pia alimpiga risasi mwandishi huyo na baadaye
alijiua kwa kujipiga risasi chini ya kidevu, risasi ambayo ilifumua kwa kiasi
kikubwa eneo la juu la kichwa chake.”
Kova
aliwaambia waandishi wa habari waliokuwa katika Hospitali ya Muhimbili kuwa,
vifo hivyo vimetokana na wivu wa mapenzi.
Mashuhuda
wa tukio
Akizungumzia
tukio hilo, mdogo wa mwandishi huyo, Goodluck Saro alisema dada yake Ufoo na
shemeji yake Mushi walikwenda nyumbani kwa mama yao huko Kibamba saa 12.00
asubuhi na kwamba baada ya kufika huko walikuwa na mazungumzo na mama yao
ambayo hata hivyo, hakuyafuatilia kwa kuwa alikuwa amelala.
Goodluck
alisema, muda mfupi baadaye alisikia sauti ya mama yake, ikimwita; “Goodluck
nakufa... Goodluck nakufa.”
Alisema alitoka chumbani na kwenda sebuleni
ambako alimkuta Ufoo akiwa ameanguka chini huku akichuruzika damu.
“Ufoo
aliponiona aliniagiza nirudi chumbani mara moja. Niliporudi chumbani, Mushi
akaanza kupiga risasi ovyo,” alidai Goodluck.
Goodluck
alisema alikuwa chumbani na ndugu zake Jonas Saro na Abel Innocent, ambao
walilazimika kupanda darini ili kuokoa maisha yao.
Alidai
kuwa baada ya Mushi kuona amewakosa ndugu zake Ufoo alikusanya nguo zote na
kuziweka karibu na mtungi wa gesi, ambao aliupiga risasi na kusababisha kuwaka
moto.
“Tukiwa
darini tulizidiwa na moshi tukalazimika kupasua paa na kuruka nje ya nyumba,”
alisema Goodluck.
Baada
ya kutoka nje alisema walipiga simu polisi na ilipotimu takriban saa tatu
asubuhi polisi mmoja alifika lakini baadaye waliongezeka na hivyo kupata
ujasiri wa kuingia ndani ya nyumba.
Mtuhumiwa
akutwa na tindikali, kamba na shoka
Goodluck
alidai kwamba walimkuta shemeji yao akiwa amejiua huku akiwa ameketi kwenye
kiti na kichwa chake kikiwa kimefumuka jambo ambalo alisema wanaamini kuwa
alijipiga risasi.
Goodluck
alisema baada ya ukaguzi, askari walimkuta akiwa na kitu kinachoaminika kuwa ni
tindikali, shoka, mifuko ya plastiki, kompyuta ndogo, kamba, pingu na risasi nane.
“Tunahisi
alikuwa na risasi kama 17 hivi kwani alitumia tisa hivi wakati wa tukio hilo na
zikabaki nane,” alisema Goodluck.
Baadhi
ya majirani walisema walisikia milio ya risasi na wakati wakiulizana kulikoni,
alitokea mtoto anayeishi kwenye nyumba ya marehemu na kuwaomba msaada akisema
kulikuwa na ugomvi.
“Tulipokwenda
tulichungulia na kuona damu zimetapakaa chumba kizima, pembeni tuliuona mwili
wa mama yake Ufoo Saro ukiwa umelala chini. Nyumba ilikuwa imejaa moshi mzito,
tulipiga simu polisi kutoa taarifa,” alisema mmoja wa majirani, Bobroy Ngowi.
Licha
ya kuwa katika maumivu makali, hadi polisi wanafika, Ufoo alikuwa ameshatoka
katika eneo la tukio mwenyewe. Ufoo aelezea mkasa mzima
Akizungumza
kwa taabu wakati akiwa kwenye gari la wagonjwa kutoka Tumbi kuelekea Muhimbili,
Ufoo alisema alijivuta kutoka nje na kutembea mwenyewe hadi barabarani.
Alisema
baada ya madereva wa Boda Boda kumwona anavuja damu nyingi, walimpakia na
kumpeleka Tumbi.
Hata
hivyo, alipofika Tumbi, anasema hakuchukuliwa vipimo kutokana na kutokuwepo kwa
mtaalamu wa x-ray ndipo ilipoamuliwa kuwa apelekwe Muhimbili.
Akiwa
amefuatana na Mwandishi Wetu, Julieth Ngarabali Ufoo licha ya kuwa na maumivu
makali, alisimulia kilichomsibu.
Ilikuwa
baada ya kufika Kibaha mizani Ufoo alipomwita mwandishi wetu: “Julieth naomba
uiname nikusimulie kitu... Unajua aliyefanya haya ni Baba Alvin (Mushi).
Amempiga risasi mama na mimi mwenyewe.”
Baada
ya kusema hivyo, alinyamaza na kuanza kububujikwa na machozi.
Baada
ya kufika Kibamba alipata nguvu na kusimulia kuwa mama yake alikuwa amefariki
katika tukio hilo... Huku akilia, alisema kuwa alipewa taarifa hizo na polisi.
“Masikini
mtoto wangu Alvin sijui itakuwaje, baba yake amejiua, amemuua mama yangu na
babu yake alishafariki... sijui atabakia na nani, maana sijui kama nitapona,”
alisema huku akilia.
Ufoo
ambaye alitoka katika chumba cha upasuaji saa 12 jioni, alisema atakapopata
nafuu ataweka hadharani mkasa mzima uliosababisha mauti na majeraha hayo.
Mushi
ni nani?
Mushi alikuwa mfanyakazi kitengo cha
mawasiliano cha Umoja wa Mataifa huko Darfur, Sudan na alikuwa na uhusiano wa
kimapenzi na Ufoo kwa zaidi ya miaka 10.
Pia
aliwahi kufanya kazi ITV na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), akiwa mpigapicha
wa televisheni.
Baada
ya kuondoka kwenye fani ya habari alijiunga na Mahakama ya Kimataifa
inayoshughulikia kesi za Rwanda (ICTR), kabla ya kwenda Sudan.
Ofisa
wa Kitengo cha Habari cha Umoja wa Mataifa huko Darfur, Said Msonda alisema
kuwa Mushi alikuwa amehamishwa kutoka kituo cha El-Jenina na kupelekwa kile cha
Al-Fasha.
“Tulikuwa
tumepanga kumwandalia tafrija ya kumuaga baada ya kurudi kutoka Tanzania na
haya ndiyo yametokea,” alisema.
Kaka
mkubwa wa marehemu, Silva Mushi alisema mdogo wake alikuwa Moshi kabla ya kuja
Dar es Salaam.
“Nilikuwa
sijawasiliana naye siku nyingi na nilikuwa sijawahi kusikia kama alikuwa na
matatizo yoyote na Ufoo,” alisema.
Msemaji
wa familia ya kina Saro, Iddi Lema alisema kuwa mazishi ya mama yake Ufoo
yamepangwa kufanyika Ijumaa katika Kijiji cha Mashari, Machame mkoani
Kilimanjaro.
Lema
alisema msafara wa kuelekea huko utaondoka Dar es Salaam Alhamisi na kwamba ndugu,
jamaa na marafiki watakutana kesho saa 10.00 kwenye Ukumbi wa Urafiki kwa ajili
ya kufanikisha taratibu hizo.
Imeandikwa na Julieth Ngarabali, Aidan
Mhando, Fidelis Butahe, Pamela Chilongola na Sanjito Msafiri
0 comments:
Post a Comment