LATEST POSTS

Tuesday, December 17, 2013

DK. SLAA AIBUA UFISADI CHC




Dk. Willibrod Slaa
 
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amedai kupata nyaraka za siri zinazobainisha ufisadi ulioko nyuma ya mashirika yaliyobinafsishwa chini ya Shirika Hodhi la Serikali (CHC).
Amesema nyaraka alizonazo ambazo serikali ya CCM inakusudia kuzifanya kuwa za siri zimechambua namna Tanzania inavyopata hasara kutokana na ubinafsishaji holela uliofanywa kwa mali za Umma.
Dk. Slaa alitoa kauli hiyo jana mjini Urambo wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Urambo Square.
Alisema mengi ya mashirika hayo ni yale yaliyoanzishwa wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere kwa ajili ya kuwasaidia wananchi.
Alitaja baadhi ya mashirika hayo kuwea ni pamoja na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), ambayo alisema serikali inamiliki asilimia 30 ya hisa pasipo wananchi kuambiwa.
Aliongeza kuwa NBC ni moja ya mashirika ya umma yaliyobinafsishwa kiholela kwa kwa thamani ya sh bilioni 15 zilizokuwa mali kauli.
Alisema nyaraka hiyo amewatumia wabunge wa chama chake na kuwaagiza waihoji serikali bungeni ili iwajibike kwa wananchi kueleza kwa nini rasilimali zao zinafujwa na viongozi wanaotakiwa kubeba dhamana ya kuongoza nchi.
“Mikononi mwangu hapa ninazo nyaraka ambazo wao wanataka ziwe za siri, wakati inahusisha ufisadi mkubwa wa rasilimali za Watanzania.
“Wananchi wenzangu mtakumbuka kuwa Mwalimu Nyerere, alianzisha mashirika ya umma yapatayo 435, ambayo moja ya madhumuni ilikuwa ni kuzalisha ajira kwa vijana wetu,” alisema Dk. Slaa.
Aliongeza kuwa madhumuni ya Mwalimu katika mashirika hayo ilikuwa fedha zinazopatikana kutokana na uendeshwaji wa mashirika hayo zitumike katika kuboresha huduma muhimu kama afya na elimu kwa kujenga zahanati, hospitali na shule za ngazi mbalimbali katika ubora unaostahili.
Dk . Slaa anaendelea na ziara mkoani Tabora kwa kufanya mikutano mbali mbali na leo atakuwa jimbo la Tabora mjini.
CHANZO: Tanzania Daima

0 comments: