Rais Jakaya Kikwete akimuapisha Jenister Mhagama kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi katika hafla iliyofanyika katika Viwanja vya Ikulu, jijini Dar es Salaam jana. Picha na Emmanuel Herman
Dar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, vitalazimika kufanya mabadiliko katika safu zake za uongozi kutokana na athari zilizosababishwa na mabadiliko yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete katika Baraza la Mawaziri.
Juzi, Ikulu ilitangaza mabadiliko katika baraza
hilo ambayo yaliwaweka kando mawaziri na manaibu waziri watano, huku
sura kumi mpya zikiingia, mabadiliko ambayo yameacha nafasi mbili wazi
katika sekretarieti ya CCM na nafasi nne katika uongozi wa Bunge.
Miongoni mwa walioteuliwa na kuapishwa jana ni
waliokuwa wajumbe wa Sekretarieti ya CCM; Dk Asha-Rose Migiro ambaye
ameteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na Mwigulu Nchemba ambaye
ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Fedha.
Nchemba ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara,
wakati Dk Migiro ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, Siasa na
Uhusiano wa Kimataifa.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye
alisema jana kuwa viongozi wa sekretarieti ya CCM wanapoteuliwa kushika
nafasi nyingine za Serikali, wanalazimika kuziacha nyadhifa zao katika
chama.
Nape alisema kwa maana hiyo, Mwenyekiti wa CCM,
Rais Kikwete atalazimika kuteua watu wa kuziba nafasi za Dk Migiro na
Nchemba. “Huu ni utaratibu tuliojiwekea katika chama kwamba viongozi wa
sekretarieti hawatafanya kazi mbili za chama na Serikali, kwa hiyo
viongozi hawa pia wataziacha nafasi za chama,” alisema Nape.
Hata hivyo Nape alisema utaratibu huo hauwagusi
wenyeviti wa chama hicho wa mikoa, ambao wameteuliwa kuwa mawaziri ama
manaibu waziri kwani uenyekiti si nafasi ya utendaji.
Katika uteuzi huo, Mwenyekiti wa CCM, mkoa wa
Simiyu, Dk Titus Kamani aliteuliwa kuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na
Uvuvi, wakati Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi aliteuliwa
kuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
“Hawa wanaweza kuendelea na nyadhifa zao za
uenyeviti katika chama, huku wakiwa na nyadhifa serikalini, hii haina
athari kwa sababu siyo watendaji wakuu wa chama,” alisema Nape.
Bungeni
Bunge pia litalazimika kuchukua hatua za kuziba
nafasi zilizoachwa wazi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge pia Kiongozi
wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii, Jenister Mhagama ambaye ameteuliwa kuwa
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Wengine ni Mahmoud Mgimwa aliyekuwa Mwenyekiti wa
Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara na sasa ameteuliwa kuwa Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Katiba, Sheria na Utawala, Pindi Chana ambaye sasa ni Naibu Waziri wa
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
Naibu Spika, Job Ndugai alisema nafasi zilizoachwa wazi na
wabunge hao zitazibwa kwa kuchagua wenyeviti wengine kwa mujibu wa
Kanuni za Bunge.
“Mapema sana kamati za kudumu za Bunge zitakutana
kabla ya Bunge la Katiba, nafasi ambazo zimeachwa wazi na walioteuliwa
kuwa mawaziri zitazibwa kwa sababu kamati husika watachagua wenyeviti
wao,” alisema Ndugai.
Kuhusu mawaziri walioachwa katika mabadiliko hayo, Ndugai alisema wao wanarejea kuwa wajumbe wa kamati.
“Kila mbunge ana haki ya kuwa kwenye kamati, kwa
hiyo tutawapanga kwenye kamati mbalimbali na hawazuiwi kuchaguliwa kuwa
wenyeviti ikiwa watapangwa kwenye kamati ambazo wenyeviti wao
wamechaguliwa kuwa mawaziri,” alisema Ndugai.
Mawaziri walioachwa kwenye uteuzi huo ni aliyekuwa
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck
Ole-Medeye, Dk Terezya Huvisa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Mazingira) na Benedict Ole-Nangoro, aliyekuwa Naibu Waziri wa
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
Wengine ni Gregory Teu, ambaye alikuwa Naibu
Waziri wa Viwanda na Biashara pamoja na Philipo Mulugo aliyekuwa Naibu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Viongozi hao wanaungana na wenzao wanne ambao
uwaziri wao ulitenguliwa na Rais Kikwete mwishoni mwa mwaka jana
kutokana na matokeo ya uchunguzi uliofanywa na Bunge kuhusu utekelezaji
wa operesheni tokomeza ujangili.
Hao ni pamoja na waliokuwa Mawaziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk
Mathayo David, Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na aliyekuwa
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment