UONGOZI wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kupitia kitengo
cha Ustawi wa jamii umemtafutia kituo cha kulelea watoto wa mitaani cha Nuru
Ophans Centre Mama aliyejifungua mapacha wanne na kubakia wawili baada ya kuugua
Nimonia kwa ajili ya uangalizi wa karibu.
Hatua hiyo imekuja baada ya uongozi wa Hospitali hiyo
kumfuata mama mwenye watoto hao Aida Nakawala(25) pamoja na mapacha wake
waliobaki kutoka kijijini kwao Chiwanda Wilaya ya Momba mkoani hapa na kuwalaza
hospitalini hapo kwa uangalizi wa karibu kwa muda wa zaidi ya wiki
moja.
Aidha baada ya afya za watoto hao kuimarika kwa kiwango
kikubwa pia Uongozi wa Hospitali hiyo imemtafutia hifadhi katika kituo cha
kulelea watoto wa mitaani cha Nuru kilichopo Uyole jijini Mbeya kwa ajili ya
uangalizi wa karibu kutoka kwa wauguzi na maafisa wa ustawi wa Jamii kutoka
Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati akiwakabidhi
watoto hao pamoja na mama yao kwenye uongozi wa kituo cha Nuru Orphans centre,
Katibu wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Aisha Mtanda, alisema wameguswa na
mazingira anayoishi mama huyo na kuamua kumpa uangalizi kwa miezi sita
zaidi.
Alisema jukumu hilo halipaswi kufanywa na Hospitali kwa
kuwa tayari walikuwa wamemaliza jukumu lao la kumhudumia alipokuwa ana matatizo
lakini wamelazimika kubeba jukumu hilo baada ya kuguswa na mazingira na hali ya
makazi ya familia hiyo.
Alisema Hospitali imekubaliana na uongozi wa Kituo cha
Nuru kwamba apewe hifadhi mama huyo na watoto wake ili apate uangalizi wa karibu
ikiwa na lengo la kunusuru maisha ya watoto waliobaki kutokana na wengine
kupoteza maisha kiuzembe kwa ugonjwa wa Nimonia.
Aliongeza kuwa Hali ya hewa ya Mkoa wa Mbeya kwa siku
zijazo kunakuwa na baridi kali sana hivyo watoto wasipokuwa kwenye uangalizi wa
karibu wanaweza kupatwa na ugonjwa wa Nimonia tena kwa kukosa matunzo kama ya
awali.
Kwa upande wake, Meneja wa Kituo cha Nuru, Amanda
Fihavango alisema alikubali jukumu la kuwapokea watoto hao pamoja na mama yao
kutokana na kuguswa na hali iliyowakuta ya kupotea kwa watoto wawili kati ya
wanne.
Aliongeza kuwa ingawa anakabiliwa na changamoto nyingi
zikiwemo za kiuchumi atajitahidi kwahudumia kadri ya uwezo wake na kuomba
wasamaria wema watakaoguswa na jambo hilo kujitolea kwa hali na mali kufanikisha
kuokoa uhai wa watoto hao pamoja na wengine anaowalea.
Alisema kituo chake hupokea watoto waliookotwa baada ya
kutupwa na wazazi wao au mama zao kufariki mara baada ya kutoka kujifungua ambao
hupelekwa na Serikali kupitia Ustawi wa Jamii ingawa haichangii fedha zozote
baada ya kuwapeleka.
Mtu yoyote mwenye kuguswa anaweza kuwasilisha mchango
wake kituoni hapo au kuwasiliana na Meneja wa Kituo cha Nuru kupitia namba za
Simu 0754 043004 kwa ajili ya kusaidia watoto hao pamoja na mama yao
kuishi hapo kwa muda wa miezi sita.
|
0 comments:
Post a Comment