KATIBU wa Taasisi na Jumuiya ya Kiislamu, Sheikh Issa Ponda,
ameendelea kusota rumande hadi pale jalada la kesi yake litakaporejeshwa
kutoka Mahakama Kuu.
Akiahirisha kesi hiyo jana hadi Aprili 16, Hakimu mkazi mkoani
Morogoro, Marry Moyo, aliitaka Idara ya Upelelezi kufuatilia jalada la
mtuhumiwa Mahakama Kuu ili kesi ianze kusikilizwa.
Sheikh Ponda anayetetewa na wakili wa kujitegemea, Batheromeo
Tharimo alifikishwa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali licha ya
kutokuwepo umati mkubwa wa wafuasi wake.
Mara baada ya kufikishwa, wakili wake Tharimo alidai kuwa
amewasiliana na wakili mwenzake Juma Nassoro ambaye alimweleza kuwa kuna
ombi waliliwasilisha Mahakama Kuu la kutaka shauri hilo kutoendelea
kusikilizwa katika Mahakama ya Mkoa wa Morogoro.
Katika ufafanuzi wake juu ya madai hayo, Tharimo alisema kuwa ombi
hilo linatokana na rufaa namba 98 ya mwaka 2013 waliyoikata mbele ya
Mahakama Kuu kuhusu Mahakama ya Kisutu kwa shitaka la kwanza la kutotii
amri halali linalomkabili Ponda mahakamani hapo.
Wakili huyo ambaye alidai kuwa uendeshaji wa kesi hiyo hautaendelea
hadi uamuzi wa rufaa waliyoikata Mahakama Kuu utakapotolewa, aliiomba
mahakama kupanga tarehe ya kutaja kesi hiyo.
Hata hivyo, uliibuka ubishano wa kisheria baina ya wakili Tharimo na
wakili wa serikali, Sunday Hiela, aliyedai ana kumbukumbu za kuonyesha
mshtakiwa alimkana wakili Tharimo.
Katika maelezo yake Hiela aliongeza kuwa mahakama inashindwa kujua
kama anamwakilisha Sheikh Ponda au anatoa maelezo ya wakili Juma Nassoro
ambaye hakuwepo mahakamani hapo.
Wakili huyo wa serikali aliendelea kumwekea pingamizi akidai kuwa
hakuna nakala yoyote ya ombi ambalo wakili Tharimo alidai kuwa
waliliwasilisha Mahakama Kuu na kwamba dhamira ya upande wa utetezi ni
kuchelewesha kesi hiyo ambayo ipo mahakamani hapo kwa zaidi ya mwaka
mmoja sasa.
Kufuatia kuwepo kwa mapingamizi katika kesi hiyo, hakimu Moyo
alilazimika kuingilia kati akisema hadi sasa mahakama bado haijapokea
jalada hilo kutoka Mahakama Kuu ili ipate muongozo wa kuendelea na kesi
hiyo.
Baadaye aliihairisha kesi hiyo hadi Aprili 16 itakapotajwa tena,
ingawa wakili Tharimo aliomba kesi hiyo itajwe Aprili 14 kwa madai kuwa
hatakuwepo kutokana na kuwa na kesi nyingine.
Sheikh Ponda alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Agosti
10, 2013 akikabiliwa na mashitaka matatu likiwemo la kutotii amri halali
iliyotolewa Mahakama ya Kisutu, kutoa maneno yenye nia ya kuharibu
imani za dini na kushawishi watu kutenda kosa.
0 comments:
Post a Comment