Matukio ya baadhi ya wanawake kukamatwa, kudhalilishwa mbele ya familia kwa kushikwa sehemu za siri bila ya ridhaa yao, na kubakwa wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Majangili nchini, ni muendelezo wa madhila mbalimbali yanayoendelea kuwakumba wanawake nchini.
Hayo yamebainishwa katika Ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyoongozwa na mwenyekiti wake James
Lembeli iliyosomwa bungeni hivi karibuni.
Operesheni hiyo ilifanyika katika maeneo mbalimbali ya nchi
iliyoongozwa na wizara tatu za Maliasili na Utalii, Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa na Wizara ya Mambo ya Ndani.
Lengo la operesheni hiyo ni kuwatafuta, kuwakamata na ikibidi
‘kuwaua’ kama si kuwachukulia sheria majangili wanaoua tembo kwa ajili
ya kupata meno yake na vifaru kwa ajili ya vipusa, badala yake baadhi ya
waliopewa dhamana hiyo wakaacha lengo la msingi na kujikuta
wakiwakamata wanawake, kuwachomea nyumba, kuwadhalilisha kwa kiwango cha
kutisha na kuwabaka.
Mwanamke mmoja (jina linahifadhiwa) wilayani Babati alivuliwa nguo
na kulazimishwa kufanya mapenzi na wakwe zake kisha kuingizwa chupa
sehemu zake za siri.
Mama mwingine mkazi wa Kata ya Matongo wilayani Bariadi, alibakwa na askari watatu huku akiwa ameshikiwa mtutu wa bunduki.
Tukio la kuuawa kinyama kwa Emiliana Gasper Maro lilipotolewa na
vyombo vya habari, Serikali kupitia Mkurugenzi wa Wanyama Pori ilitoa
taarifa kwa umma ikipinga taarifa iliyorushwa kwenye vyombo vya habari
Oktoba 19, mwaka huu kuhusu mauaji ya kutisha yaliyofanywa na askari wa
kupambana na ujangili.
Serikali iliwatetea askari wa Operesheni Tokomeza Ujangili kuwa hawahusiki na kifo cha Emiliana.
Hata hivyo, taarifa ya utetezi ilizungumzia majina mawili tofauti
ya Evelyn Gasper na Mariana Gasper Mallo wa eneo la Olongadiola wakati
muathirika halisi ni Emiliana Gasper Maaro mkazi wa kijiji cha Omgadida,
Gallapo.
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) kwa kushirikiana na
Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP), Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania
(TAWLA),Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (Zafela) na Kituo cha
Usuluhishi cha Tamwa (CRC), inatekeleza mpango wa kutokomeza ukatili na
unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto (Gewe II) katika
wilaya 10 za Tanzania Bara na Zanzibar.
Ili kufanikisha mpango huo wa miaka miwili (2012-2014) Tamwa
iliongoza uundaji wa kamati katika wilaya 10 kwenye vijiji 60 vya
Tanzania Bara na Zanzibar zenye jumla ya wajumbe 720.
Kazi kubwa ya kamati hizo ni kufuatilia masuala ya ukatili unaofanywa dhidi ya wanawake na watoto wa kike kwenye maeneo yao.
Taarifa ya Ripoti ya Kamati ya Bunge iliyochunguza sakata hilo,
yawezekana imepita sehemu ndogo ya hali halisi ya matukio yalivyokuwa
nchini kutokana na muda iliopewa, uchache wa wajumbe ambao siyo rahisi
kupita kila kijiji na kila sehemu, hivyo kuwa na uwezekano mkubwa wa
baadhi ya matukio haya kubainishwa wazi licha ya kuathiri wanawake na
watoto.
Hivyo ni muhimu kwa wanaharakati popote walipo ikiwa ni pamoja na
Kamati zilizoundwa na Tamwa katika maeneo mbalimbali ya nchi kuendelea
kufichua madhila mbalimbali yaliyowapata watu kutokana na operesheni hii
ambayo baadhi ya watu wamepata vilema vya kudumu na vifo wakiwamo
baadhi ya wanaume na watoto.
Baadhi ya wananchi waliopoteza maisha katika operesheni hiyo na
vijiji vyao kwenye mabano ni Wegesa Kirigiti (Remagwe), Peter Masea
(Mrito-Tarime), Mohamed Buto, Massi na Gervas Nzoya (Kasulu-Kigoma).
Utekelezaji wa Operesheni hiyo ni dhahiri umekiuka sheria hasa
ibara ya 14 ya Katiba isemayo “Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata
hifadhi ya maisha yake kutoka kwa jamii kwa mujibu wa sheria” na ibara
namba 15 (1) isemayo “ kila mtu anayo haki ya kuwa huru na kuishi kama
mtu huru”.
Inatisha kuona askari wa Jeshi la Wananchi na Jeshi la Polisi
walioiva kimafunzo kuthamini ustaarabu, kujali utu, kuheshimu na
kuzingatia haki za binadamu wanageuka na kufanya unyama kama huo dhidi
ya maisha ya raia na mali zao ambao walipaswa kutumia mafunzo yao
kuwalinda.
Tayari mawaziri wanne wamejiuzulu kutokana na kadhia hiyo ambao ni
Mawaziri wa Maliasili na Utalii Balozi Khamis Kagasheki, Mambo ya Ndani
Dk. Emmanuel Nchi, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Shamsi Vuai Nahodha
na wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dk. Mathayo David.
Sasa inasubiriwa kuundwa Tume ya Kimahakama ili matokeo ya kina zaidi yapatikane na hatua zaidi zichukuliwe kwa wahusika wote.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
0 comments:
Post a Comment