LATEST POSTS

Tuesday, March 18, 2014

Maajabu ya Shule ya Sekondari Tongoni

Sehemu ya mandhari ya Shule ya Sekondari Tongoni iliyopo mkoani Tanga. Shule hii ni miongoni mwa shule zilizoshika mkia katika Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2013.
 
Tangu ianzishwe mwaka 2007, haijawahi kuwa na mwanafunzi aliyepata daraja la kwanza, la pili wala la tatu. Mwaka huu haina wanafunzi wa kidato cha nne, kwa kuwa wanafunzi 44 kati ya 47 walifeli mtihani wa kidato cha pili mwaka juzi.
 
Shule ya Sekondari Tongoni ni moja ya shule zilizofanya vibaya katika matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne mwaka 2013.
Katika matokeo hayo yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) Februari mwaka huu, shule hiyo, iliyopo Wilaya ya Tanga Mjini mkoani Tanga, ilishika nafasi ya tatu kati ya shule 10 za mwisho kitaifa.
Hii siyo mara ya kwanza kwa Tongoni kuwa katika kundi la shule zinazoburuza mkia katika mitihani ya kidato cha nne. Mwaka 2012 pia ilikuwamo katika orodha ya shule 10 za mwisho.
Historia ya shule hiyo, iliyopo karibu kilometa 20 kutoka Tanga Mjini, inaonyesha tangu itoe wahitimu wa kwanza wa kidato cha nne mwaka 2010, haijawahi kuwa na mwanafunzi aliyefaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza, la pili na la tatu.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Shule hiyo, Mfaume Juma, kilele cha hali duni ya taaluma shuleni hapo kinajidhihirisha mwaka huu kwa kutokuwa na wanafunzi wanaosoma kidato cha nne.
Hali hiyo anasema inatokana na wanafunzi 44 kukariri kidato cha pili baada ya kufeli mtihani wa kidato cha pili mwaka 2012. Wanafunzi waliofaulu mtihani huo walikuwa watatu tu, jambo lililowalazimu kuwahamishia shule nyingine.
 
Sababu za kufanya vibaya
Kwa mujibu wa Mwalimu Juma, Sekondari ya Tongoni inakabiliwa na changamoto kubwa za utoro uliokithiri, uchelewaji shule, vitendo vinavyoshadadiwa na wazazi kukosa mwamko wa elimu.
“Uchelewaji huu ni wanafunzi wa kisiwa cha Mwarongo pamoja na wa mjini Tanga. Hawa wa Tanga hadi walisubiri basi la Raha Leo linalokwenda Pangani, basi linatoka Tanga saa 1:30 na kufika huku kati ya saa 2:40 na saa 3:20,” anaeleza na kuongeza kuwa kwa wanafunzi wa Mwarongo wanaoishi kisiwani wanalazimika kusubiri kivuko ambacho siyo cha uhakika.
 
Ina nyenzo lakini inafelisha
Imezoeleka kwamba sababu kubwa ya kudorora kwa elimu katika shule nyingi za umma ni ukosefu wa walimu na nyenzo za kujifunzia kama vile vitabu na maktaba.
Hata hivyo, Shule ya Sekondari Tongoni pamoja na kupata bahati ya kuwa na walimu na vifaa, bado imeendelea kufanya vibaya, jambo linaloshangaza wadau wa elimu.
Kwa mfano, Ofisa Elimu ya Sekondari Jiji la Tanga, Bashiry Shellimo anasema shule hiyo ina bahati ya kupangiwa walimu wa kutosha karibu masomo yote.
“Hii shule ina jumla ya wanafunzi 123 wasichana wakiwa 52 na71 ni wavulana. Ina madarasa na madawati mengi kuliko mahitaji, ina vitabu vya kutosha, ina maabara inayohamishika,’’anasema.
 
Nidhamu kwa wanafunzi
Shule hii inakabiliwa na changamoto nyingine tete ya wanafunzi wake kujihusisha na vitendo vya kihuni, ikiwamo kuwa na uhusiano wa kimapenzi.
Pamoja na uongozi wa shule kushindwa kukubali au kukana uwepo wa vitendo hivyo, wakazi wanaoishi jirani na shule wanasema vitendo vya ngono vimetamalaki, tena vikifanywa dhahiri na wanafunzi.
“Watatafuta mchawi wa matokeo mabaya ya kidato cha pili na cha nne katika shule yetu ya Tongoni hawatampata kamwe, lakini kiukweli lazima niseme wazi ni hao wenyewe wanafunzi hawataki kusoma badala yake wanaendekeza uzinifu nyakati za masomo,’’anasema mkazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Malau Bakari.
Anaongeza: “Ikigongwa kengele ya mapumziko saa nne utakuta wasichana na wavulana wanaingia vichakani, tena huku jirani na nyumbani kwangu. Wanafanya ngono waziwazi na hii imekuwa ni desturi kwao tangu ilipoanzishwa mwaka 2007. Tangu muda huo mpaka leo wanafunzi wanaigana kwa kufanya uzinifu.”
Hoja ya nidhamu mbaya kwa wanafunzi hao, inaungwa mkono na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya shule hiyo, Omari Bashiri, ambaye hata hivyo anawashukia wanafunzi kutoka nje ya eneo la Tongoni kuwa ndiyo wanaoharibu sifa ya shule.
Anasema wanafunzi hao kutoka Tanga mjini na Mwarongo, wamekuwa wakieneza sumu mbaya kwa wenzao wanaowasema wanaishi kijijini ilipo shule.
 
Adhabu kwa walimu
Kutokana na kufanya vibaya, huku shule ikiwa na mazingira mazuri ya kitaaluma, Idara ya Elimu ya Halmashauri ya Jiji la Tanga, imelazimika kuchukua hatua za kuwashusha vyeo na kuwahamisha Mkuu wa Shule na Makamu wake.
Ofisa Elimu Sekondari mkoani humo, Bashiry Shellimo anasema hatua hiyo ni mwanzo wa kuhakikisha shule za sekondari zilizopo jijini Tanga hazifanyi tena vibaya katika mitihani ya taifa.
“Tumeshtushwa na matokeo ya mwaka huu. Shule ya Tongoni na nyingine mbili zimo katika orodha ya shule 10 zilizoshika mkia, hii ni aibu, anaeleza.

0 comments: