IKIWA ni takriban zaidi ya wiki moja imepita baada
ya Mkurugenzi wa Mabasi ya J4 Express, Juma Mahende ‘J4” kudaiwa kuua
kwa kuwapiga risasi wafanyabiashara wenzake wawili, kigogo huyo amebanwa
na polisi kuhusiana na mauaji hayo.
Ally Mohamed enzi za uhai wake.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, DCP Charles Mkumbo amethibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa polisi bado wanafanya uchunguzi
wa ndani juu ya tukio hilo huku mtuhumiwa wakimshikilia.
“Tunafanya uchunguzi wa ndani ili kubaini sababu za J4 kuwaua watu
hao…waliuawa kikatili na silaha iliyotumika ni bastola aina ya Brown
yenye namba 00092890,” alisema Mkumbo.
J4 ambaye mabasi yake yanayofanya safari kutoka Mwanza kwenda mikoa
mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi, anadaiwa kuwapiga risasi
wafanyabiashara wawili, Ally Mohamed Abeid na Claude Steven Sikalwanda
wakazi wa Jiji la Mwanza Julai 13, mwaka huku chanzo cha tukio hilo
kikitajwa kuwa ni kudhulumiana katika biashara.
Cloud Steven enzi za uhai wake.
Gazeti hili lililifuatilia tukio hilo ambalo limekuwa gumzo mjini
Mwanza ambapo liliweza kumpata Ramadhan Mohamed Abeid ambaye ni mdogo
wa Ally Mohamed aliyeuawa na alisimulia kama ifuatavyo:
“Siku ya tukio hilo kaka yangu alinipigia simu saa 8:30 mchana
akinitaka nimpelekee gari alilotaka kununua wakati huo akiwa Nyakato,
wilayani Nyamagana jijini hapa.
“Nilipofika nilimkuta kaka yangu akiwa na Claude pamoja na mtu ambaye
namfahamu kwa sura ambapo waliku wa wakimsubiri J4 ili awapatie
fedha kutokana na biashara waliyokuwa wamefanya, tulikaa hapo mpaka saa
11 jioni.
“Walipoona J4 amechelewa kaka yangu aliomba twende mjini kutengeneza
simu yake wakati huo wakiendelea kuwasiliana na J4 kuhusu biashara zao
lakini alisikika kulalamika sana juu ya fedha zake, ilipofika saa moja
kasoro jioni nikaomba kwenda kufuturu, nikawaacha wakisubiri simu kwa
fundi huyo ndiyo ukawa mwisho wa kuonana nao kwani walikuwa pamoja,”
alisema Ramadhani.
Ally mohamed akizikwa.
Naye dada wa Claude, Aziza Steven alisema usiku huo marehemu
waliwahi kurudi nyumbani wakiwa katika hali ya kawaida na waliandaliwa
chakula cha usiku wakala lakini Ally Abeid wakati anakula alikuwa
anapigiwa simu na J4 akimtaka wakaonane ili kupeana pesa walizokuwa
wamefanya biashara zao.
“Marehemu hakukubali kwenda usiku huo, akamtaka waonane kesho yake
asubuhi, kutokana na mvutano huo Ally alivaa suruali na shati jeupe na
miguuni alivaa ndala wakaondoka wote huku Ally akisema wanaenda kuchukua
shilingi milioni 25 kwa J4 walizokuwa wamekubaliana katika biashara
zao, ikawa mara yao ya mwisho kuongea na kaka yao.
Baada ya Ally na Steven kuuawa ndugu zao Ramadhani na Aziza wakiwa
pamoja mmoja wao alisema: “ Sisi tulipata taarifa usiku kuwa ndugu zetu
wameuawa, tulikusanyika na saa 12 asubuhi tulikwenda Hospitali ya Rufaa
Bugando tukaona miili yao ndipo tukaanza kufuata taratibu za kuweza
kupata maelezo ya kitaalamu.
“Daktari mmoja alisema baada ya kuchunguza miili ya ndugu zetu,
iligundulika Ally alipigwa risasi tatu kifuani na Steven alipigwa risasi
moja kifuani na kusababisha vifo vyao papo hapo,” alisema Ramadhani.
Inadaiwa kuwa mara baada ya J4 kuwaua watu hao maeneo ya Nyakato
kulikuwa na baadhi ya majirani ambao hawakuwa mbali sana na eneo la
tukio waliliambia gazeti hili kwa masharti ya kutotaja majina yao kuwa
risasi ndizo zilizowashitua wakaenda eneo la tukio.
“Tulipofika nyumbani kwa J4 tulimkuta akiwa amesimama karibu na hao
marehemu na baada ya muda mfupi polisi walifika eneo la tukio
wakamkamata na kumuingiza kwenye gari na maiti kisha wakaelekea
Hospitali ya Bugando,” alisema shuhuda mmoja kwa sharti la kutotajwa
jina.
Marehemu Claude alikuwa ni mkazi wa Nyansaka nje kidogo ya Jiji la
Mwanza, alikuwa mfanyabiashara wa nafaka, ameacha mke pamoja na watoto
wa nne, kwa upande wa Ally alikuwa akiishi maeneo ya Igoma na alikuwa
akijishughulisha na shughuli za ujenzi lakini pia alikuwa mfanyabiashara
wa baa na gesti maeneo ya Igoma, ameacha watoto watatu na mke.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Malongo (pichani) amezihakikishia
familia na ndugu wa marehemu waliouawa kuwa watahakikisha haki
inatendeka kwa mshtakiwa kwani hakuna mtu ambaye yupo juu ya sheria.
0 comments:
Post a Comment