NAIBU Waziri wa Katiba na Sheria, Angellah Kairuki, amesema kuanzia
mwakani kesi zitakazohusiana na ukatili wa kijinsia, mashauri yake
yatasikilizwa ndani ya miezi mitatu hadi kutolewa hukumu.
Kairuki alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati wa
uzinduzi wa kijitabu cha mwongozo wa kuwasaidia wanawake waliofanyiwa
ukatili kilichoandaliwa na Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake na
Watoto (WLAC).
Alisema ili kuhakikisha hilo linafanikiwa kutakuwa na vikao maalumu
katika mahakama zinazoendesha kesi hizo, hatua ambayo alisema imeafikiwa
na nchi zote za Maziwa Makuu.
“Ni kweli kumekuwepo na ucheleweshaji wa kesi hizi, hali inayowafanya
walalamikaji kuachana na kesi hizo kwa kuona kuwa wanapotezewa muda
wao, ndio maana kwa pamoja nchi hizo ziliamua kuja na azimio moja, ili
kuona watuhumiwa wa makosa haya wanashughulikiwa mara moja,” alisema.
Pamoja na mikakati hiyo, Kairuki alitoa wito kwa asasi
zinazoshughulika na masuala ya kuwatetea kinamama na watoto
kushirikiana na viongozi wa dini ambao wataweza kuwahubiria waumini wao
umuhimu wa kuishi kwa amani na katafuta suluhu ya matatizo kwa amani.
Mwenyekiti wa WLAC, Nakazael Tenga, alisema wakati takwimu za utafiti
wa afya Tanzania ya mwaka 2010 zikionyesha asililimia 39 ya wanawake
wote Tanzania wameathirika kwa namna moja au nyingine na ukatili wa
kimwili tangu wakiwa watoto, mkoa wa Dodoma umeonekana kuongoza kwa
vitendo hivyo kwa asilimia 70.
Mkoa wa Mara ambao awali ulikuwa ukiongoza sasa hivi vitendo
vimepungua na kufikia asilimia 66.4, Ruvuma (50.8) na Morogoro (50.1),
takwimu ambazo Tenga alisema haziridhishi kwani karibu kila mkoa nchini
unakabiliwa na titizo hilo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa WLAC, Theodosia Muhulo, alisema ipo haja
ya kuanzishwa mahakama ya familia ambayo itakuwa ikishughulikia kesi
zote zinazohusiana na migogoro ndani ya familia.
CHANZO: TANZANIA DAIMA
0 comments:
Post a Comment