HALMASHAURI zote za wilaya nchini zimepigwa marufuku kuandaa vikao
vya halmashauri bila kutoa taarifa kwa wabunge kwa sababu nao wana
haki ya kuhudhuria vikao hivyo Kikatiba.
Hayo yalielezwa Bungeni mjini hapa jana na Naibu Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),
Aggrey Mwanri, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Kasulu
Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi).
Mbunge huyo alitaka kujua, Serikali inazichukulia hatua gani baadhi
ya halmashauri nchini zikiwemo za Kasulu na Kibondo, ambazo huandaa
vikao vya halmashauri bila kuwaita wabunge na hasa wakati vikao vya
Bunge vikiendelea.
Mbunge huyo pia, alihoji ni kwa nini makatibu wa wabunge hata
wakiingia kwenye vikao hivyo hawalipwi posho kwa madai kuwa si wajumbe
wa vikao wakati maofisa tarafa na watendaji wanalipwa posho hizo pindi
wanapoingia kwenye vikao hivyo.
Akijibu swali hilo, Mwanri alisema tayari Serikali imeandaa taarifa
itakayopelekwa kwa halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa zinaandaa
vikao kulingana na ratiba za Bunge ili wabunge ambao ni wajumbe wa
vikao hivyo nao wapate fursa ya kuhudhiria.
Alisema kikatiba Wabunge nao ni madiwani wana haki zote za
kuhudhuria vikao vya halmashauri, na kupiga marufuku halmashauri zote
nchini kuandaa vikao vya halmashauri bila kumpa taarifa mbunge.
“Huyu mbunge ana mchango mkubwa kwenye vikao hivi, anahudhuria vikao
vikubwa kama Bunge, hivyo ana uzoefu na uelewa mkubwa,” alisisitiza
Mwanri.
Aidha Kuhusu posho kwa maofisa tarafa, Naibu Waziri huo alikiri kuwa
huwa wanalipwa posho wakiingia kwenye vikao hivyo, kwa sababu wao ni
wasaidizi wakubwa wa Mkuu wa Wilaya na wanatambulika kisheria wakati
makatibu wa Bunge pamoja na kuwa na sifa ya usaidizi kwa mbunge bado
hawajatambulika kisheria kuweza kulipwa posho katika vikao hivyo.
Alisema upo uwezekano wa suala hilo kushughulikiwa kwa wabunge
kuwasilisha maoni na mapendekezo ya kuibadilisha Sheria iliyopo ya
halmashauri ambayo itaweza kuwatambua makatibu wa Bunge kama wasaidizi
wa wabunge na walipwe posho kwenye vikao hivyo.
0 comments:
Post a Comment