LATEST POSTS

Monday, May 12, 2014

DAKTARI BIGWA AFA KWA UGOJWA WA DENGEU


Waombolezaji wakimfariji Leticia Filbert, mke wa daktari bingwa wa Hospitali ya Temeke, marehemu Dk Gilbert Buberwa nyumbani kwake Kinyerezi, Dar es Salam jana. Picha na Salim Shao



Dar es Salaam. Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akili nchini, Gilbert Buberwa amefariki dunia kutokana na ugonjwa wa dengue.
Kifo cha Dk Buberwa kinafanya idadi ya watumishi wa afya waliofariki dunia kutokana na ugonjwa huo kufikia wawili baada ya muuguzi Hamida Likoti kufariki dunia wiki iliyopita.
Ugonjwa huo uliolipuka mkoani Dar es Salaam, umezua taharuki kwa wakazi wake kwa sababu hauna tiba na unasababishwa na mbu, Aedes Egyptae, anayeuma mchana na anayeweza kuzaliana katika majisafi yaliyotuama.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania(MAT), Dk Primus Saidia alisema jana kuwa Dk Buberwa alifariki dunia saa saba usiku wa kuamkia jana akiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Dk Buberwa alianza kuumwa ugonjwa huo akiwa kazini katika Hospitali ya Temeke na kulazwa na hali yake ilipobadilika, alihamishiwa MNH kwa matibabu zaidi
“Kadiri siku zilivyozidi kwenda alibainika kwamba viungo vyake muhimu, yaani ini na figo vimeharibika, hivyo alisafishwa figo huku akiwa amelezwa Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU).
Dk Saidia alikumbusha kuwa virusi vya dengue havina tiba isipokuwa dalili zake ambazo ni homa, kuumwa kichwa na viungo vya mwili – ndizo zenye tiba.
Dk Buberwa alianza kuugua Mei 3, mwaka huu na siku iliyofuata alipelekwa hospitali na mkewe ambako alilazwa ili kupata uangalizi wa karibu wa madaktari wenzake.
Kaka wa marehemu, Wakili Nickson Ludovick alisema: “Tunasubiri ndugu kutoka Bukoba na Musoma kwa mazishi yatakayofanyika hapa Dar es Salaam katika makaburi ya Kinyerezi keshokutwa.”
Madaktari, wauguzi walazwa
Dk Malima alisema hadi jana, wafanyakazi tisa wa Hospitali ya Temeke walikuwa wamelazwa kutokana na homa hiyo.
Alisema wafanyakazi hao ni madaktari watano, wauguzi watatu na mtaalamu mmoja wa maabara. “Kwa kipindi cha wiki mbili zilizopita tumepokea wagonjwa wa dengue waliothibitika 15,” alieleza Dk Malima.
Muuguzi wa zamu katika Hospitali ya Temeke, Shamim Kanju alisema wafanyakazi wanaendelea kuambukizwa kutokana na kuwa katika mazingira hatarishi kwa muda mrefu. Mtaalamu wa maabara, Eliud Kishebuka ambaye ni mmoja wa wagonjwa waliothibitika kuwa na homa hiyo, alisema alianza kujisikia mgonjwa juzi asubuhi, hivyo akaamua kwenda kufanya vipimo Mwananyamala ambavyo vilithibitisha kuwa ameambukizwa.
Utambuzi wa ugonjwa
Dk Saidia alisema wataalamu wa vipimo hawajaelekezwa ipasavyo namna ya kutambua mgonjwa huo.
Alisema endapo mgonjwa atachukuliwa kipimo kamili cha damu (full blood picture) na kuona kupungua kwa chembehai mgando nyeupe za damu, wajue kwamba hicho ni kiashiria kikuu cha ugonjwa wa dengue.
Mwandishi The Citizen augua,
Mwandishi wa Gazeti la The Citizen, Mkinga Mkinga ni miongoni mwa watu walioambukizwa ugonjwa huo
Mkinga alisema jana kwamba alianza kuhisi homa na maumivu makali ya kichwa tangu Jumanne iliyopita na alipokwenda hospitali ilibainika kuwa ni homa ya dengue.
“Nilipewa dawa za kutuliza pamoja na kunywa maji mengi, kwa sasa niko nyumbani kwangu ninaendelea nazo lakini kichwa bado kinauma na homa inakuwa kama ya vipindi,” alisema.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imesema wagonjwa wa dengue wameongezea na kufikia 399 hadi jana.
Ofisa mwandamizi wa wizara hiyo, Dk Janeth Bugamba alisema jana kuwa kuna uwezekano wa idadi ya wagonjwa kuwa kubwa zaidi kwa kuwa hakuwa amepata takwimu kutoka hospitali zote.
Msemaji wa MNH , Aminiel Aligaesha alisema wagonjwa wa dengue wanaongezeka kwa kasi katika hospitali hiyo.

Alisema hadi kufikia jana, wagonjwa 65 walifika katika hospitali hiyo na kutibiwa kisha kurejea nyumbani na wengi ni kutoka maeneo ya jirani na hospitali hiyo wakiwamo wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Muhimbili (Muhas) ambao hata hivyo, hakutaja idadi yao.
source mwanachi







.

0 comments: