LATEST POSTS

Friday, April 25, 2014

Yajue malezi kwa mtoto chini ya miaka mitatu

Malezi na ukuaji wa mtoto ni masuala muhimu kwa kila mzazi. Katika makala haya nitaeleza kidogo kuhusu maendeleo ya mtoto tangu anapozaliwa hadi kufikia umri wa miaka mitatu.
Kipindi hiki ni muhimu kwani maeneo yote ya mtoto yanakua kwa kasi. Ziko sehemu tatu zinazoonyesha dalili za ukuaji huu nazo ni sehemu za ubongo, ukuaji wa hisia na stadi na mwishowe ni ukuaji wa ufahamu wa lugha kulingana na jamii inayomzunguka.
Ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2010 inaonyesha kuwa vifo kwa watoto wachanga katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara vinaongezeka.
Aidha, kwa watoto walio hai hasa wa umri wa mwaka moja, theluthi moja wana utapiamlo. Sababu za utapiamlo zinatajwa kuwa ni pamoja na umaskini, hali mbaya ya uchumi inayosababishwa na vita, mkusanyiko wa watu, maradhi kama Ukimwi na malaria na upweke.
Misingi mingi ya utamaduni inasambaratishwa kutokana na wanawake kushiriki katika kilimo shambani, kuajiriwa katika mashamba makubwa kama vibarua, kukimbilia mijini kutafuta ajira viwandani na nyumbani, uhamaji inaosababishwa na kukosa amani na utulivu maeneo ya asili kutokana na vita.
Zaidi ya hayo, ziko familia zenye mzazi mmoja na mara nyingi ni wanawake wasioolewa. Malezi kwa watoto wanaozaliwa katika familia hizi wana matatizo chungu nzima.
Watafiti wa masuala ya watoto wamebaini kuwa mtoto anapozaliwa, uzito wa ubongo wake ni asilimia 25 ya uzito wa ubongo wa mtu mzima. Anapotimiza miaka mitatu uzito wa ubongo huongezeka kwa kuzalisha mamilioni ya seli na viunganishi baina ya seli hizi zanazojulikana kama ‘synapses’.
Lipo pia suala la kutengamana kijamii na kisaikolojia kwa maana kwamba mwingiliano wa jamii kwa malezi ya mtoto ni jambo la kuzingatiwa.
Ziko changamoto nyingi anazokabiliana nazo mtoto anapokua. Mambo hayo ni kutokuridhika na hali anayoishi na kulia mfululizo bila sababu zinazoeleweka.
Changamoto hizi zinatofautiana kati ya mtoto na mtoto kwani kwa kawaida watoto hawafanani katika hisia zao. Kila mtoto anazaliwa akiwa na hisia zake.
Kulala usingizi ni eneo mojawapo linalowakera wazazi hasa katika kipindi cha mwanzo cha uhai wa mtoto. Ziko njia zinazotumika katika kushughulikia watoto wanaolia ili wapate usingizi.
Kwanza ni kuchunguza kama mtoto ana njaa, ni mgonjwa au ana kiu. Njia nyingine ni kuchunguza kama kuna kero katika sehemu anayokaa kama kuna unyevu, joto au baridi.
Wazazi wengi hupenda kulala na watoto wao wachanga lakini ifahamike kuwa nguo zitumikazo katika kitanda cha wakubwa hazifai kutumiwa na watoto wachanga.
Kama ukiamua kulala na mtoto jitahidi kumlaza karibu nawe lakini kwenye kitanda kidogo kilichoambatishwa na hicho cha mzazi wake au unaweza kutengeneza kitanda kidogo cha mtoto karibu na kitanda chako ili uwe karibu na mwanao.
Pamoja na tahadhari zote hizo haishauriwi kulala na mtoto kama mzazi anavuta sigara, ana kunywa pombe, ana mafua, ni mwenye usingizi mzito. Hizi ni hatua za kuzingatia katika malezi.

0 comments: