LATEST POSTS

Thursday, July 10, 2014

CHADEMA WAMVAA SITTA


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimemvaa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, kikisema kuwa hajielekezi kuhakikisha katiba mpya inakidhi moja ya vigezo muhimu ambavyo ni kuwa na uhalali wa kisiasa unaotokana na maridhiano au muafaka wa kitaifa.
Kauli ya CHADEMA imekuja siku moja baada ya Sitta kukaririwa na gazeti moja la kila siku (Sio Tanzania Daima), akisema ameitisha kikao cha wajumbe 27 wa Kamati ya Mashauriano ili kunusuru mchakato wa katiba mpya.
Kwa mujibu wa Sitta, lengo la kikao hicho kitakachofanyika Julai 24 na kuwashirikisha viongozi wa dini, ni kuondoa mpasuko kati ya wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na wajumbe wengine.
Taarifa ya CHADEMA kwa vyombo vya habari jana, iliyosainiwa na Ofisa Habari wake, Tumaini Makene, ilisema kuwa Sitta kama Mwenyekiti wa Bunge hilo, amedhihirisha masuala kadhaa.
Alitaja masuala hayo kuwa ni kutojua anachokitafuta, kwamba katika hali ya juujuu inaweza kudhaniwa kuwa anatafuta suluhu yenye kuleta maridhiano na hatimaye muafaka wa kitaifa kwenye suala la katiba mpya.
“Taarifa yake ikisomwa kwa makini na kina, inaonyesha namna ambavyo ‘harakati’ zake hizo ni mwendelezo wa hila za watawala kusaka katiba mpya kwa kura, badala ya maridhiano yanayosimamia maoni, maslahi na matakwa ya wananchi,” alisema.
Akinukuu, Makene alisema; “Pamoja na mambo mengine, Sitta alisema upo uwezekano wa Ukawa kurudi bungeni lakini wakisusa tena kadiri mjadala utakavyoendelea. Iwapo itatokea hali hiyo, Bunge litaangalia upya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo inataka theluthi mbili kufanya maamuzi.”
Alisema kauli hiyo inadhihirisha kuwa Sitta hajielekezi katika kuhakikisha kuwa katiba mpya inakidhi moja ya vigezo muhimu, ambavyo ni kuwa na uhalali wa kisiasa unaotokana na maridhiano au muafaka wa kitaifa.
“Na hii ndiyo sehemu kubwa inapolalia hila ya walioko madarakani, wakiongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kupanga kutumia wingi wa kura kuamua suala nyeti la katiba mpya, kwa sababu tu wanapigania kuhakikisha matakwa yao yanawekwa mbele kutokana na maelekezo ya vikao vya chama hicho,” alisema.
Katika suala la pili, Makene alisema Sitta ameendeleza lugha ya dharau na kubeza, ambayo ilikuwa ikitumiwa na wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka CCM wanaounda kundi la Tanzania Kwanza.
“Hilo linadhihirika pale aliponukuliwa akisema ‘kutakuwa na watu karibu 27, mimi nikiwa mwenyekiti, atakayevimba kichwa na kudharau, wananchi watajua nia yake ni tofauti na katiba mpya’.
“Kwa mtu yeyote makini, hawezi kuamini kuwa maneno hayo yanaweza kutumiwa na mtu anayetaka kuonekana anasaka suluhu kwenye jambo nyeti kama katiba,” alisema.
Makene aliongeza kuwa maneno hayo ya Sitta yanaibua shauku zaidi ya kujua kwanini tayari anaonekana ‘kujikinga’ kwamba kuna viongozi watadharau huo wito wake au uteuzi wake.
“Je, Sitta amefanya uteuzi huo kama nani kuweza kupata watu 27 nchi nzima, ameanza kushtukia uhalali wa uteuzi wake huo ambao haujulikani kaufanya lini, wapi, katika mazingira gani, akimhusisha nani, anajishtukia kuwa ameteua watu ambao hawatakubalika?” alihoji.
CHADEMA iliendelea kuhoji, kama hao viongozi wa dini ambao amewateua Sitta ni wale wale ambao tayari wamewasikia ndani ya Bunge la Katiba wakisahau wajibu wao katika jamii, kisha wakatoa misimamo yao hadharani kuungana na CCM dhidi ya wananchi?
Makene alisema CHADEMA wanaamini kuwa Sitta tayari ana upande kutokana na taarifa yake kujaribu kuonyesha au kulazimisha taswira kuwa tatizo la mkwamo huu wa katiba mpya ni Ukawa na kuamua kutoliangalia jambo hilo katika ‘picha pana’ na kulichukulia kwa uzito wake.

Chanzo: Tanzania Daima

0 comments: