LATEST POSTS

Thursday, January 2, 2014

Sitta: Hatuwezi kuwa na marais watatu

     http://freemedia.co.tz/daima/wp-content/uploads/2014/01/sitta.jpg
 Mhe. Samwel Sitta

WAKATI Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amewasilisha rasimu ya pili ya mabadiliko ya Katiba kwa Rais Jakaya Kikwete, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Samuel Sitta, amesema Tanzania haiwezi kuongozwa na marais watatu.
Sitta alisema anakubaliana na mawazo ya tume ya Warioba ya kuwa na serikali tatu, lakini hakubali Rais wa Zanzibar na Tanganyika nao waitwe marais kama yule wa Muungano.

Akizungumza na gazeti hili jana, Sitta alisema kuwa ili serikali tatu zifanye kazi kwa kuheshimiana, kuwekeana mipaka, rais wa Tanganyika na wa Zanzibar, wapewe majina na hadhi nyingine ili Tanzania iwe na rais mmoja tu wa Muungano.
“Niliposikia maoni na ufafanuzi wa kina jinsi serikali tatu zitakavyokuwa, nimekubaliana na mawazo ya tume kwamba tuwe na serikali tatu. Lakini kwa maoni yangu tuwe na amiri jeshi mkuu mmoja tu ambaye ni Rais wa Muungano, maana hatuwezi kuwa na marais watatu kwenye nchi mmoja,” alisisitiza.
Waziri huyo mwandamizi wa Serikali ya Rais Kikwete, alitolea mfano wa Shirikisho la Afrika Mashariki (EAC) kwamba rasimu yake imependekeza kuwa na rais mmoja tu na si marais sita wanaounda shirikisho hilo.
Pia alipendekeza jina la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania libadilishwe na badala yake liitwe Shirikisho la nchi za Tanzania.
Akizungumzia msimamo wa Chama chake Cha Mapinduzi (CCM), kupinga serikali tatu na kutaka muundo wa serikali mbili uendelee, Sitta alisema kuwa CCM isibaki kuwa kichwa ngumu kupinga serikali tatu.
Alisema CCM inakosea kung’ang’ania serikali mbili wakati Katiba ya Zanzibar ndiyo iliamua serikali mbili, hivyo serikali ya tatu kwa sasa haiepukiki.
Akitolea mfano, alisema Katiba ya Zanzibar inataka miswaada yote inayopitishwa na Bunge la Jamhuri iridhiwe kwanza na Baraza la Wawakilishi, jambo ambalo alisema si sahihi.
Alisema Katiba ya Zanzibar imefanya mambo mengi kuihalalisha Zanzibar kuwa nchi kamili na imefanya mambo hayo bila ridhaa ya Tanzania Bara.
Alisema ili kubaki na serikali mbili, lazima Zanzibar ikubali kuifumua Katiba yake inayotoa mamlaka kamili kwa rais wa visiwa hivyo, jambo ambalo alisema Wazanzibari hawawezi kulikubali.
“Mimi nilipomsikiliza Jaji Warioba safari hii, jinsi alivyojenga hoja ya serikali tatu, nimeona kuna hoja za msingi sana zipo kwa sababu kuna mambo makubwa na ya msingi yameshafanyika. Huwezi kupitisha Katiba inayosema miswada inayopitishwa bungeni isifanye kazi Zanzibar hadi Baraza la Wawakilishi likae na kuridhia, ukishafika hapo, basi serikali tatu haziepukiki,” alisisitiza Sitta.
Sitta alisema tume ya Warioba imefanya kazi kubwa na nzuri kwani rasimu ya pili imekwenda mbali kuangalia vitu kama zawadi za viongozi, jambo ambalo zamani viongozi waliona ni haki yao kupata zawadi za aina hiyo bila kujali kwamba hiyo ni rushwa.
Kwa mujibu wa Sitta, kuna mambo ya msingi ya kuendelea kujadili nje na ndani ya CCM nayo ni namna ya kuiendesha Serikali ya Muungano kwani kwa maoni ya tume, serikali hiyo itakuwa ikichangiwa zaidi na Tanganyika, jambo ambalo linaweza kuibua manung’uniko ya upande mmoja wa Muungano.
Aliwataka Wana CCM na wadau wengine kuifanyia kazi kauli ya Rais Kikwete aliyokaririwa mara kuwa vyama visipojali masilahi ya taifa katika mchakato wa Katiba, Katiba mpya itakwama na Watanzania watalazimika kuendelea kutumia katiba ya sasa.
 Chanzo: Tanzania Daima

0 comments: