LATEST POSTS

Monday, April 7, 2014

Yala: Shule iliyogeuka ‘kisiwa’

 
Sehemu ya Shule ya msingi Yala ikiwa  imejaa maji.

Yala ni shule ya msingi iliyopo katika Kijiji cha Yala Kata ya Luhanga Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya na ipo umbali wa kilomita 40 kutoka Barabara Kuu ya Mbeya-Iringa, ili kufika shuleni hapo inakulazimu kutembea kwa mguu kutokana na magari na pikipiki kushindwa kufika.
Shule hiyo ina muda wa zaidi ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, imezungukwa na mito minne ambayo imekuwa ikijaa maji kipindi cha masika na kusababisha kukatika kwa mawasiliano na ukosefu wa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na elimu.
Kutokana na tatizo hilo la mito kujaa maji shule hiyo imekuwa ikigeuka kuwa kisiwa na kusababisha wanafunzi na walimu kushindwa kufika shuleni kwani mito hiyo haina madaraja ya kuwawezesha kupita na kufika shuleni hapo.
Wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo wamekuwa wakitoka katika Vitongoji vya Mwashikamile, Ruaha, Waninyika, Mtakuja, Yala na Lusaka na wote hushindwa kuvuka mito hiyo na kufika shuleni huku walimu pia wakikumbwa na adha hiyo kutokana na shule hiyo kutokuwa na nyumba za kuishi Walimu.
Jairos Mpale ni Mwenyekiti wa serikali ndogo ya maendeleo ya Mwashikamile katika Kijiji cha Yala anasema kuwa tatizo hilo limekuwa kubwa zaidi kwa mwaka huu ukilinganisha na miaka mingine.Hii ni kutokana na mvua zinanyesha kwa wingi na wanafunzi wamekaa nyumbani muda mrefu bila kwenda shule.
“Watoto wetu wameshindwa kwenda shuleni hapo tangu shule zote zilipofunguliwa Januari, kutokana na mito kujaa maji na kuna mamba wengi na viboko hivyo ni vigumu kuvuka kwenda katika Shule ya Yala na watoto wetu wamekosa masomo na hatujui ni lini wataanza masomo,” anasema.
Naye Mtendaji wa kijiji cha Yala shule ilipo, Isaac Ngera anasema kuwa tatizo hilo huwa linajitokeza mara kwa mara katika msimu wa mvua na mito hiyo imekuwa ikijaa na kusababisha wananchi kushindwa kupata huduma mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja elimu, afya na majisafi na salama.
Aliitaja mito iliyojaa maji kuwa ni Itambo na lwashimala na vitongoji vilivyopo ng`ambo ya mito hiyo ni Ruaha na Woninyika kwa upande wa Kusini kuna vitongoji vya Mtakuja na Lusaka ambavyo vipo ng`ambo ya Mto Itambo na yote imejaa maji hakuna mawasiliano na upande wa pili.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Stephano Mlewa anasema kuwa kwa sasa hali ni mbaya katika shule hiyo kwani hakuna mwanafunzi anayefika shuleni hapo.
“Siyo kwa wanafunzi pekee hata kwa Walimu ni tatizo kubwa kwani wanaishi katika kitongoji ambacho kipo mbali na shule hiyo na inawalazimu wavuke mito miwili ambayo kwa sasa imejaa maji hivyo hakuna masomo,” anasema.
Anasema kuwa shule hiyo pia ina changamoto ya madarasa kwani ina jumla ya vyumba vya madarasa vinne pekee na wanafunzi wapo kuanzia darasa la kwanza hadi la saba hivyo husoma kwa kupokezana.
Ofisa Elimu Wilaya ya Mbarali, Henerico Batinoluho anasema kuwa shule ina wanafunzi zaidi ya 400 na kwamba mwaka huu shule ilifunguliwa Januari 6, lakini wamefanikiwa kuingia darasani katika kipindi cha wiki moja pekee.

“Hivyo hakuna elimu yoyote ambayo wanaipata wanafunzi katika Shule ya Yala kwani kwa utaratibu na kanuni ambazo mtoto anatakiwa kusoma shule ni kuanzia siku 194 hadi 196 lakini kwa sasa watoto hao hawajaingia darasani kwa robo muhula na haijulikani ni lini maji yatapungua ili waweze kuingia darasani,” anasema.
Anasema kuwa kutokana na hali ilivyo ya mvua kuendelea kunyesha katika maeneo hayo, wanafunzi hao wanatarajia kuingia darasani kuanzia Mei na kitaaluma watakuwa nyuma ya wenzao waliopo katika shule nyingine ambazo wanaendelea na masomo kwa sasa.
Kiwango cha ufaulu katika shule hiyo
Ofisa elimu huyo anasema kiwango cha ufaulu katika shule hiyo kimekuwa kikishuka siku hadi siku kutokana na mazingira hayo magumu yanayosababisha wanafunzi kuchelewa kuanza masomo mara shule zinapokuwa zimefunguliwa.
Anasema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu takwimu za kiwango cha ufaulu zinaonyesha kuwa mwaka 2010 alifaulu mtoto mmoja, 2011 walifaulu watoto wawili, 2012 walifaulu watoto tisa na mwaka jana 2013 hakuna mwanafunzi aliyefaulu na kujiunga kidato cha kwanza.
Anasema kuwa kwa sasa kuna wanafunzi 21 wa darasa la saba wakiwamo wanaume 13 na wasichana wanane na wengi wao wameacha shule kutokana na uwepo wa mazingira magumu ya kujifunzia katika shule hiyo.
Kauli ya wazazi wa watoto wanaosoma katika shule hiyo
“Hakuna ambacho watoto wetu wanakipata katika shule hii zaidi ya kufanya vibaya kwani baadhi ya watoto wamekuwa wakimaliza darasa la saba bila kujua kusoma na kuandika kutokana na mazingira haya magumu yaliyopo katika Shule ya Yala,” anasema Lingson Kakwambi.
Kakwambi anasema kuwa ili kuondokana na tatizo hilo na kuwasaidia wanafunzi kupata elimu bora ni vyema Serikali ikawasaidia kuweka madaraja katika mito hiyo itakayowawezesha wanafunzi na walimu kufika shuleni kwa urahisi.
Naye Watson Mwasemba anasema kuwa suluhisho la tatizo hilo ni wazazi kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha nyumba za walimu zinajengwa ili kuwaweze kukaa jirani na shule na kujenga madaraja kwenye mito hiyo ili njia ziweze kupitika wakati wote wa masomo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Adamu Mgoyi anasema tatizo hilo limewakumba wanafunzi ambao wanatoka katika vitongoji vilivyopo mbali na shule.
“Kwa kweli kwa sasa ni vigumu wanafunzi kufika shuleni na wanaofika ni wachache sana kwani mito imejaa maji mengi wanafunzi na walimu wanashindwa hivyo kuna mikakato ambayo kama halmashauri inayofanya ili kuweza kutatua tatizo hilo,” alisema.
Anasema kuwa kwa sasa wanashauriana na wataalamu ili kuangalia namna ya kuwasaidia wananchi wanaokaa katika kijiji hicho cha Yala na kuhakikisha wanafunzi na walimu wanawezeshwa kufika shuleni hapo muda wote wa masomo.
“Mazingira ya mito hiyo ni magumu kwani haina mwelekeo mmoja mvua zikinyesha mito inatanuka na maji kujaa sehemu kubwa hivyo kama madaraja hayatawekwa kitaalamu yatamezwa na maji hayo,” anasema.

0 comments: