Kwa kuwa waandishi wengi wamesoma katika vyuo mbalimbali vya uandishi wa habari, imeonekana kuwa kuna haja ya kuwa na mwongozo wa uandishi bora na aina za mitindo inayotumika na kukubalika.
Mwongozo huu umejikita katika matumizi fasaha na sanifu ya lugha ya Kiswahili ambayo ndiyo msingi katika uandishi wa habari.
Ifahamike kuwa kila kampuni ya uchapishaji wa magazeti au vitabu na kampuni za televisheni na redio huwa na mtindo wao wa kuandika au kutangaza habari ambao ni tofauti kidogo na vyombo vingine katika matumizi ya lugha ya Kiswahili. Hata hivyo ziko mbinu ambazo ni za jumla kwa kila mwandishi ambazo hana budi kuzifuata kama kwa mfano matumizi ya tahajia ya maneno, miundo ya sentensi na mpangilio wa maneno. Tofauti zinazojitokeza ambazo hutumiwa na wachapishaji ama wa magazeti au wa vitabu zinazojulikana kama ‘House style’ ni ndogo na haziwezi kuathiri sana uandishi kwa jumla.
Maelezo yafuatayo yametokana na utafiti pamoja na ushauriano baina ya wataalamu wa lugha.
Maelezo
Msingi wa maelezo yaliyoandikwa umezingatia miongozo iliyowahi kutolewa na Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) siku za nyuma kama ilivyoandikwa katika machapisho yao kama kitabu cha “Jifunze Kiswahili Uwafunze Wengine,’ pamoja na ‘Mwongozo wa Uandishi’.
Kwa kuanzia ningependa kufafanua baadhi ya maneno yanayokanganya kiasi fulani wasomaji wengi kutokana na kushindwa kuyapambanua. Sababu kubwa ya mkanganyiko huu ni athari ya lugha za asili katika Kiswahili sanifu pia ni misingi mibovu wa sarufi ya Kiswahili inayosababishwa na walimu wa shule za msingi wasiokuwa na ujuzi wa kutosha katika taaluma katika fani ya Fonolojia, Fonetiki, Mofolojia, Semantiki na Sintaksia. Pia wako wale wanaoathiriwa na lugha za kigeni kama Kiarabu na Kiingereza. Lugha hizi za kigeni kimetufanya tuione lugha ya Kiswahili kama chotara wa lugha nyingine wakati lugha hii ina misingi ya lugha ya Kibantu. Nitaanza kufafanua baadhi ya maneno nna vifungu vya maneno kwa utaratibu wa kutumia alfabeti. Kwa mfano:
A
Ajali/ajari:
Ajali ni tukio lenye madhara yanayotokea ghafla.
Ajari ni malipo kwa kazi ya ziada na jina linalofahamika ni ovataimu ambalo limetoholewa kutoka katika neno la Kiingereza la ‘overtime’.
Aidha/au /ama:
Neno aidha asili yake ni Kiarabu na tangu likopwe, matumizi yake hayajabadilika. Kuna wakati tunalitumia kama waaidha. Watumiaji wengi wanafuata mtindo wa Kiingereza wa ‘either ... or’. Tunasoma kwa mfano: “Wataalamu wa Kichina watabaki aidha bara au visiwani. Matumizi sahihi ni “Wataalamu wa Kichina watabaki ama bara au visiwani.
Maana ya aidha ni tena, basi, zaidi ya hayo, vilevile. Kwa mfano:
Kabla ya kwenda sokoni nitapitia aidha benki kuchukua fedha.
Ahirisha/hairisha:
Neno sahihi ni ahirisha.
Kuahirisha maana yake ni kuchelewesha jambo kwa makusudi ili lifanyike baadaye.
Adhima/azma:
Neno adhima si neno sahihi la Kiswahili ila liko neno adhimisha ambalo maana yake ni kufanya sherehe ya kukumbuka kwa tukio fulani kama vile siku ya kuzaliwa, siku ya kufunga ndoa, siku ya kupata uhuru, n.k.
Neno lingine linalofafana na hilo ni adhimu ( kiv) –enye sifa, iliyotukuka, tukufu, jalili.
Azma ni jambo linalokusudiwa kufanywa, makusudio au lengo. Wakati mwingine huandikwa kama azima.
Alimradi/ilimradi:
Haya ni maneno yenye maana moja. Maana yake ni ili, iwapo, kwa masharti kwamba, mradi.
Aidha:
Maana ya aidha ni vilevile, pamoja na hayo, pia, isitoshe n.k. Kuna wakati tunachanganya aidha na au katika sentensi moja. Hii inatokana na athari ya Kiingereza ya kutumia ‘either … or’... Kwa usahihi inatakiwa iwe ‘ama / au’ tunapotaka kulinganisha mambo.
B
Budi:
Neno hili likisimama peke yake lina maana ya hiari. Tukisema ,”Wakulima ni budi walime” tuna maana kuwa wakulima ni hiari walime.Tunatakiwa kusema “Wakulima ni lazima walime au wakulima hawana budi kulima. Kwa usahihi tunasema “Wakulima hawana budi kulima” (yako maneno yanayofanana kimuundo kama sina budi, hatuna budi, hawana budi , huna budi)
Baadaye/baadae :
Neno sahihi ni baadaye
D
Digiti/Digitali:
Digiti ni nomino na limetoholewa kutoka kwa neno ‘digit’ lenye maana ya tarakimu. Neno hili ni nomino na ni sahihi. Digitali ni kisifa (adjective). Kwa kawaida tunatohoa nomino na wala siyo kisifa. Hivyo neno sahihi ni ‘digiti”.
Durusu/rudufu:
Haya ni maneno yanayochanganywa na yana maana tofauti. Kudurusu ni kupitia tena maandishi yaliyoandikwa kwa madhumuni ya kusahihishwa au kuboreshwa na kutoa toleo jipya.
Rudufu ni kufanya nakala, kufanya kitu madhubuti k.v kurudufu nyuzi kuwa imara.
Darubuni:
Ni chombo cha kuonea mbali; kionea mbali yaani ‘Telescope/binoculars’.
Dahili/sajili: Maana ya kudahili ni kutaka kujua habari za watu kwa kuulizauliza au kudadisi. Kusajili ni kuweka orodha ya kmbukumbu za vitu au watu kwa kuviandika katika daftari maalumu.
F
Fedha/pesa/hela:
Haya ni maneno yenye maana moja lakini yana asili tofauti. Maneno mengine yanayofanana na hayo ni sarafu, fulusi, faranga ambayo hutumika katika malipo. Maneno yote yanakubalika. Hata hivyo tuna mazoea ya kutumia neno fedha upande wa bara na pesa upande wa visiwani.
Fikiri /dhani.
Maneno haya yanafanana kwa kiwango fulani lakini wengi wetu huyachanganya na kuyatumia kama visawe. Yana tofautiana kidogo. Fikiri ni kutumia ubongo kutatua jambo, kutafakari, kuwaza. Kudhani ni kufikiri bila kuwa na uhakika.
G
Ghairi-
Kuacha kutenda kilichokusudiwa.
Ghushi/gushi:
Neno sahihi ni ghushi
H
Hadubini:
Ni chombo cha kuona vitu visivyoonekana kwa macho (Microscope).
Hoteli/mahoteli :
Neno sahihi ni hoteli.
Hovyo/ovyo:
Neno sahihi ni ovyo
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment