MKOA wa Kigoma unazalisha tumbaku zaidi ya tani 5,000 kwa mwaka.
Naibu waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima alitoa kauli
hiyo bungeni mjini hapa jana akijibu swali la Mbunge wa Kigoma Kusini,
David Kafulila (NCCR-Mageuzi), ambaye alitaka kujua ni kwa nini mpaka
sasa mkoa huo haujapewa hadhi ya kuwa mkoa wa Kitumbaku ili kusogeza
huduma kwa wakulima ambao kwa sasa wanategemea huduma kutoka Urambo.
Alifafanua kuwa mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa mikoa inayozalisha
tumbaku nchini ambapo zaidi ya tani 5,000 huzalishwa kwa mwaka.
Malima alisema mkoa huo umepitishwa kulima tumbaku kwa mujibu wa
sheria ya tumbaku namba 24 ya mwaka 2001 na kanuni zake za mwaka 2005.
Aidha, alisema pamoja na kiasi hicho cha uzalishaji mkoa wa Kigoma
haujapewa hadhi ya kuwa mkoa wa Kitumbaku kutokana na changamoto ya
upatikanaji wa fedha ili Bodi ya Tumbaku iweze kufungua ofisi na
kusogeza huduma karibu kwa wakulima wa zao hilo kama ilivyo kwa mikoa
mingine ya kitumbaku.
Alisema kwa kutambua mchango wa wakulima wa tumbaku wa mkoa wa
Kigoma, serikali kupitia Bodi ya Tumbaku katika mwaka wa fedha 2013/14
inatarajia kufungua ofisi zake mkoani Kigoma ili kusogeza huduma kwa
wakulima wa zao hilo.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment