ASKARI wa Jeshi la Polisi na raia mmoja wamefikishwa
mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Mbeya wakituhumiwa kwa makosa mawili ambayo ni
kula njama za kutenda kosa pamoja na wizi wa mtoto.
Watuhumiwa hao ni pamoja na Mshtakiwa wa kwanza aliyekuwa
Ditektivu Constebo wa Polisi mwenye namba WP 5367 Prisca Isaya (35) mwenyeji wa
Ilala Dar es salaam ambaye hata hivyo alivuliwa vyeo na kufukuzwa kazi kabla ya
kupandishwa Mahakamani na Salehe Mwangosi (28) mkazi wa Njisi wilayani Kyela
Mkoa wa Mbeya.
Akisoma mashtaka yanayowakabili Mwendesha mashtaka wa
Serikali, Juliana William, mbele ya Hakimu wa Wilaya ya Mbeya, Maria Batulaine,
alisema watuhumiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na makosa mawili waliyoyatenda
Aprili 4, Mwaka huu.
Alisema kosa la kwanza ni kula njama kwa nia ya kutenda
kosa la kuiba mtoto kinyume cha kifungu cha 384 (16) cha kanuni ya adhabu
kilichofanyiwa marejeo mwaka 2002 walilofanya Aprili 4, Mwaka huu katika eneo la
Songwe wilayani Kyela.
Alitaja kosa la pili kuwa ni Wizi wa mtoto kinyume cha
kifungu cha 169 (1) (a) sura ya 16 ya kanuni ya adhabu kama ilivyofanyiwa
marekebisho mwaka 2002.
Mwendesha mashtaka huyo aliiambia Mahakama kuwa
washtakiwa wote kwa pamoja mnamo Aprili 6, Mwaka huu katika eneo la Zahanati ya
Njisi Wilaya ya Kyela Mkoani hapa kwa maksudi waliiba mtoto mwenye umri wa siku
saba kutoka kwa mama yake mzazi Mboka Mwakikagile.
Washtakiwa wote kwa pamoja walikana kuhusika na tukio
hilo ambapo upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa shauri hilo umekamilika na
upo tayari kuwaleta mashahidi wake kwa ajili ya kuendelea na usilizwaji wa
kesi.
Kwa upande wake Hakimu aliahirisha kesi hadi Mei 6, Mwaka
huu na kwamba dhamana kwa washtakiwa iko wazi kama watakidhi vigezo ambavyo ni
kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wenye mali zisizo hamishika zenye thamani ya
shilingi Milioni 5, barua ya mtendaji na barua kutoka kwa mwajiri kwa ajili ya
mshtakiwa wa kwanza.
Hata hivyo walishindwa kuwa na wadhamini waliokidhi
vigezo vya mahakama na kuamliwa kurudishwa rumande hadi Mei 6, Mwaka huu kesi
itakapo kuja kwa ajili ya kusikilizwa.
Chanzo: Mbeya yetu
|
0 comments:
Post a Comment