LATEST POSTS

Tuesday, July 2, 2013

SHEREHE YA SIKU YA SERIKALI ZA MITAA YAFANA WILAYANI URAMBO


Kila tarehe 1 Julai, huwa ni siku yamaadhimisho ya siku ya Serikali za Mitaa, maadhimisho ambayo hutoa fursa kwa jamii nzima kutafakari kwa kina juu ya utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo iliyopangwa na iliyotekelezwa katika kipindi cha mwaka husika, lakini pia kutafakari mipango ijayo kwa lengo la kuhakikisha kuwa, mipango yote inatokana na matakwa ya Wananchi wenyewe ili kupambana na umasikini na kujiletea maendeleo endelevu, pia kutambua ubora wa huduma zitolewazo na Halmashauri kwa Wananchi wake.
Ujumbe wa maadhimisho hayo kwa mwaka huu wa 2013 ni " AMANI,UADILIFU, NA UWAJIBIKAJI KWA WOTE NI NYENZO MUHIMU KATIKA MCHAKATO WA KATIBA MPYA NA USTAWI WA SERIKALI ZA MITAA".
Kwa Wilaya ya Urambo ( Wilaya ya Urambo na Kaliua), maadhimisho haya yalifanyika Kiwilaya katika Kata ya Igagala iliyopo Kaliua ambapo mgeni rasmi alikuwa Mhe. Saveli Mwangasame Maketta ambaye kwabahati mbaya hakuweza kuhudhuria na badala yake aliwakilisha na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Mhe. Haruna Kasele (Diwani wa Kata ya Kazaroho).
Akiwasilisha taarifa fupi ya maendeleo ya Halmashauri ya Wilaya ya Urambo kwa mgeni rasmi Mhe.Haruna Kasele,Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Bw. Gwatako N.Gwatako alisema kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Urambo katika mwaka 2012/2013, imetekeleza shughuli mbalimbali za Maendeleo kwa Wananchi wake zikiwemo za kiuchumi na za kijamii zenye jumla ya Tshs. bilioni mbili, mia sita thelathini na tano milioni, mia nane ishirini na saba elfu, mia nane sitini na nane na senti ishirini na nane zilizotolewa katika mwaka wa fedha wa 2012/2013. Aidha alisema,shughuli hizo zilifanikiwa kutokana na ushirikiano wa Wananchi, Wataalamu, Viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa madhehebu ya dini, Serikali kuu na Wafadhili mbalimbali wa ndani na nje.
Mkurugenzi huyo aliendelea kutaja mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika idara mbalimbali na vitengo vya Halmashauri hiyo ikiwemo idara ya elimu msingi ambapo kwa sasa, Halmashauri ya Wilaya ya Urambo ina jumla ya shule za Msingi 167 kutoka shule za Msingi 156 zilizokuwepo mwaka 2011/2012. Hivyo kuna ongezeko la shule mpya 11 zilizosajiliwa kati ya shule 18 ambazo zinatarajiwa kusajiliwa.
Akisoma hotuba kwa niaba ya Mgeni rasmi katika sherehe hiyo Mhe. Haruna Kasele alisema kuwa, ujumbe wa mwaka huu wa maadhimisho hayo ni muhimu sana hasa kwakuzingatia kuwa, Serikali imeunda tume ya kuratibu maoni ya Wananchi kuhusu uundwaji wa Katiba mpya itakayoendelea kujenga umoja wa Kitaifa. Aliwataka Wananchi wote kujitokeza kushiriki katika kutoa maoni yao kupitia mabaraza ya Katiba katika ngazi zote.
Aidha, alisisitiza suala la usimamizi wa miradi ya maendeleo iliyopo kwenye maeneo yao ili ikamilike kwa wakati na iwe na thamani ya fedha kwani miradi mingi imekuwa haitekelezwi kama inavyopaswa na kusababisha fedha za Serikali pamoja na michango ya wananchi kutotumika kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa mgeni rasmi aliwaagiza wananchi kuwa, maendeleo yao yataletwa na wao wenyewe hivyo wawe tayari kushiriki katika shughuli za miradi ya maendeleo na kuhakikisha kwamba inakuwa endelevu.
Kwa upande wa sekta ya afya, Mheshimiwa mgeni rasmi alisema kuwa, Serikali inajitahidi kwani kwa sasa, Wilaya ya Urambo( Urambo na Kaliua) ina magari ya kubebea wagonjwa manne ambapo Halmashauri imezigawa gari hizi kwa kila Tarafa yaani Urambo gari moja,Ulyankulu gari moja (msaada wa TCRS), Usoke gari moja na Kaliua gari moja. Alisema, uwepo wa magari haya umesaidia sana kupunguza vifo vya akina mama na watoto na kuwezesha wagonjwa mahututi kufikishwa hospitali kwa wakati. Aidha,Serikali imenunua pikipiki za miguu mitatu sita ambazo tatu zimegawiwa Urambo na tatu zimegawiwa Kaliua kwa ajili ya kubebea wagonjwa ( wakina mama wajawazito wanaopata matatizo wakati wa kujifungua).
Mwisho, alisistiza wananchi kujitolea nguvu kazi (20%) kwa ajili ya kutekelea miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao ili miradi iweze kuwa na ubora kwa kuwa kutokana uchangiaji hafifu wa nguvu za Wananchikwenye miradi ya maendeleo  shughuli nzima ya ujenzi itatumia 80% ya gharama hitajika na hivyo miradi haiwezi kukamilika 

Kikundi cha sanaa cha mapigo tisa kutoka Igagala kikitoa burudani katika siku ya Serikali za Mitaa

Maafisa usalama Wilaya ya Urambo na Kaliua

Wenyeviti wa CCM. Kushoto ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kaliua na Kulia ni Mama Martha Susu Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Urambo

Kusho Mwenye suti ni Mheshimiwa Haruna Kasele Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo ambaye alimwakilisha mgeni Rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Serikali za Mitaa.

Kushoto mwenye suti ya Blue ni aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Ndugu Gwatako N.Gwatako. Kulia ni Mhe. Haruna Kasele.

Wenyeviti wa CCM Wilaya Kaliua na Urambo wakifurahia jambo

Kwaya ya Mapigano ya Igagalatayari kwa kutoa burududani

Kutoka kushoto ni Afisa Tawala Wilaya ya Urambo na kulia ni Mhe. Modester Buyobe Diwani wa Kata ya Seleli na pia ni Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kaliua.

 
 
 

0 comments: