LATEST POSTS

Friday, October 25, 2013

WAFUGAJI WA KIJIJI CHA LUMBE WALALAMIKIA FAINI YA N'GOMBE WANAYOTOZWA

WAKAZI wa Kijiji cha Lumbe, Kata ya Ukumbisiganga, wilayani Kaliua Mkoani Tabora, wamelalamikia faini ya sh 180,000 wanayotozwa kwa kila ng’ombe anayeingia katika hifadhi ya taifa na kusema faini hiyo haiwatendei haki.
 
Walitoa kauli hiyo hivi karibuni mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatma Mwassa, aliyetaka kujua kero zinazowakabili wafugaji wa kata hizo.
Akizungumza kwa niaba ya wafugaji wenzake, Gunze Pamagi, alisema hivi karibuni baada ya ng’ombe wao zaidi ya 5,000 kuingia kwa bahati mbaya katika hifadhi ya taifa, walikamatwa na kila ng’ombe mmoja alitozwa sh 180,000, badala ya sh 30,000.
 
Walisema hatua hiyo imewashangaza hata kufikia mahali wanahisi watu wa Maliasili hulazimisha kutaifisha mifugo yao kwa nguvu kwa ajili ya kujipatia fedha kutoka kwa wafugaji.
 
“Ni kweli mifugo yetu ilikamatwa katika hifadi ya taifa na baada ya hapo sisi tuko tayari kulipia faini hiyo lakini tunakatishwa tamaa na faini ya sh 180,000, hapa tunaona kama tunaibiwa,” alisema Pamagi.
 
Akijibu malalamiko hayo, Mwassa alisema licha ya kujionea hali hiyo, wafugaji wanapaswa kutambua kuwa zoezi linaloendelea ni la kitaifa na si la mkoa.
Alisema atakachofanya ni kumuomba waziri mwenye dhamana ili wafugaji waweze kulipa faini sitahiki.
 
Sina uamuzi mwingine kwa sasa mpaka niwasiliane na waziri mwenye dhamana ili mlipe faini stahiki, ila tambueni serikali inajua changamoto mnazokabiliana nazo,” alisema Mwassa.
 
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments: