Kilosa. Hatimaye Daraja la Magole la Mto Mkundi ambalo tuta zake
zilisombwa na maji na kusababisha huduma ya usafiri kati ya Morogoro na
Dodoma kukatika kwa siku tatu, limefunguliwa kwa kuruhusiwa magari ya
mizigo yenye uzito wa zaidi ya tani saba kupita.
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli aliyefungua
daraja hilo jana saa 4.45 asubuhi alisema, kazi ya kutengeneza tuta hizo
zilizokuwa zimesombwa na mafuriko yaliyotokea Januari ya kuamkia 22,
saa 11 alfajili,ilifanyika kuanzia Alhamisi asubuhi kwa wahandisi wa
Wizara ya Ujenzi kusimamia kazi hiyo.
Dk Magufuli alisema, kukatika kwa tuta za daraja
hilo haijawahi kutokea tangu kujengwa kwa daraja hilo miaka ya 70 na
kwamba tuta hizo lilisombwa kwa mita 50 upande wa Morogoro na mita 20
upande wa Dodoma.
“Kama hatua za haraka zisingechukuliwa, ujenzi huu
wa tuta za daraja ungechukua miezi miwili hadi mitatu mpaka kukamilika
kwake, lakini niliwataka mainjinia (wahandisi) wangu kufanyakazi usiku
na mchana ili liweze kutumika na wananchi wapate huduma za kimsingi,
kwani magari mengi ya mizigo yamebeba bidhaa zinazohitajika upande wa
pili,” alisema Waziri Magufuli.
Waziri huyo wa ujenzi, pamoja na kuwapongeza
wahandisi hao kukesha usiku na mchana, aliwataka wasafiri wa mabasi na
magari madogo, kuendelea kutumia Barabara ya Melela-Kilosa kutokea
Dumila hadi foleni ya malori itakapomalizika.
Pia Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa
Morogoro, Boniface Mbao alisisitiza uamuzi huo wa Waziri Magufuli
kuzingatiwa na madereva ili zoezi hilo liweze kukamilika kwa haraka.
Kwa upande wao madereva wa magari makubwa na ya
masafa marefu, walimwomba Waziri Magufuli kuwaruhusu kupita mizani bila
kupima kwa kuonyesha risiti walizokwishapima katika mizani ya Kibaha.
Pia waliomba ili kukabiliana na foleni
iliyojitokeza kwa sasa na kwa baadaye, malori yasiyo na mizigo yapite
bila kupima, rasta katika milima ziondolewe, yabaki matuta na mizani ya
Kihonda iondolewe au kutengenezwa kutokana na kushindwa kufanya kazi
nyakati za mvua, mambo ambayo Dk Magufuli aliahidi kuyafanyia kazi ila
la kuacha kupima mizani alisema ni vigumu kwa vile lipo kisheria.
Baada ya kujibu maombi ya madereva hao wa malori,
Dk Magufuli aliwataka wahandisi hao wa wizara kuendelea kubaki katika
eneo hilo hadi daraja litakapo kamilika, kutokana na barabara hiyo
kutegemewa kupitisha zaidi ya magari makubwa 3,000 kwa siku.
Barabara ya Morogoro-Dodoma imekuwa ikipitisha
magari madogo na mabasi zaidi ya 25,000 kwa siku kupitika hali ya
waathirika wa mafuriko katika eneo hilo bado si shwari kutokana na
kulala nje ya nyumba zao na wengine kulala barabarani.
Akizungumza na gazeti hili mmoja wa waathirika
Haruna Rajabu alisema, kama misaada hiyo haitasimamiwa kikamilifu upo
uwezekano wa kuzuka kwa migogoro kwani kwa kiasi kikubwa waathirika wa
mafuriko hayo wamepoteza vyakula na mavazi.
Alisema yanapotokea majanga ya aina hiyo mara nyingi, kunazuka migogoro baada ya misaada inayotolewa kutolewa kwa kujuana na.
Wakati mwingine kutolewa kwa watu walionusurika badala ya kuwapa
kipaumbele watu walioathirika kwa kiasi kikubwa pamoja na watu
wasiojiweza kama wazee, wajane na watoto.
Hata hivyo Haruna aliiomba Serikali na wasamaria
wema kuwa pamoja na kupeleka misaada ya vyakula pia misaada ya sare za
shule, viatu na madaftari vinahitajika kwani wanafunzi wengi nao
wamepoteza vifaa hivyo muhimu.
Vilevile aliiomba Serikali kupeleka misaada ya
mbegu za mahindi, mpunga na mazao mbalimbali kwani mafuriko hayo
yamesababisha mbegu na mazao yaliyopandwa kwenye mashamba nazo kuzolewa
na maji na hawana mbegu za kupanda.
Naye Fatuma Mbonde mjane mwenye watoto wanne
ambaye pia ni mwathirika wa mafuriko hayo aliiomba Serikali kupeleka
dawa za magonjwa ya milipuko kwani kutokana na mafuriko hayo vyoo vingi
vimebomoka na hivyo vinyesi kuelea juu ya maji.
Aliomba pia msaada wa majisafi na umeme kwani kwa
sasa visima vya asili na mabomba yameziba na mengine kung’oka kabisa,
huku eneo hilo la Magole likiwa gizani kutokana na nguzo za umeme
kuanguka na kuzolewa na maji.
0 comments:
Post a Comment