RAIS
Jakaya Kikwete amewashangaa wanasiasa wanaokosoa kitendo cha Serikali
yake kukopa fedha nje ya nchi kuwa kinazidisha deni la taifa, kwamba
hawana ufahamu na kufafanua kuwa katika kuharakisha maendeleo ya nchi,
kukopa ni jambo la kawaida.
Alisema
hata mataifa makubwa yaliyopiga hatua kubwa kwenye maendeleo yamekuwa
yanakopa na akasisitiza kuwa uamuzi wa serikali kwenda nje kukopa
amekuwa anaufanya ili kupata fedha kwa ajili ya kujenga miundombinu
ambayo itaifanya nchi ipige hatua kubwa kimaendeleo.
Alitoa
mfano kuwa hata kama mtu anaeendesha duka ni lazima akakope benki kama
anataka kuendeleza duka lake, kama hatafanya hivyo kwa kuamini kuwa
fedha anazopata kwa kuuza bidhaa zitalitunisha duka hilo basi asubiri
miujiza ya kumpatia faida.
Aliyasema
hayo wakati akizungumzia uamuzi wa serikali yake kuwenda kukopa nje kwa
ajili ya kujenga miundombinu mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa mkongo wa
taifa ambao alisema lengo lake ni kuweka misingi ya miundombinu wakati
taifa linapoelekea kwenye utekelezaji wa ujenzi wa viwanda vya kisasa.
Rais
Kikwete alisema baada ya kufanya uamuzi huo aliamua pia kuwekeza kwenye
utafiti kwa kuhakikisha kuwa Serikal inatenga fedha kwa ajili ya
kuwasomesha watafiti, kununua vifaa vya utafiti na kukarabati vituo vya
utafiti ambayo alisema vingi vilikuwa kwenye hali mbaya.
“Tulianza
na Sh bilioni 10, tunashukuru sasa hivi tupo kwenye Sh bilioni 60 na
naamini kuwa Rais atakayekuja ataendeleze juhudi hizi kwa kutenga fedha
zaidi kwa ajili ya tafiti maana nikiangalia hali ya baadaye ya maendeleo
ya nchi hii inategemea watafiti, wanasayansi na wabunifu,” alisema Rais Kikwete.
Rais
alisema anajivuna kwamba anaondoka madarakani wakati shughuli za
utafiti zimepata uhai na kwamba juhudi zilizofanywa na Serikali yake za
kuwaendeleza wabunifu zimezaa matunda mengi kwani kwa sasa nchi ina
watafiti wazee na vijana wanaofanya mambo makubwa yanayotambulika
kimataifa.
Alisema
fedha zilizotolewa na serikali yake zimesaidia kusomesha watafiti 517
katika kozi za shahada ya uzamili na uzamivu na vituo 20 vimekarabatiwa
na miradi 70 ya utafiti imetekelezwa.
“Ndio maana nasema kiongozi anayekuja asipoliendeleza hili, mwambieni mzee unatuletea matatizo.”
Mkurugenzi
Mkuu wa Costech, Dk Hassan Mshinda alisema kongamano hilo la nne
limewakusanya wanasayansi, watafiti, watunga sera na wabunifu
mbalimbali.
Alisema
mada 80 zitajadiliwa ikiwemo tafiti mbalimbali zilizofanywa na watafiti
wa ndani, kujadiliana changamoto za kupeleka utafiti sokoni na
upatikanaji wa teknolojia na jinsi ya kuhuisha sayansi asili na sayansi
ya kisasa.
Dk
Mshinda alimshukuru Rais Kikwete kwa kujali na kuwapa umuhimu watafiti
kuliko miaka ya nyuma na akasema kuwa anaamini kuwa msingi uliowekwa
utaendelezwa na awamu ijayo.
Alisema
juhudi zilzofanyuwa na Rais Kikwete zimeungwa mkono na nchi za Sweden
na Finland ambao nao sasa wameamua kutoa fedha kusaidia juhudi za
serikali katika kufanya tafiti.
0 comments:
Post a Comment