My God! Bibi harusi mtarajiwa aliyejulikana kwa jina la Edna Sangawe
(34), mkazi wa Mikocheni B jijini Dar anadaiwa kunyongwa na watu
wasiojulikana na mwili wake kutelekezwa maeneo ya Changanyikeni,
Makongo-Juu, Dar, Risasi Jumamosi lina kisa kizima.
ILIVYOKUWA
Kwa mujibu wa chanzo makini, Machi 31, mwaka huu muda wa saa 2:00 usiku, bwana harusi mtarajiwa aliyetajwa kwa jina moja la Stanley, alipigiwa simu na mtu asiyemjua kuwa aende mbali kidogo na kwake.
“Aliyempigia simu alimwambia anamhitaji kwa ajili ya matengenezo ya friji kwani Stanley ni fundi wa mafriji.
“Bila kujua kinachoendelea, jamaa alikwenda hadi mahali alipoelekezwa
na aliambiwa akifika mahali hapo asigonge geti mpaka mtu huyo
atakapofika, alipofika hakuona mtu na alipopiga simu haikupokelewa,”
kilisema chanzo hicho.
Ilielezwa kwamba, kwa kuwa hakukuwa na dalili za mtu yeyote kuonesha
kumuita, Stanley aliamua kurudi kwake, alipofika hakumkuta mchumba wake
ambaye alimuacha anapika.
APATA SHAKA
Ilifahamika kwamba jamaa huyo
alipoingia ndani kwake alijaribu kumtafuta Edna bila mafanikio ndipo
akahisi huenda atakuwa amekwenda kafuata mahitaji dukani lakini muda
ulizidi kuyoyoma, alimua kwenda kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi
cha Chuo Kikuu (Mlimani) ambapo polisi walimwambia zikipita saa 24 arudi
tena.
AKUTWA AMENYONGWA
Ilizidi kudaiwa kwamba katika
kuendelea kumtafuta kwa kuulizia nyumba hadi nyumba ndipo jirani mmoja
alipomwambia kuwa alisikia kelele kwa mbali na waliposogelea eneo
alilosikia sauti walimkuta Edna akiwa amenyongwa.
Stanley alirudi Kituo cha Polisi cha Chuo Kikuu na kutoa taarifa
ambapo polisi wafika eneo la tukio na kuchukua mwili huo na kuupeleka
katika Hospital ya Taifa Muhimbili, Dar kwa uchunguzi zaidi.
POLISI WAMSHIKILIA MCHUMBA’KE
Ilifahamika
kwamba ilibidi polisi wamshikilie Stanley kwa uchunguzi zaidi na pia kwa
usalama wa maisha yake kwa kuwa siku ya tukio, Stanley ndiye aliyekuwa
pamoja na marehemu.
MAJIRANI WA MAREHEMU WASHTUKA
Wakizungumza na
gazeti hili huku wakiomba kutotajwa gazetini, majirani wa marehemu
walisema walipokea taarifa hizo kwa mshtuko kwani awali walidhani ni
utani wa Sikukuu ya Wajinga (Aprili Mosi).
“Mwanzoni tulijua ni utani kutokana na leo ni siku ya wajinga lakini
niliwashauri wenzangu tuelekee Kituo cha Polisi cha Chuo Kikuu kufahamu
baada ya kupigiwa simu na mmoja wa wanandugu wa mwanaume, tulipofika
kituoni ndipo tukaamini,” alisema mmoja wa majirani hao.
KABLA YA TUKIO
Wakisimulia maisha ya marehemu,
majirani hao walisema marehemu kabla ya kupatwa na umauti, alikuwa
katika taratibu za vikao vya harusi ambavyo vilishaanza hivyo vikao
hivyo vikabadilika na kuwa mikakati ya mazishi.
“Kabla ya tukio hilo, marehemu alikwenda kwao Moshi mkoani
Kilimanjaro wiki moja iliyopita na mchumba’ke (Stanley) kwa lengo la
kutambulishana na mikakati ya ndoa kupamba moto kwani ilikuwa ifanyike
siku chache kabla ya tukio hilo la kusikitisha.
“Walipotoka Moshi walikwenda Tanga kwa upande wa mwanaume kwa lengo
hilohilo la utambulisho na tulijua anarudi nyumbani leo (Jumanne) hapa
alipopanga lakini cha kushangaza tulipigiwa simu na kwenda kukuta
msiba,” alisema jirani.
MAZISHI
Mwili wa marehemu ulihifadhiwa katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo hadi tunakwenda mitamboni,
taratibu za mazishi zilikuwa zikiendelea na ilielezwa kuwa wamepanga
kuusafirisha mwili wa marehemu nyumbani kwao Moshi.
KAMANDA WA POLISI
Gazeti liliwasiliana na
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Dar, ACP Camillus Wambura
ambaye alikiri kupokea taarifa za tukio hilo na kwamba polisi
wanaendelea na uchunguzi ili kujua aliyehusika na mauaji hayo.
0 comments:
Post a Comment