Kamanda wa polisi Mkoa wa Tabora
HATMA
ya Mkuu wa Kituo cha Polisi Igunga mkoani Tabora, SP Edson Mfuru
anayedaiwa kumuachia mtuhumiwa Magata Singu anayetuhumiwa kumpa mimba
mwanafunzi wa darasa la sita mwenye umri wa 14 katika Shule ya Msingi
Hani Hani, iliyopo Igunga sasa ipo mikononi mwa kikosi cha kupambana na
rushwa (TAKUKURU).
Wakati TAKUKURU wakiingilia kati suala hilo, taarifa zaidi zinasema
kuwa Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Peter Ouma anafanya jitihada za
kumnusuru SP Mfuru asikabiliane na mkono wa sheria.
Hatua ya RPC Ouma kuhusishwa kumuokoa SP Mfuru, inatokana na madai ya
kushindwa kuwachukulia hatua askari wanaodaiwa kuchana karatasi
iliyoandikwa maelezo ya binti aliyelalamika (RB) pamoja na ile ya
mtuhumiwa kukamatwa kwa mara ya kwanza.
Uamuzi wa TAKUKURU umekuja siku chache baada ya Kamanda Ouma kukutana
na OCD wa Igunga, Abed Maige pamoja na OCS Mfuru katika kikao cha ndani
ambapo maofisa hao wa polisi walimueleza RPC namna siri za polisi
zinavyovujishwa, na kumuomba awasaidie kukabiliana na hali hiyo.
Katika kikao hicho cha ndani, inaelezwa kuwa RPC Ouma aliwaeleza wazi
kuwa kukithiri kwa rushwa na kudhulumiana ndiyo chanzo cha baadhi ya
mambo ya polisi kuvuja hadharani.
Hata hivyo, katika kikao hicho inaelezwa kuwa lilitolewa agizo la
kuwahamisha baadhi ya askari waliotuhumiwa kuwa nyuma ya siri za
kuachiwa mtuhumiwa Singu.
Jambo jingine lililosababisha TAKUKURU waingilie kati ni pamoja na
mtu aliyemwekea dhamana Singu kuendelea kuwa nje huku mtuhumiwa
aliyewekewa dhamana akiwa hajulikani alipo.
“Bado hali ni mbaya na sasa TAKUKURU wameshaingilia kati kwa kuanza
kumhoji mlalamikaji na pia kutaka kujua sababu za mtuhumiwa kutofikishwa
mahakamani,” kilisema chanzo chetu ndani ya Jeshi la Polisi Igunga.
Kwa mujibu wa habari hizo, miongoni mwa watu watakaotoa maelezo mbele
ya TAKUKURU ni pamoja na askari aliyemkamata mtuhumiwa na yule
aliyeshika faili la kesi kabla ya mtuhumiwa kuachiwa.
Kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Igunga, John Ngunangwa alipoulizwa juu
ya kikosi chake kuingilia kati suala hilo, alikiri kulifuatilia huku
akikataa kutoa maelezo zaidi kwa ajili ya kukamilisha taratibu za
kuwakamata wahusika.
RPC Ouma alipoulizwa hatua zilizochukuliwa na Jeshi la Polisi kwa watuhumiwa, alisema bado wako kwenye uchunguzi.
Alipotakiwa kueleza kama kunahitajika uchunguzi zaidi ya kuanzia
katika kitabu cha kumbukumbu ya matukio ya polisi na kufuatilia namba
aliyopewa mlalamikaji katika tuhuma hizo, RPC Ouma alisema yupo katika
kikao na kukata simu.
Hivi karibuni, gazeti hili liliandika juu ya mtuhumiwa Magata Singu
kuachiwa kwa dhamana ya sh mil. 3.4 kutokana na tuhuma za kumpa mimba
mwanafunzi wa darasa la sita mwenye umri wa miaka 14.
Ilielezwa kuwa Novemba 9, wazazi wa mtoto huyo walifika katika Kituo
cha Polisi Igunga na kufungua mashitaka na kupewa namba ya jalada, RB
IG/1430/2013 na kisha mtuhumiwa kukamatwa Novemba 10 na kuachiwa Novemba
11.
Chanzo: Tanzania
0 comments:
Post a Comment