Tanga. Rais Jakaya Kikwete amewataka viongozi
wa dini nchini kuwahimiza waumini wao kuwachagua wanasiasa wasiokuwa
waovu, wasiofanana na uovu au hata kuukaribia.
Amewataka kuepuka makundi ya kisiasa na wasiwape
mwanya wanasiasa wenye dhamira ovu katika kutafuta madaraka kwa thamani
yoyote na wawakemee wale wanaotaka kupata madaraka kwa gharama yoyote.
Alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa
maadhimisho ya miaka 125 tangu kuingia kwa injili katika ukanda wa Pwani
ya Tanga na Milima ya Usambara uliofanyika katika Viwanja vya
Mbuyukenda jijini hapa.
“Wanasiasa wanaotaka madaraka kwa njia yoyote ile,
muwanyanyapae, wakatalieni kwa macho makavu, hawa si watu wema
watatufikisha pabaya,” alisema Rais Kikwete.
Alisema hayo baada ya Askofu wa Kanisa la Kiinjili
la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk Stephen Munga
kumweleza kwamba akiwa mkuu wa nchi anao wajibu wa kuhakikisha Taifa
linavuka kwa amani na usalama katika kipindi hiki kigumu cha uchaguzi.
Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM,
alisema katika kipindi hiki, viongozi wa madhehebu ya dini wasijiingize
katika makundi ya wanasiasa kwa sababu mambo yakiharibika itakuwa hakuna
pa kukimbilia.
Aliwataka viongozi wa dini watumie nyumba za ibada
kuliombea Taifa livuke salama katika kipindi hiki kigumu badala ya
kuwapangia vyama au viongozi wa kuwachagua.
“Tunawategemea kuwahimiza na kuwakumbusha kutumia
haki na wajibu wao vizuri, muwahimize na kuwakumbusha kuwa watatakiwa
kufanya mambo matatu muhimu; Kwanza, kujiandikisha, pili, kujitokeza
kwenda kupiga kura na tatu kuchagua viongozi wazuri, wasiokuwa waovu,
wasiofanana na uovu na kuukaribia uovu, watakaosukuma mbele gurudumu la
maendeleo na kujali masilahi mapana ya jamii husika na nchi yetu.”
“Viongozi wa dini muwe kama mimi, nina wagombea wa
urais 42, kama nitaonyesha kuwa upande wa mgombea yeyote kati yao, basi
nitakuwa nimeharibu mchakato mzima wa uchaguzi.
“Tusiwape mwanya wanasiasa wenye dhamira ovu
kuwafarakanisha Watanzania. Tuendelee kukemea matumizi mabaya ya fedha,
rushwa, hila, ghiliba na hujuma katika uchaguzi. Tunapaswa kufanya hivyo
tena zaidi sasa, wakati wa michakato ya ndani ya vyama vya siasa na
baadaye wakati wa uchaguzi,” alisema.
Alisema hiki ni kipindi nyeti na kwamba, viongozi
wa dini pamoja na Watanzania kwa ujumla wanapaswa kufahamu kuwa Tanzania
haina kinga ya milele ya amani na utulivu, kama itavurugwa haitakuwa
lulu ya Afrika tena kama ilivyo sifa yake.
“Tuwakemee wanasiasa wapenda madaraka kwa gharama
yoyote, ambao watataka kutumia fedha kununua ushindi au ubaguzi wa
rangi, kabila, dini na kadhalika, kuwabagua wapinzani wao na kujijenga
kisiasa. Nawaomba msiwasikilize wala kuwaendekeza kwani mchezo wao ni
mauti yetu. Wakatalieni kwa macho makavu na kwa kweli muwanyanyapae,”
alisema.
Rais Kikwete ambaye wiki hii atakuwa na kibarua cha kuongoza
vikao vya kuwachuja wagombea kupitia CCM, alisema hawapaswi kukaa kimya
dhidi ya watu wanaokiuka maadili na kuchochea mifarakano katika Taifa.
“Hawa si watu wema, watatufikisha pabaya.
Hawaitakii mema nchi yetu. Kamwe tusiruhusu wachezee dini zetu ambazo ni
mhimili muhimu sana wa amani yetu,” alisema.
Alisema tofauti na ukabila ambao pamoja na ubaya wake, unaweza kuhusisha eneo dogo, dini zinahusisha nchi nzima.
“Hakuna mtu, dini wala eneo litakalonusurika.
Tutapoteza ile sifa yetu ya kihistoria ya kuwa lulu na mfano wa amani
katika Afrika. Tusikubali kumchukiza Mungu akatukasirikia na kutuadhibu
kwa jambo ambalo liko ndani ya uwezo wetu kulizuia lisitokee. Kwa kweli
mambo yakiharibika, hatuwezi kumlaumu mtu mwingine yeyote, bali sisi
wenyewe. Katu hatuwezi kusema ni mapenzi ya Mungu, bali itakuwa ni
makosa yetu wenyewe.”
Aliwaomba viongozi wa dini: “Limeni mraba wenu
vizuri nasi tulime wetu. Msiwape nafasi viongozi wa siasa na hata wa
dini kutumia majukwaa ya dini kuendeleza masilahi yao ya kisiasa na hasa
kupandikiza chuki katika jamii. Msiwe sehemu ya makundi ya wagombea au
vyama vya siasa. Mnatakiwa msiwe na upande, muwe juu ya pande zote. Hapo
ndipo mtakapofanya vizuri kazi yenu ya ulezi na kuponya Taifa iwapo
kutatokea matatizo.”
Kauli ya askofu
Askofu Munga mbali na kueleza historia ya kuingia
kwa injili katika eneo la Pwani ya Tanga na Milima ya Usambara, alisema
kanisa hilo litaliombea Taifa livuke salama katika Uchaguzi Mkuu...
“Tunakuahidi kukuombea wewe na nchi ivuke kwa amani na salama. Wewe kama
mkuu wa nchi una mzigo mzito wa kuhakikisha unatuvusha vyema.”
Alisema kilele cha maadhimisho ya miaka 125 ya
kuingia kwa Injili kitakuwa Julai 12, mwaka huu katika Kanisa la Makao
Makuu ya Dayosisi mjini Lushoto na zaidi ya vijana 125 watatembea
kuanzia Tanga hadi Lushoto kwa kupita njia ambazo Wamisionari walipitia
kwa miguu wakati wakieneza injili.
Alisema katika kipindi cha miaka 125, KKKT
Dayosisi ya Kaskazini Mashariki imeendesha huduma nyingi za kuisaidia
jamii ikiwa ni wajibu wake wa kutobagua kwa itikadi za kidini wala
rangi.
0 comments:
Post a Comment