Serikali
imesema kuanzia Julai mosi mwaka huu, ajira za utumishi wa umma
zitakuwa zikiombwa kwa njia ya mtandao, ili kuongeza ufanisi wa mchakato
wa kuwapata watumishi wenye sifa na kupunguza malalamiko ya kupotea kwa
barua za maombi.
Akizindua
baraza la kwanza la wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Sektretarieti ya
Ajira katika Utumishi wa Umma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi),
Celina Kombani alisema mtandao huo umezinduliwa na waombaji watapaswa
kuingia katika tovuti maalumu ya ajira na kutuma maombi
yaliyoambatanishwa na vyeti vya taaluma walizosomea.
“Maombi
kwa njia ya mtandao yatapunguza kazi ya kuchambua maelfu ya barua za
maombi ya kazi zilizokuwa zinatumwa, itapunguza pia manung’uniko kwamba
barua zimetumwa kisha zimekaliwa tu,” alisema Kombani.
Waziri
huyo, alisema kwa kutumia utaratibu huo mpya, wananchi wanaotaka ajira
serikalini watakuwa na uhakika kuwa barua zao zimefika na kupokewa na
wahusika. Pia, wanaweza kupata mrejesho kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu
zao za mkononi.
Kwa
upande wake Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma,
Xavier Daudi alisema baada ya kuona mchakato wa kuajiri unachangamoto
nyingi, waliamua kubuni mfumo wa kuomba ajira kupitia mtandaoni.
“Utaratibu
huu utatupunguzia gharama, wanafunzi wanaohitimu kila mwaka vyuoni ni
maelfu kwa maelfu na nafasi tunazopata serikalini kupitia sekretarieti
ya ajira hazizidi 12,000 kila mwaka,” alisema Daudi.
Hata
hivyo, katibu huyo alisema wamekuwa wakipata changamoto kubwa kutokana
na baadhi ya waombaji kutumia vyeti vya kughushi na hivyo kulazimika
kwenda kwenye vyuo husika kuvithibitisha.
0 comments:
Post a Comment