TAKRIBANI siku 9 tangu kutokea kwa uporaji wa silaha
na mauaji ya askari wanne na raia watatu katika Kituo cha Polisi
Stakishari jijini Dar es Salaam, moshi mweupe wa ukweli umenza kufuka.
Gaston polisi aliyenusurika.
Uchunguzi na vyanzo mbalimbali vya habari wakiwemo polisi ambao
hawakutaka kutajwa majina yao, umesaidia timu ya waandishi wetu kubaini
jinsi tukio hilo la kinyama lilivyofanyika.
“Wavamizi inaonesha walipanga zoezi hilo mapema, walijua wapi ghala
la silaha lipo, walisoma pia mazingira ya ulinzi yalivyo pale kituoni
nyakati za usiku,” polisi mmoja wa Stakishari aliyeomba hifadhi ya jina
lake alisema.
UVAMIZI ULIVYOKUWA
Imeleezwa na mashuhuda wa tukio hilo kwamba majira ya saa 5 usiku,
Julai 12, mwaka huu, watu zaidi ya 16 wakiwa na bunduki huku wakiwa
wamevalia makoti meusi, walifika kituoni hapo kwa staili ya kutaka
huduma lakini ghafla walifanya shambulizi la kushtukiza.
“Niliona
pikipiki kama saba zinaingia eneo la kituo, nikadhani ni bodaboda wana
shida kituoni, ghafla nikaanza kusikia milio ya risasi.“Nikakimbia
kuelekea nyumbani kujifungia, baada ya hali kutulia nikarudi kituoni
nikakuta askari na raia wameuawa,” alisema shuhuda wa tukio hilo ambaye
hakupenda kutajwa jina lake.
POLISI, RAIA WALIVYOUAWA
Habari zinadai kuwa baada ya wahalifu hao kufika kituoni hapo, watatu
kati yao walitengeneza mzozo wa kuigiza ili kuwahadaa askari
waliokuwepo kituoni kuwa kufika kwao kulikuwa ni kupata huduma na siyo
vinginevyo.
Inaelezwa kwamba wakati wahalifu hao wakizozana kuelekea mapokezi ya
polisi, wenzao walitawanyika kuzunguka eneo lote la kituo kwa lengo la
kudhibiti usalama.
“Askari mwenye silaha alikuwa mmoja pale kituoni, alipowaona wale
watu watatu aliwauliza shida yao, kabla hajawajibu wakamfyatulia risasi
zilizomjeruhi begani na kifuani.“Alipodondoka chini waliingia mapokezi,
wakakuta polisi wawili na raia watatu, wakawaua wote kwa risasi.
“Askari wengine wawili waliwafuata vyumbani walikokuwa wamekimbilia
kujificha, wakawaua, baadaye wakavunja ghala la silaha na kuiba,” chanzo
chetu kilisema.
RAIA WALIFUATA NINI KITUONI?
Uchunguzi unaonesha kuwa raia watatu waliouawa katika tukio hilo,
walikwenda kituoni hapo usiku kwa ajili ya kupata msaada wa polisi
kufuatia tuhuma za kuibiwa kwa shilingi laki nne kwenye eneo walilokuwa
wamekaa.
Inaelezwa kwamba, Jackline Mdume (marehemu) mkazi wa Manzese, Dar
aliitwa na rafiki yake aliyetajwa kwa jina la utani la Mchakarikaji
mwenyeji wa Tabata Kisukulu ili wakabadilishane mawazo ya kimaisha.
Akiwa na rafiki yake kwa mazungumzo, muuzaji wa vinywaji baridi
aliyekuwa akiwahudumia, alilalamika kuibiwa kiasi cha shilingi laki nne
ambapo mtuhumiwa wake mkuu alikuwa ni Jack.“Baada ya mzozo wa muda mrefu
wakakubaliana waende polisi, Erick Swai (marehemu) alijitolea gari la
kuwapelekea kituoni.
“Baadaye Swai akamuomba kijana mwingine (jina halikupatikana)
amsindikize, wakamchukua na Jack. Mlalamikaji na mwenyeji wa Jack
wakasema wataenda kwa usafiri wao, wakiwa kituoni ndiyo yakatokea hayo
mauaji,” alieleza mtoa habari wetu.
ASKARI MAJERUHI AONGEA
Akiongea na gazeti hili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wiki
iliyopita, askari aliyejeruhiwa katika tukio hilo la kikatili, PC
Gaston Shadrack alisema kupona kwake ni mipango ya Mungu.Akiongea kwa
masikitiko huku Mkuu wa Kituo (OCS) wa Stakishari akiangua kilio baada
ya kumuona askari wake aliyenusurika, Gaston alisimulia kuwa
walitangulia watu wanne wakiwa wamevaa makoti huku wakilumbana kama
watu waliodhulumiana.
Majeruhi huyo alipojaribu kuwahoji, ghafla walichomoa silaha na kuanza mashambulizi makali.
“Mimi baada ya kupigwa risasi niliangukia tumbo hivyo walidhani
nimekufa, hawakuhangaika na mimi tena, waliingia kituoni, wakaua askari
wenzangu pamoja na raia.
“Mmoja kati ya watu wale alikuja nilipokuwa nimeanguka, akanipiga
teke, akawaambia wenzake ‘amekufa’, niliendelea kujilegeza huku
nikiilalia bunduki yangu wasiione.
“Sikuwa na nguvu za kuinuka, walipomaliza uhalifu wao walitoka kwa tahadhari kubwa, niliendelea kutulia pale chini.
“Wakati wanaondoka pikipiki moja iligoma kuwaka, nikafyatua risasi mbili zilizompiga mmoja wao, akadondoka,” alisema PC Gaston.
WAHALIFU WALIONDOKAJE?
Habari kutoka eneo la tukio zinadai kuwa baada ya kufanya mauaji na
kukusanya silaha, wahalifu hao walitoweka kupitia njia tofautitofauti.
Aidha, inadaiwa kuwa rundo la bunduki walizopora waliziingiza kwenye
gari aina ya Toyota Noah la rangi nyeusi ambalo lilikuja na kuegesha
karibu na kituo hicho.Inaelezwa kuwa mbali na bunduki, wahalifu hao
walifanikiwa kuiba pia radio ya mawasiliano ya kipolisi (radio call)
ambayo waliitumia kujua namna walivyokuwa wakifuatiliwa na vyombo vya
usalama.
SILAHA ZINAZOIBWA ZINAPELEKWA WAPI?
Kitendawili cha wapi silaha zinazoibwa zinapelekwa na kwa kazi gani,
bado hakijateguliwa ingawa yamekuwepo madai kuwa kuna kundi la watu
ambalo linakusanya silaha hizo kwa lengo la kufanyia uhalifu mkubwa.
Baadhi
ya wananchi ambao hawakupenda kutajwa majina yao, waliviomba vyombo ya
usalama kuyachunguza mapori ya Kisarawe na Mkuranga, Mkoa wa Pwani na
mkoani Morogoro kwa madai kuwa misitu hiyo inatumiwa na wahalifu kupata
mafunzo na kuhifadhi silaha.
“Mambo mengine tunaogopa kuyazungumza waziwazi lakini serikali
ikiamua kufanya uchunguzi kwenye misitu mikubwa pamoja na kufuatilia
nyendo za baadhi ya mashirika ya dini, watabaini mambo mazito sana,”
alisema mwananchi mmoja mkazi wa Kisarawe alipozungumza na gazeti hili.
FAMILIA ZA ASKARI WALIOUAWA ZANENA
Mke wa marehemu CPL Peter Sabuni mwenye namba E 1279, Mary Sabuni
alishangazwa na mauaji ya mumewe huku akijiuliza kama ataweza kuwatunza
watoto akiwa peke yake.“Nipo kwenye wakati mgumu, mtu niliyekuwa
namtegemea ameuawa kinyama, sijui nitawalea vipi wanangu,” alisema Mary
huku akiangua kilio.
Naye
ndugu wa CPL Gaudiani Cyprian ambaye alijitambulisha kwa jina moja la
David, alisema wamepata msiba mzito na ambao hauelezeki.“Nafikiri unajua
kuwa baada ya msiba wa ndugu yangu kutokea, mama yetu alipopata taarifa
alidondoka na kufariki dunia, hivi ninavyokwambia tuna misiba miwili
mizito.”
Aidha mke wa SGT Adam Nyamuhanga mwenye namba D 69652, Jesca Adam
alisema haamini kilichotokea, anaona kama ni ndoto ya mchana.“Mume wangu
aliniaga anakwenda kazini atarudi kesho, mpaka usiku saa tatu siku ya
tukio niliwasiliana naye, leo naambiwa ameuawa! Siamini,” alisema.
Naye mdogo wa marehemu H 1030, PC Antony Komu aliyejitambulisha kwa
jina la ‘Komu Mdogo’ alisema amepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha
kaka yake.“Kaka yangu alikuwa ndiyo kila kitu kwangu, ndiye alikuwa
akinisomesha, sasa sijui nitasomaje, naona giza kwenye maisha yangu,”
alisema.
KAMISHINA KOVA HUYU HAPA
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Kipolisi Dar es
Salaam, Kamishna Suleiman Kova wakati anawaaga wapiganaji hao, alisema:
“Nakemea na kulaani kitendo hiki cha kinyama na tutahakikisha
waliohusika wanakamatwa wote kwa muda mfupi. Pia tutahakikisha serikali
inalipa mafao kwa kila askari aliyepoteza maisha.”
OMBI KUTOKA KWA POLISI
Baadhi ya maofisa wa polisi wameiomba serikali kuangalia namna ya
kuwasaidia watoto wa marehemu ili kuwawezesha kupata haki zao za msingi
likiwemo suala la elimu.
“Tumesikia Kamishna Kova amesema atasimamia mafao ya marehemu, hilo
ni sawa lakini waangalie jinsi ya kuwasaidia watoto hasa wale wadogo
ambao wazazi wao wamepoteza maisha wakilitumikia taifa,” alisema polisi
mmoja kwa sharti la kutotajwa jina lake.
Source: Global publishers
0 comments:
Post a Comment