LATEST POSTS

Tuesday, September 9, 2014

MTOTO ATEKWA, ABAKWA, ATOBOLEWA MACHO


MTOTO Happiness Kashinje (9) (pichani)aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Negezi mjini Shinyanga, ameokotwa akiwa amekufa baada ya kudaiwa kutekwa na watu wasiojulikana kabla ya kubakwa na kutobolewa macho.
Mtoto Happiness Kashinje (9) pichani kulia enzi za uhai wake.

Tukio hilo lilijiri hivi karibuni Nhelegani, Kata ya Kizumbi kilometa chache kutoka nyumbani kwao.
Habari zilizofika Uwazi kuhusu mkasa huo zinasema, Happiness aliyekuwa akiishi na shangazi yake, alipotea Agosti 27, mwaka huu baada ya kuaga kuwa anakwenda saluni kupunguza nywele na hakurudi tena hadi  siku iliyofuata mwili wake ulipookotwa ukiwa umeanza kuharibika.
Tukio hilo la kinyama lilmegusa hisia za wakazi wengi wa Manispaa ya Shinyanga hasa ikizingatiwa kuwa mwishoni mwa mwaka jana, muuza urembo mmoja alikamatwa kwa tuhuma za kuwabaka na kuwatoboa macho wanafunzi wanne wa shule za msingi za Manispaa ya Shinyanga. Mtuhumiwa huyo alihukumiwa kifungo cha maisha jela.
Baadhi ya watoto walioathirika katika matukio ya ubakaji uliofanyika katika maeneo tofauti ya Mji wa Shinyanga walilazwa kwa muda mrefu katika hospitali ya mkoa na wengine kupelekwa Bugando jijini Mwanza lakini hata hivyo, baadhi yao macho yao yameathirika.
Kwa mujibu wa maelezo ya mlezi wa mtoto Happiness, John Njai ambaye ni mume wa shangazi yake, siku moja kabla ya tukio, marehemu aliomba shilingi mia tano kwa ajili ya kunyolea nywele.
Baada ya kupewa hela hiyo inadaiwa bibi yake alimtaka anyoe nywele hizo nyumbani ili fedha hiyo itumike kwa matumizi mengine, lakini alikataa kwa madai kuwa angenyolewa vibaya na hivyo kuchekwa na wenzake shuleni.
Bibi huyo alimruhusu mjukuu wake kwenda saluni na kwamba akiwa njiani anarudi aliomba lifti kwa watu wawili waliokuwa kwenye baiskeli moja lakini walimnyima kwa madai ya kukosa kiti cha nyuma.
Baada ya kuchelewa kurudi nyumbani, wazazi na walezi walipata wasiwasi hivyo kuanza kumfuatilia kwa ndugu na majirani, lakini hawakufanikiwa licha ya kutoa tangazo msikitini juu ya kupotea kwa binti huyo.
Pia walitoa taarifa kwa mwenyekiti wa mtaa, Kituo cha Polisi cha Nkomo na kwa ndugu na jamaa wanaowafahamu na hatimaye Agosti 28, mwaka huu, mtu mmoja alisema mwili wa mtoto wa kike anayekadiriwa kuwa na miaka tisa au kumi umeokotwa katika Kijiji cha Nhelegani ukiwa umeharibika.
Polisi waliuchukua mwili huo kwa ajili ya uchunguzi, baadaye waliruhusu mazishi yake huku hofu na simanzi zikiwa dhahiri kwenye nyuso za ndugu, jamaa na marafiki. Hapiness alizikwa katika makaburi ya familia yaliyoko kijijini Negezi.

0 comments: