Mmiliki wa nyumba iliyogongwa na basi la Luhuye Kijiji cha Itwimila A, wilayani Busega, mkoani Simiyu ametaka mmiliki wa basi hilo kumlipa fidia ya Sh40 milioni kutokana na kupoteza mali nyingi.
Paulina Luge, ambaye ni mjane alisema gari hilo liliacha njia na kupinduka mara tatu hatimaye ikagonga nyumba yake yenye vyumba vitano na kusababisha hasara kubwa ya samani, hali ambayo imemrudisha nyuma kimaendeleo.
Luge alisema hivi sasa familia yake inaishi kwa tabu, huku vijana wakiume wakilala kwenye hema na mabinti wanalala kwa majirani.
Alisema tayari Serikali ya Kijiji cha Itwimila imefanya tathmini ya hasara iliyosababishwa na basi hilo na kwamba, inatarajia kupeleka taarifa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Busega.
Alisema alikuwa akitoka kwa majirani aliona basi linakuja ghafla lilianza kupinduka kuelekea kwenye nyumba yake, alipiga makelele huku akiwataka watoto kutoka ndani.
“Nashukuru Mungu watoto waliwahi kutoka, ndipo basi hilo liligonga mti hatimaye ukuta wa nyumba yangu na kuanguka, limeharibu kila kitu hakuna nilichotoa ndani,” alisema.
Alitaja vitu vilivyoharibiwa kuwa ni vitanda vine, makochi jozi moja, baiskeli tano. meza tatu na kufa kwa mbuzi watano.
Mtoto wa mwenye nyumba
Flora Luge (15), ni mtoto wa mmiliki wa nyumba anasoma darasa la saba Shule ya Msingi Itwimila, alisema baada ya mama yao kuwataka kutoka nje haraka, yeye (Flora) alikuwa chumbani, akiwa kwenye harakati za kujiokoa alipigwa na tofali mkono wake wa kushoto na kuumia.
“Baada ya kutoka nje nilishtuka kukuta watu wamejaa na wengine wanaruka kutoka ndani ya basi, ambao wengine walikuwa wamefunikwa nguo na kuingizwa kwenye magari huku wengine wakilia kwa uchungu kutokana na maumivu waliyopata,” alisema.
Katika ajali hiyo, watu kumi walifariki papo hapo na mmoja alikufa njiani akipelekwa Hospitali ya Rufani ya Bugando, huku wengine watano wakifariki hospitalini.
Kauli ya mtendaji wa kijiji
Mtendaji wa Kijiji cha Itwimila A, James Mayiga alisema siku ya tukio uongozi wa wilaya kupitia Ulinzi na Usalama walifika kutoa pole na kwamba, waliahidi kufuatilia fidia ya nyumba na mali zilizokuwamo ndani.
Mayiga alisema Mkuu wa Wilaya ya Busega, Paul Mzindakaya aliwataka uongozi wa kijiji kufanya tathmini ili kujua thamani halisi ya mali zilizoharibiwa, ili kuweza kudai fidia ikiwamo ujenzi wa nyumba hiyo.
Alisema alifika eneo hilo baada ya kupigiwa simu na wananchi, alianza kusaidia majeruhi.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment