ZAIDI
ya familia 30 za wakazi wa kijiji cha Kasense nje kidogo ya Manispaa ya
Sumbawanga, wamekosa pahala kuishi baada ya nyumba zao kubomolewa na
nyingine kuezuliwa mapaa kutokana na mvua kubwa iliyoambatana na upepo
kunyesha.
Mvua hiyo iliyonyesha juzi kuanzia saa 9 alasiri na ilidumu kwa saa
mbili huku upepo huo ukiangusha miti na kuwatia hofu wakazi wa kijiji
hicho.
Diwani wa Kasense, Cretus Jumbe, alisema mvua hiyo pia iliharibu
madarasa matatu na nyumba mbili za walimu katika shule ya Msingi Kasense
ambazo nazo ziliangukiwa na miti kwenye mapaa yake.
Jumbe alisema hadi sasa kuna takriban nyumba 32 zilizopata madhara
hayo ambapo familia zote zimehifadhiwa kwa ndugu na jamaa zao wakisubiri
msaada zaidi toka serikalini.
Mkururugezni wa Manispaa ya Sumbawanga, William Shimwela, ambaye
alifika eneo hilo muda mfupi baada ya maafa hayo, alisema timu ya
wataalamu inatarajiwa kufika leo kufanya tathmini ya maafa na kuangalia
ni msaada upi wa haraka unatakiwa.
“Tutakaa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ambaye ni Mkuu wa wilaya
ili kuona hatua zingine zinazofuata kwani tayari tumejionea hali halisi
ya wananchi walivyoathirika kutokana na tukio hilo na wanahitaji msaada
wa haraka kwa sababu hawana sehemu za kuishi,” alisema Shimwela.
Alisema madarasa yaliyoharibika yanahitaji ukarabati kabla ya Januari mwakani, ili wanafunzi waweze kuendelea na masomo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment