-Aagiza kukamilishwa kwa uundwaji wa mabaraza ya wafanyakazi katika utumishi wa umma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete juzi, Alhamisi, Aprili 17, 2014, alifanya mazungumzo na majadiliano ya kina na viongozi wa vyama vyote vya wafanyakazi nchini yenye nia ya kutafuta njia za kuboresha maslahi na ustawi wa wafanyakazi nchini.
Mazungumzo hayo ya muda mrefu yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam
yalihudhuriwa pia na Waziri wa Kazi na Ajira Mheshimiwa Gaudensia M.
Kabaka, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi) Mheshimiwa Celina
Kombani, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) Mheshimiwa Hawa
Ghasia, Waziri wa Fedha Mheshimiwa Saada Mkuya na Katibu Mkuu Kiongozi,
Balozi Ombeni Y. Sefue.
Aidha, mazungumzo hayo yalihudhuriwa na maofisa waandamizi wa
Serikali wakiwemo Makatibu Wakuu wa Wizara ambazo zinahusika moja kwa
moja na maslahi na ustawi wa wafanyakazi na uongozi wa vyama vya
wafanyakazi uliongozwa na uongozi wa juu wa Muungano wa Vyama vya
Wafanyakazi Tanzania - TUCTA.
Rais Kikwete na viongozi hao wa vyama vya wafanyakazi nchini kwa
zaidi ya saa 10 walijadili hali ya utekelezaji wa masuala na mambo
yaliyokubaliwa katika kikao chao cha namna hiyo kilichofanyika Februari
27, Mwaka jana wa 2013.
Vile vile, Rais Kikwete na viongozi hao wakiwemo wale wa Chama cha
Walimu Tanzania (CWT) walichambua kwa kina hoja za wafanyakazi
zilizowasilishwa kwa Rais Kikwete na vyama hivyo.
Hoja hizo zilijadiliwa katika kikao hicho. Miongoni mwa hoja hizo ni
ajira kwa wageni na athari zake kwa ajira ya Watanzania, athari za
kuzuka kwa mawakala wa ajira nchini, watumishi waandamizi wa Serikali
kushikilia nafasi za uongozi katika vyama vya wafanyakazi na athari
zake, ushirikishwaji wa wafanyakazi katika bodi za taasisi za umma na
Serikali na uhamisho wa maofisa kazi ambao Rais Kikwete aliuagiza miaka
mitatu iliyopita.
Hoja nyingine zilizojadiliwa ni hali ya afya ya wafanyakazi katika
migodi mbali mbali nchini, bei ya umeme majumbani na athari yake kwa
wafanyakazi, uwezekano wa kupunguza tena kodi kwenye mishahara ya
wafanyakazi jambo ambalo Serikali ililifanya Mwaka 2013, madai ya
malimbikizo ya mapato ya wafanyakazi, madeni ya walimu na uwezekano wa
nyongeza ya mishahara kwa walimu.
Katika kikao hicho, Rais Kikwete ameagiza wizara, idara na taasisi
zote za Serikali na umma ambazo hazijatekeleza hitaji la kisheria ya
kuundwa kwa mabaraza ya wafanyakazi katika utumishi wa umma kufanya
hivyo mara moja bila kuchelewa.
Rais Kikwete ametoa muda hadi Mei Mosi, mwaka huu, kwa wizara, idara
na taasisi hizo kuwa tayari zimeunda mabaraza hayo na amemwagiza Balozi
Sefue kutuma barua za maagizi hayo ya Rais kwa wizara, idara na taasisi
husika.Aidha, Rais amesema kuwa mwishoni mwa mwaka huu atapenda kupata
taarifa kuhusu hali ya uanzishwaji na utendaji wa mabaraza hayo ambayo
ni muhimu kwa uwakilishi wa wafanyakazi katika uendeshaji wa taasisi za
umma ambazo wanazifanyia kazi.
Rais Kikwete amekiambia kikao hicho: “Wafanyakazi lazima
washirikishwe kikamilifu katika uendeshaji wa taasisi wanazozifanyika
kazi na hasa katika vikao vyote vya bajeti za wizara, idara na taasisi
za umma ambako wameajiriwa.”
Imetolewa na;
Kurugenzi ya mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
19 Aprili, 2014
Kurugenzi ya mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
19 Aprili, 2014
0 comments:
Post a Comment