Dodoma. Kiongozi wa Kambi Rasmi yaUpinzani Bungeni, Freeman Mbowe kwa siku ya pili jana alikuwa katika wakati mgumu kuunda baraza jipya kivuli la mawaziri.
Baraza hilo ambalo kwa mara ya kwanza litajumuisha wabunge kutoka vyama vya vingine vya upinzani vya NCCR-Mageuzi na CUF lilikuwa litangazwe jana. Baraza Kivuli lililokuwapo lilijumuisha wabunge wa Chadema pekee.
Habari za uhakika zilizopatikana jana zilisema kuwa juzi Mbowe na wasaidizi wake wa karibu alikuwa akiunda baraza lake hilo hadi saa 8:00 usiku wa kuamkia.
“Yuko kwenye hatua za mwisho kukamilisha Baraza hilo … jana (juzi) amefanya kazi hiyo hadi saa 8:00 usiku wa manane,” kilidokeza chanzo kimoja.
Baraza hilo jipya linaonekana kuvuta hisia za wabunge wengi wa CCM kutokana na baadhi yao kuligusia wakati wakichangia Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu
Miongoni mwa wanaotajwa kuingizwa katika baraza hilo ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila na Mbunge wa Mkanyageni kupitia CUF, Mohamed Habib Mnyaa.
Kuingizwa katika Baraza hilo kivuli kwa wabunge wa NCCR-Mageuzi na CUF ni matunda ya ushirikiano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ulioasisiwa wakati wa Bunge Maalumu la Katiba.
Umoja huo ndio uliowaongoza wajumbe karibu 200 wa Bunge Maalumu la Katiba kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba.
Alipoulizwa kuhusu ahadi yake ya kutangaza baraza hilo jana, Mbowe alisema ameahirisha na sasa atalitangaza leo.
“Nafahamu wabunge na wananchi wana shauku ya kufahamu watakaoingia katika baraza kivuli lakini naomba niseme sitalitangaza leo kama nilivyoahidi,” alisema.
0 comments:
Post a Comment