LATEST POSTS

Thursday, July 10, 2014

Ridhiwani akabidhi sekondari vitanda 267


MBUNGE wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, amekabidhi vitanda 267 katika shule za sekondari za bweni saba jimboni humo vyenye thamani ya sh milioni 53.4.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vitanda hivyo ambavyo vimepatikana kwa ufadhili wa Kampuni ya M.M.I, Ridhiwani alisema ametoa vitanda hivyo ikiwa ni kutekeleza ahadi zake alipokuwa akiomba kura kuongoza jimbo hilo Machi mwaka huu.
Shule zilizonufaika na msaada na idadi ya vitanda kwenye mabano ni Lugoba (38), Chalinze (50), Moreto (50), Mandela (25), Talawanda (24), Kiwangwa (25) na Kikaro (60).
Alisema baadhi ya shule tatizo la uhaba wa vitanda limemalizika na zilizobaki watakamilishiwa katika awamu ijayo.
“Nimekabidhi vitanda 267 ambavyo nimesaidiwa na Kampuni ya M.M.I, niliahidi nitamaliza tatizo la uhaba wa vitanda kwenye shule za sekondari za bweni katika jimbo langu, nimeanza kutimiza na ifikapo Desemba tatizo hili liwe limekwisha,” alisema.
Ofisa Mawasiliano wa M.M.I, Abubakary Mlawa, alisema vitanda hivyo vimetolewa kupitia kampuni ya Mamba Cement baada ya kupata maombi kutoka kwa mbunge huyo.
Mlawa alisema kampuni yao imekuwa ikisaidia changamoto mbalimbali shuleni, ili kuwajengea wanafunzi mazingira mazuri ya kupata elimu, waweze kuongeza idadi ya ufaulu.

Chanzo: Tanzania Daima

0 comments: