Mabadiliko makubwa ya matumizi ya barabara katikati ya Jiji la Dar es Salaam yanaanza rasmi Jumatatu.
Hatua hiyo inalenga kupunguza msongamano wa magari na kuimarisha hali ya usafiri
Mabadiliko yatakayofanyika
Kwa kiwango kikubwa, mabadiliko hayo yataathiri watumiaji wa magari binafsi na ya abiria. Mabasi yote yanayopita Barabara ya Kilwa sasa yataishia Stesheni na kurudi kupitia njia hiyohiyo.
Mabasi yanayopita Barabara za Nyerere na Uhuru, yataishia Mnazi Mmoja na kurudi kupitia njia zao. Pia kutakuwa na mabasi yatakayoanzia Mnazi Mmoja kupitia Bibi Titi, Maktaba hadi kituo cha Posta ya Zamani – Benki ya NBC na kurudi kupitia njia hiyohiyo.
Mabasi yote yanayopita Barabara ya Ali Hassan Mwinyi kwenda katikati ya jiji yataishia katika Kituo cha YMCA, Barabara ya Upanga na kurudi kupitia njia hiyo.
Katika Barabara ya Sokoine, magari yatakayoruhusiwa ni ya binafsi kuanzia Kituo Kikuu cha Polisi kwenda Kivukoni, Hospitali ya Ocean Road hadi kwenda kuungana na barabara nyingine ikiwamo ya Ali Hassani Mwinyi.
Kwa upande wa Barabara ya Samora, badala ya kuanzia Mnara wa Saa kwenda hadi Hospitali ya Ocean Road, sasa magari madogo binafsi yataanzia katika hospitali hiyo (Ocean Road) kurudi Mnara wa Saa. Kwa mujibu wa mabadiliko hayo, njia zote za daladala hazitakatiza katika barabara ya Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (BRT), isipokuwa yanayotoka Mnazi Mmoja kwenda Posta ya Zamani ambayo yatakatiza katika eneo la Akiba katika makutano ya Barabara za Morogoro na Biti Titi.
Akizungumzia mabadiliko hayo, dereva teksi anayefanya shughuli zake katikati ya jiji, Salumu Hamdan alisema hakuwa na taarifa za mabadiliko hayo hadi jana.
Hata hivyo, Meneja Uhusiano wa Wakala wa Usafiri wa Haraka (Dart), William Gatambi alisema ofisi yake imetoa matangazo kupitia vyombo mbalimbali vya habari ili kuwafahamisha wananchi mabadiliko yao.
Gatambi alisema alama za kuongoza watumiaji wa barabara bado zinaandaliwa na muda wowote zitawekwa ili kuleta ufanisi katika mabadiliko hayo... “Hayo ni mabadiliko ya kawaida, wananchi watayazoea tu.”
0 comments:
Post a Comment