Mawaziri na Manaibu Waziri katika picha ya pamoja na Rais Jakaya
Kikwete, Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal, Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue (wanne kushoto
mbele), baada ya Rais kuwaapisha Ikulu jijini Dar es Salaam jana. Picha
na Emmanuel Herman.
Dar es Salaam. Wadau mbalimbali wa uchumi, wamekosoa uteuzi wa
Manaibu Waziri wa Wizara ya Fedha, wakisema uteuzi huo haujalenga
mikakati ya kuleta maboresho ya kuondoa changamoto zilizopo katika
wizara hiyo.
Manaibu walioteuliwa juzi na Rais Jakaya Kikwete
ni pamoja na Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba na Mbunge wa
Mkuranga, Adam Malima.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Ajira nchini
(TAESA), Eliezer Mwasele alisema viongozi hao wamewekwa kwa lengo la
kutimiza malengo ya kisiasa.
“Ni mwaka mmoja tu umebakia tuingie kwenye
uchaguzi mkuu na ukiangalia Mwigulu ni mtu wa kusimamia sera na mipango
ya chama, nadhani hiyo ni ‘strategic Plan’ (mkakati maalumu) ili
kujipanga kisiasa,” alisema Mwasele.
Mwasele amepongeza uteuzi wa Waziri mpya wa Fedha,
Saada Mkuya akisema: “Sina shaka naye, ila hao manaibu hakuna lolote
katika suala la uwajibikaji, hawana uwezo wa kiutendaji ila ni siasa
tu,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Maofisa Watendaji
Wakuu wa Kampuni binafsi (CEO’s Roundtable), Ali Mufuruki alisema
viongozi hao wanatakiwa kuwa makini na changamoto kubwa zinazohitaji
kupatiwa majibu kwa sasa.
Mufuruki alitaja changamoto kubwa mbili ambazo ni
juhudi za ukusanyaji wa kodi pamoja na mvutano wa suala la mafuta na
gesi kwa Watanzania.
Kuhusu ukusanyaji wa kodi, Mufuruki alisema mpaka
sasa wafanyabiashara wengi bado hawajawa tayari kukubaliana na matumizi
ya mashine za EFD.
“Binafsi sioni tatizo kwenye matumizi ya mashine
kwa sababu ili kukuza uchumi ni lazima kila mtu alipe kodi, lakini cha
kushangaza suala hilo mpaka limekuwa likipingwa na viongozi wa CCM, ni
makosa,” alisema.
Kwa upande wake, Profesa Humphrey Mushi kutoka
kitengo cha Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alitaja maeneo
makubwa matatu ya kuzingatiwa na mawaziri hao ambayo ni kuhakikisha
serikali inapunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima, kuwekeza bajeti kubwa
katika sekta nyeti za Kilimo na Reli.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment