LATEST POSTS

Monday, December 2, 2013

TUSIADHIMISHE SIKU BALI TUDHAMIRIE KUUTOKOMEZA UKIMWI

Kila Disemba Mosi ni siku ya Ukimwi Duniani ambapo watu kwenye maeneo mbalimbali hukutana kwa lengo la kupeana elimu ya kujikinga na kupiga vita ugonjwa wa UKIMWI. Siku hii iliasisiwa na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) mwaka 1998 na inaendelea kuadhimishwa kila Desemba mosi kwa uratibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Ukimwi (UNAIDS).
Tanzania ni miongoni mwa mataifa yanayoadhimisha siku hiyo, ambapo Rais Jakaya Kikwete atawaongoza wananchi wake, hususan wakazi wa Dar es Salaam ambako Siku ya Ukimwi Duniani inaadhimishwa kitaifa.
Maadhimisho hayo yalianza Novemba 25 kwa wadau wa ukimwi kufanya maonyesho ya shughuli za wadau kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini humo.
Hapa Tanzania maadhimisho ya siku hiyo yanabebwa na kaulimbiu ya ‘Tanzania bila maambukizi mapya ya VVU; vifo vitokanavyo na ukimwi na unyanyapaa inawezekana.’
Tunaungana na watu wote duniani wanaoadhimisha siku hii kwa kukumbuka ndugu, jamaa, marafiki, wazazi na wenza wetu waliotangulia mbele ya haki kutokana na ugonjwa huu.
Ni wazi kwamba ukimwi ni janga la dunia hususani kwa nchi zinazoendelea Tanzania ikiwemo, kila familia hapa nchini kwa namna moja ama nyingine inalo kovu linalotokana na ukimwi.
Yamefanyika makongamano mengi makubwa na madogo yanayoelezea jinsi ya kujikinga na maambukizi mapya ya VVU, kutowaambukiza wengine, kuishi kwa matumaini na kutowanyanyapaa walioathirika.
Hivi sasa taifa lipo kwenye mkakati wa kudhibiti ukimwi kwa kufikia azima ya sifuri tatu, yaani maambukizi mapya sifuri, vifo sifuri na unyanyapaa sifuri ifikapo mwaka 2015.
Mkakati huo unahimiza utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) na maazimio yaliyowekwa kwenye mkutano maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ukimwi uliofanyika mwaka 2001 nchini Marekani.
Tunakumbuka pia mwaka 2007 Rais Kikwete alianzisha kampeni ya kupima kwa hiari VVU ili kubaini walioathirika, ambapo yeye na mkewe walipima kwanza.
Ni kampeni iliyoleta hamasa kwa kiasi kikubwa na kupunguza kasi ya unyanyapaa uliokithiri katika jamii, hali iliyoharakisha vifo kwa wapendwa wetu huku wengine wakihofia kupima, kwa sababu dawa hazikuwepo.
Hivi sasa tunaweza kusema kasi ya maambukizi mapya imepungua baada ya wananchi kupata elimu sahihi ya kujikinga na kutumia dawa za kufifisha makali ya ugonjwa huo ikiwemo kupungua sana kasi ya unyanyapaa.
Tanzania Daima Jumapili tunawahimiza Watanzania wote kushirikiana katika kutokomeza maambukizi mapya ya VVU ili kuwa na taifa salama. Ni kweli tukiamua tunaweza kuufanya ugonjwa wa ukimwi kuwa historia.

0 comments: