LATEST POSTS

Thursday, January 9, 2014

Operesheni Ujangili yazoa vigogo 21

  • Nyalandu atangaza hatua dhidi yao, kasi ya ujangili inatisha
Lazaro Nyalandu

KIMBUNGA cha Operesheni Tokomeza Ujangili, kimeendelea kufyeka vigogo, safari hii maofisa 21 wa Idara ya Wanyamapori nchini, wamesimamishwa kazi.
Kusimamishwa kwa vigogo hao kulitangazwa jana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.
Hatua ya kusimamishwa kwa vigogo hao, imekuja takribani mwezi mmoja umepita tangu Rais Jakaya Kikwete alipowang’oa mawaziri wanne kutokana na kuwapo kwa madai ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu wakati wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Waliokumbwa na kimbunga hicho ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo David Mathayo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki ambaye kabla ya hatua ya Rais Kikwete kutangaza kuwang’oa, alitangaza kujiuzulu mwenyewe.
Nyalandu alisema kusimamisha kwa vigogo hao 21 kumetokana na uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili za kuhusika na ujangili na vitendo vya rushwa.
Alisema watumishi hao pia wamebainika kusaidia mtandao wa ujangili nchini, hivyo mbali ya kuwasimamisha hatua zaidi ikiwemo kuwafukuza kazi na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria, zitachukuliwa dhidi yao.
Hata hivyo, licha ya kutangaza kuwasimamisha kazi vigogo hao, Nyalandu alishindwa kutaja majina yao na badala yake alitaja mapori ya hifadhi wanayotoka na idadi yao.
“Wizara baada ya kufanya uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili baadhi ya watumishi wa Idara ya Wanyamapori wanaotuhumiwa kuhusika na ujangili na vitendo vya rushwa  na kusaidia mtandao wa ujangili nchini, imewasimamisha watumishi 21 wa idara hiyo kutoka mapori ya akiba na kanda za kikosi dhidi ya ujangili na hatua zaidi zinachukuliwa dhidi yao kwa mujibu wa sheria,” alisema Nyalandu.
Alitaja vikosi wanavyotoka na idadi yao kwenye mabano kuwa ni Kikosi dhidi ya Ujangili Arusha (11), Pori la Akiba Rukwa –Lwafi (4), Kikosi dhidi ya Ujangili Bunda (1), Pori la Akiba Maswa (3), Pori la Akiba  Selous  (1) na mapori ya akiba Lukwika, Lumesule –Msanjesi (1).
Nyalandu alisema wizara pia imemsimamisha kazi na kumchukulia hatua za kumfikisha mahakamani askari wa wanyamapori, Agostino Lori (42) kutoka mkoani Singida kwa tuhuma za vitendo vya hujuma, rushwa na ujangili dhidi ya wanyamapori.
Pia alisema askari huyo alikutwa  na bunduki mbili na ndege aina ya Heroe ‘flamingos’ 12, aliokuwa akiwahifadhi uani mwa nyumba yake kinyume cha sheria.
Aliongeza kuwa wizara haitasita kumchukulia hatua mtumishi yeyote anayetumia wadhifa wake kuhujumu rasilimali za taifa.
Hata hivyo, aliongeza kuwa hali ya ujangili nchini ni mbaya kutokana na tembo kuendelea kuuawa kwa kasi ya kutisha.
Alisema mwezi Desemba pekee, takwimu zinaonyesha kuwa tembo 60 waliuawa katika mapori mbalimbali ya hifadhi ya taifa.
“Sisi tunatumia njia mbalimbali za kiitelijensia kuhakikisha kuwa tunawatia nguvuni wote wanaojihusisha na ujangili, hivyo wasifikirie kuwa hawatojulikana na uchunguzi unaendelea dhidi yao,” alisema Nyalandu.
Pia alisema serikali ipo katika mchakato wa kuhakikisha inaongeza idadi ya askari wanyamapori katika mapori yake ya akiba ili kukabiliana na mauaji ya tembo na wanyama wengine.
Kusimamishwa kwa vigogo hao wa Maliasili na kutimuliwa kwa mawaziri wanne, kumetokana na ripoti ya Kamati ndogo ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyoongozwa na Mbunge wa Kahama, James Lembeli ambayo ilibaini kuwapo ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kunakodaiwa kusababishwa na uzembe wa mawaziri waliotimuliwa.

Chanzo: Tanzania Daima

0 comments: