Dar es Salaam. Wakati timu ya wahandisi
ikiendelea kufanya tathimni na marekebisho ya awali ya kipande cha reli
reli kilichoharibika eneo la Godegode kutokana na mvua kubwa zilizoanza
kunyesha mwanzoni mwa Januari mkoani Dodoma, hali imekuwa mbaya zaidi
baada ya kipande kingine kuharibika upya.
Kufumuka upya kwa kipande kingine cha reli
kumetokana na mvua zilizonyesha alfajiri ya juzi na kusababisha maji
kufunika eneo la reli hali iliyopelekea maji kufurika na kusababisha
uharibifu huo.
Hali hiyo imetokea baada ya muda wa wiki mbili
ambapo Kampuni ya Reli ilitangaza kukamilisha ukarabati wa kipande hicho
ili kuruhusu njia ya reli kupitika.
Akizungumza na gazeti hili, Kaimu Mkurugenzi wa
Kampuni ya Reli, Mhandisi Paschal Mafikiri alisema kuwa njia ya reli
katika eneo la Godegode imezidi kuwa mbaya zaidi kutokana na mvua hizo
kusababisha kufumuka kwa kipande kingine.
“Tathimini na marekebisho ya awali yamefanywa na
wahandisi wetu na tukakubaliana tuweke tuta lingine, lakini kabla hilo
halijafanyika mvua zimeharibu eneo lingine,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema kwamba marekebisho hayo
yanaweza kuchukua wiki mbili zaidi kukamilika kwake mpaka kurejesha
huduma za usafiri kwa watumiaji wa reli hiyo.
“Siwezi kusema kwa usahihi njia hii itaanza
kutumika lini, ila baada ya kurudi timu ya wataalamu iliyokuwa eneo la
tukio hapo ndio tutakuwa na taarifa zaidi, lakini kwa sasa ninachoweza
kusema hali ni mbaya eneo la Godegode na Gulwe.”
Januari 10 mwaka huu Kampuni ya Reli ilitanganza
kusimamisha safari zote za reli ya kati kwa muda usiojulikana kufuatia
kuwepo kwa uharibifu mkubwa wa kipande cha reli eneo la Godegode na
Gulwe uliotokana na mvua.
0 comments:
Post a Comment