WAKATI Bunge Maalumu la Katiba likikutana kesho kwa ajili ya kupokea
taarifa za kamati na kuanza mjadala wa jumla kwa wajumbe wote, Rais
Jakaya Kikwete ameridhia ombi la kulisitisha kuanzia Aprili 28 hadi
Agosti mwaka huu, ili kupisha Bunge la Bajeti liendelee na vikao vyake.
Tangu kuanza kwa Bunge hilo Februari 18, mwaka huu, wajumbe wameweza
kujadili sura mbili pekee za rasimu ya katiba ambazo hata hivyo uamuzi
wake utategemea majadiliano yatayofanyika baada ya kamati zote
kuwasilisha taarifa zao kuanzia kesho.
Bunge hili limetumia takribani wiki tatu kujadili kanuni zake, na
hivyo kupunguza muda wake wa siku 70 uliowekwa kisheria bila kuanza
kujadili sura na ibara za rasimu hiyo.
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta alizungumza na waandishi wa
habari jana baada ya kukutana na viongozi wawili wakuu wa dini, Askofu
Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama
Sitta alisema kuwa juzi alipokutana na Rais Kikwete alimueleza
umuhimu wa kuongeza muda kwa Bunge hilo ambapo alionyesha nia ya
kulisogeza hadi Agosti mwaka huu.
Alisema kwa sasa wapo katika hatua za mwisho za kumalizia kuipitia
sura ya kwanza na ya sita ya rasimu inayozungumzia muundo wa serikali
ambapo kesho wenyeviti wa kamati 12 za Bunge hilo watawasilisha taarifa
zao kwa mtiririko bila majadiliano.
“Wakishawasilisha tunatarajia wiki ijayo wajumbe wote kupata fursa ya
kuchangia kwa uwiano, lakini niseme kuwa sina hakika kama kwa muda
uliosalia tutakuwa tumemaliza maana sheria namba 83 ya mabadiliko ya
katiba inasema ni siku 70 tu, hivyo itakuwa ni aibu rasimu ipitiwe sura
mbili pekee kati ya sura 17 zilizopo,” alisema.
Alieleza kuwa baada ya Bunge la Katiba kuahirishwa, litaanza Bunge la
Jamhuri kwa ajili ya bajeti hadi Juni, na Julai wataitumia kwa kuwapa
wabunge nafasi ya kutembelea majimbo yao ili Agosti Bunge la Katiba
liweze kurejea tena kuendelea kupitia sura nyingine.
Sitta alifafanua kuwa baada ya Bunge Maalumu kuhitimisha kazi yao,
watakabidhi kwa Rais Kikwete na mwenzake wa Zanzibar rasimu ya katiba
inayopendekezwa kwa ajili ya kuiwasilisha kwa wananchi waweze kuipigia
kura ya ama kuikubali au kuikataa.
“Unajua licha ya kuwepo purukushani nyingi za hapa na pale nia ya
wabunge wengi ni kupata katiba bora na nzuri hivyo mchakato utakamilika
tu,” alisema.
Akizungumzia sababu ya kuwatembelea viongozi hao, Sitta alisema kuwa
katiba inamgusa kila raia na ndiyo sababu kama mwenyekiti wa Bunge
Maalumu aliamua kukutana nao ili kuwafahamisha wametoka wapi, wako wapi
na nini kinaendelea.
Sitta aliongeza kuwa kwa kutambua nafasi ya viongozi hao katika jamii
hasa kwa kuongoza kundi kubwa la Watanzania, amekutana nao ili kuwasihi
na kuelimisha wananchi wengi wanaowaongoza ikiwemo kuliombea Bunge hilo
litoke salama.
Sitta atia shaka
Katika hatua nyingine, ziara ya Sitta kwa viongozi wakuu wawili wa
dini imeacha maswali mengi ambapo baadhi ya watu wameitafsiri kama
kampeni ya Chama Cha Mapinduzi kutafuta uungwaji mkono katika kutetea
mfumo wake wa muundo wa serikali mbili.
Hatua hiyo inatokana na msimamo wa viongozi hao wawili kuwa sambamba
na ule wa CCM katika suala la muundo wa Muungano ambapo wote wanataka
serikali mbili.
Vyanzo vyetu vya ndani vimedokeza kuwa kwa muda mrefu CCM ilikuwa
ikitafuta namna ya kupenyeza karata yake ili kupata uungwaji mkono wa
Kanisa Katoliki ambalo lina wafuasi wengi nchini.
Hivi karibuni, Kardinali Pengo alilazimika kukutana na vyombo vya
habari ili kuweka sawa taarifa iliyokuwa imetolewa na Tume ya Haki na
Amani ya Baraza la Maaskofu wa kanisa hilo kupitia kwa Askofu Mkuu wa
Jimbo Kuu la Tabora, Paul Ruzoka akitaka mapendekezo ya wananchi kwenye
rasimu kuhusu serikali tatu yaheshimiwe.
Alisema maoni hayo ni yake binafsi wala si msimamo wa kanisa hilo
huku akiweka bayana kuwa yeye ni muumini wa serikali mbili, lakini pia
akasisitiza kwamba hayo ni maoni yake.
Wapinzani wajipanga
Kutoka mjini Dodoma, taarifa zinaeleza kuwa wajumbe wa kambi ya
upinzani wamejipanga ipasavyo kutengeneza taarifa ya maoni kinzani kwa
ajili ya kukata ngebe za CCM, wakidai inatumia wingi wake kutaka
kubadili maudhui ya vifungu vya rasimu kutoka mapendekezo ya serikali
tatu kwenda mbili.
Tanzania Daima Jumatano limedokezwa kuwa wajumbe hao kupitia maoni
yao kinzani ya wachache, wameandaa hoja kadhaa za kulishawishi Bunge
zima ili kuhakikisha mapendekezo ya muundo wa serikali tatu
unaopendekezwa na wananchi kupitia rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya
Katiba yanapitishwa yalivyo.
“CCM walitegemea kutumia kamati kuburuza wajumbe ili kupata theluthi
mbili ya kura kwa pande zote waweze kubadili rasimu watakavyo kutoka
serikali tatu kwenda mbili, lakini imeshindikana baada ya kukosa kura
hizo kwenye takribani kamati zote.
“Sasa wameandaa taarifa za kuleta bungeni wakionyesha wajumbe wengi
kwenye kamati wamependekeza serikali mbili, na hivyo wamebadili vifungu
vya rasimu vionyeshe hivyo, hatutakuwa tayari kwa hili, nakuhakikishia
moto utawaka, sisi tumejipanga kwa hoja wao wanatumia wingi wao bila
hoja… tutaona,” alisema mtoa taarifa.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment