Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Hamis Kigwangalla akichangia jambo bungeni siku za hivi karibuni mjini Dodoma. Picha na Maktaba
Dar es Salaam. Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Hamis Kigwangalla yuko hatarini kuvuliwa uanachama wa chama hicho, hatua ambayo endapo itachukuliwa itasababisha apoteze nafasi yake ya ubunge.
Uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya
Nzega mkoani Tabora tayari umemjadili Dk Kigwangalla katika vikao vyake
vya Kamati za Usalama na Maadili na Kamati ya Siasa, kuhusu kile
kinachodaiwa kuwa ni utovu wa nidhamu wa mbunge huyo.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana jioni
zinasema baada ya vikao hivyo vilivyofanyika Januari 11 mwaka huu,
imeazimiwa kuwa suala la Dk Kigwangalla pamoja na madiwani watano
wilayani humo lipelekwe katika ngazi ya CCM mkoa na baadaye taifa.
Dk Kigwangalla jana alipotafutwa kuzungumzia suala
hilo alisema: “Hata mimi nimesikia taarifa hizo, isipokuwa sijapewa
taarifa rasmi. Ila nafahamu kwamba vikao vya chama vilikuwepo na mimi
niliitwa ila kama ambavyo nimeshasema siwezi kuhudhuria”.
Gazeti hili lilimtafuta Mbunge huyo machachari
kutokana na taarifa yake aliyoitoa kwenye mitandao ya Facebook na
Tweeter akieleza kuhusu taarifa za kuwapo mpango wa kumfukuza uanachama.
Kupitia mitandao hiyo Dk Kigangwalla aliandika:
“Nimepokea taarifa kuwa madiwani walioungana na wananchi wa Nzega pamoja
na mimi kupinga uamuzi wa Baraza la Madiwani kuzigawa pesa kwenye Kata
wameadhibiwa na Kamati ya Siasa ya Chama Wilaya ya Nzega, bila
kusikilizwa na ilhali miongoni mwa ‘mahakimu’ hawa ni watu waliokuwa
wakilalamikiwa na madiwani na wananchi. “
Mbunge huyo aliongeza: “Nimepewa taarifa kuwa
mapendekezo ya adhabu dhidi yangu kutoka wilayani kwenda vikao vya juu,
...tena bila kusikilizwa maana nilitoa udhuru, ni kuwa ninyang’anywe
kadi ya uanachama wa CCM. Nimeshangazwa sana na kusikitishwa na jinsi
chama kinavyoendeshwa Nzega.”
Mbunge huyo alisema anaamini viongozi wakuu wa CCM
wanafuatilia kwa karibu suala hilo na watachukua hatua stahiki, huku
akisema hatahudhuria tena kikao chochote cha CCM wilayani humo.
“Kama chama hiki kimefika huku, kwamba kuna watu
wana nguvu kuliko chama, kwamba wachache wanaweza kuwaonea wengine kwa
kuwa wana vyeo na mamlaka ya kufanya hivyo na hakuna wa kuingilia kati
na kusema ‘no’, basi sina haja ya kuendelea kupambana,” aliongeza.
Aliendelea: “Nimechoka, sintokata rufaa wala
sintolalamika tena. Watekeleze hukumu hiyo. Sintojitetea na
sintohudhuria kikao chochote kile kuanzia sasa, nimechoka kupambana na
watu wenye nguvu, nimechoka. Ni bora kuwa mnyonge, lakini ukabaki na
uhai, uzima, heshima na furaha yako”.
Kauli ya CCM Nzega
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nzega, Amos Kanuda
alikiri Dk Kigwangwalla kujadiliwa katika vikao vya chama vya wilaya,
ikiwamo Kamati ya Siasa.
Chanzo: Mwananchi
Alisema makosa ya Mbunge huyo ambayo yalijadiliwa katika kikao
hicho ni kufanya mkutano wa hadhara na kuwaporomoshea matusi madiwani
wenzake ambao hawakuwa upande wake wakati wakijadili mgawo wa fedha.
Mwenyekiti huyo alisema CCM baada ya kuona mgogoro
huo wa madiwani wake unakua, kiliamua kuwajadili watuhumiwa na kwamba
uamuzi wa kikao hicho ni siri.
Alisema CCM bado inaendelea kumjadili mbunge huyo na kwamba kikao kingine kitafanyika Februari mosi mwaka huu.
Alisema uamuzi wa kikao hicho utapelekwa CCM Mkoa wa Tabora na wao watalijadili na kupeleka mapendekezo yao chama taifa.
Chimbuko la mgogoro
Mgogoro uliokigawa CCM katika Wilaya ya Nzega,
unatokana na tofauti za kimtazamo kuhusu jinsi ya kutumia fedha Sh2.3
bilioni zilizotolewa na Kampuni ya Uchimbaji wa Madini ya Resolute kama
kodi ya huduma kwa halmashauri ya wilaya hiyo.
Dk Kigwangalla pamoja na madiwani kadhaa wanapinga
kupindishwa kwa azimio la Baraza la Madiwani ambalo lilielekeza fedha
hizo zitumike kuanzisha Benki ya Jamii ya Nzega (Nzega Community Bank
Ltd - NCB) na Kampuni ya Ujenzi ya Jamii ya Nzega (Nzega Community
Construction Corporation Ltd - NCCCL).
Lengo la Kampuni ya NCCCL lilikuwa ni kujenga
uwezo kwa kuwa na vifaa vya ujenzi wa barabara za halmashauri na mashine
ya uchimbaji wa visima kwa ajili ya huduma za maji.
Hata hivyo, wakati utekelezaji wa azimio hilo
ukiwa umeanza, Januari 4 mwaka huu kiliitishwa kikao cha dharura kwa
lengo la kubadili maazimio ya awali.
Zamu hii madiwani wakiungwa mkono na uongozi wa
CCM wa wilaya walikuja na mpango kwamba fedha hizo zigawanywe kwenye
kata, azimio ambalo linapingwa vikali na baadhi ya madiwani wakiongozwa
na mbunge huyo.
Baada ya azimio jipya kupitishwa, Dk Kigwangalla
aliitisha mkutano wa hadhara na kuwahutumia wananchi na mwishoni mwa
mkutano huo wananchi waliazimia kufungua kesi mahakamani kuzuia kutumika
kwa fedha hizo.
Ni katika mkutano huo ambapo Dk Kigwangalla
anadaiwa kuwatusi baadhi ya madiwani waliokuwa kinyume na yeye, matamshi
ambayo yamesababisha kuanzishwa kwa mchakato wa kumvua uanachama.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment