LATEST POSTS

Friday, April 17, 2015

Mbinu za uandishi bora (Sehemu ya pili)

Hadhari/Tahadhari:
Hadhari ni nomino na tahadhari ni kitenzi. Hadhari ni uangalifu. Hadhari kabla ya athari/hatari. Tahadhari ni kitenzi. Kuepuka jambo ili usipatikane na hatari au ubaya.
Hatima/ hatma:
Neno sahihi ni hatima
Harusi/arusi :
Maneno yote mawili yanatumika ila kwa mazoea ya wengi neno harusi ndilo linalotumika zaidi.
I
Idadi/nambari:
Idadi ni jumla ya vitu au mambo yanayohesabika. Nambari limetokana na neno namba (number) yana maana ya tarakimu kama 1, 2, 3, 4, 5.
Idadi ni namba au hesabu ya kujumuisha.Tunasema idadi kubwa ya Watanaznia ni wakulima.
J
Jingine/Lingine:
Yote ni  sahihi ila hutegemea muktadha husika.
Jinsi na jinsia.
 Jinsi ni namna kitu kilivyo au kiumbe kama vile binadamu, wanyama au ndege. Tunayo jinsi ya kike na jinsi ya kiume. Kwa lugha ya kigeni ni ‘sex’.ku
Jinsia  ni hali ya kuwa mume au mke. Masuala yanayohusiana  na mwanamume na mwanamke. Kwa lugha ya kigeni ni ‘gender’.
K
Kuwapo /Kuwepo:
Neno linalosadifu ni kuwapo ijapokuwa kwa mazoea watu wengi wanatumia kuwepo.
Kiwanda/Karakana :
Kiwanda  ni mahali penye sehemu za kuundia vitu mbalimbali  kama milango, vioo, madirisha, magurudumu, n.k. Sehemu hizi hufahamika kama karakana. Hivyo kiwanda huwa ni mkusanyiko wa karakana mbalimbali.
Kampuni/Makampuni:
Neno sahihi ni  kampuni na   wala siyo makampuni.
Kurudufu: Maana yake ni kunakili  au kutoa nakala nyingine.
Kimbiza /Wahisha:
Kukimbiza ni kufuata kitu au mtu kwa mbio nyuma  au kufukuza. Kuwahisha ni kutenda jambo  mapema kabla halijaharibika. Waandishi wanatumia ‘kukimbiza badala ya kuwahisha.                               
Kuongea/kuzunguma:
Tofauti kati ya maneno haya ni ndogo sana. Kuongea ni kushiriki katika mazungumzo. Kuzungumza ni kusema maneno katika mkutano au kwenye mjadala au baraza na kutoa maoni.
Kupeleka  ni kuchukua kitu au mtu na kukifikisha/kumfikisha mahala fulani. Tukiongeza kiambishi cha –ea tunapata kupelekea kwa maana ya kufikisha kitu kwa niaba ya…Mtoto alimpelekea mzazi wake mbegu shambani. Hivi sasa matumizi ya pelekea yanaleta kichefuchefu kwa Waswahili.
Kuyeyuka/kuyayuka:
Neno sahihi ni yeyuka kwa maana ya kugeuka kwa kitu kigumu kuwa kioevu.
Kunyauka/kukauka:
Kunyauka ni kufifia kwa sababu ya ukame au joto. Kukauka ni kutoka maji na kuwa kavu
Kengeuka:
Kwenda kombo, angamia. Kengeua ni kumfanya mtu afuate njia mbaya au tabia mbaya, kupotosha.
Kutokana/Kufuatia: Maneno haya mawili yanatumika kama vile yana maana moja. Kwa kweli yana maana tofauti kabisa. Kwa mfano tunasema,” Kutokana na njaa kali inayowakabili wananchi wa Bariadi, serikali imepeleka magunia 20,000 ya mahindi. Ni makosa kusema, “ Kufuatia njaa kali inayowakabili wananchi wa Bariadi, serikali imepeleka magunia 20,000 ya mahindi.
Kugharamia/kugharimia:
Neno sahihi ni kugharimia badala ya kugaramia. Gharama ni nomino.
Kwa ujumla/kwa jumla:
Maneno yote yanatumika kutegemeana na maudhui.Tunasema  kwa jumla maisha ni magumu. Hata hivyo neno linatumika kama: Kwa ujumla wake mvua imekithiri. Ni makosa kutumia, ‘Kwa ujumla tumefanikiwa…bali kwa jumla tumefanikiwa.’
Chanzo: Mwananchi

0 comments: